1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

OSLO: Mshindi wa tuzo la amani la Nobel 2006, Muhammad Yunus, aelezea furaha yake

13 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CD3G

Tuzo la amani la Nobel mwaka huu wa 2006 limetunukiwa raia wa Bangladesh, Muhammad Yunus, na banki yake ya Grameen Bank ambayo inatoa mikopo kwa ma milioni ya watu maskini nchini mwake. Muhammad Yunus, mwenye umri wa miaka 66, amekabidhiwa tuzo hilo sio tu kwa shughuli hizo za kuwaendeleza watu kiuchumi, bali pia kuhusu mchango wake kuelekea demokrasia na haki za binaadamu, imesema kamati ya Nobel mjini Oslo nchini Norway.

Baada ya kutangazwa mshindi wa tuzo hilo, Muhammad Yunus, alisema anayo furaha kubwa:

´´ Hii ni habari nzuri, sio tu kwa mimi binafsi, bali pia kwa ma milioni ya watu wanaotoa au wanaopewa mikopo midogo midogo ya kujiendeleza. Ninafurahi sana na tena sana .

Hiyo itatupa nguvu zaidi katika vuguvugu letu´´.

Benki ya Muhammad Yunus, Grameen, hutoa mikopo hasa kwa akinamama bila dhamana ili waweze kuanza miradi yao ya biashara ndogo ndogo.Serikali ya Ujerumani imekaribisha uteuzi huo. Msemaji wa kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Thomas Steg, amesema Benki ya Grameen, ingefaa kuwa mfano.