1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ouattara aitisha maandamano ya amani Cote d´Ivoire

15 Desemba 2010

Ouattara anataka kudhibiti vyombo vya dola aweze kutawala nchini. Jumuiya ya kimataifa inamtambua Ouattara kama rais mpya wa Cote d´Ivoire

https://p.dw.com/p/QYul
Kiongozi wa upinzani wa Cote d´Ivoire, Alassane OuattaraPicha: AP

Kiongozi wa upinzani nchini Cote d'Ivoire Alassane Ouattara ameimarisha harakati zake kuchukua madaraka nchini humo, kwa kuwaagiza wananchi wa Cote d'Ivoire kufanya maandamano ili achukue uongozi wa afisi za serikali nchini humo. Jumuiya ya kimataifa pamoja na Umoja wa Mataifa unamtambua Ouattara kama mshindi wa uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo mwezi uliopita, lakini Laurent Gbagbo, ambaye alijitangaza rais, amekatalia madarakani.

Tangu jana hali nchini Cote d'Ivoire imeonekana inaanza kuchukua mwelekeo mwingine tangu mgogoro wa kisiasa kuanza wiki mbili zilizopita.

Kambi ya Alassane Ouattara sasa imewataka wafuasi wake kufanya maandamano ya amani ili kiongozi huyo aweze kuchukua uongozi wa kituo cha kitaifa cha televisheni pamoja na afisi za serikali nchini Cote d'Ivoire. Katika mji wa Tiebissou, maafisa wa usalama wanaomuunga mkono Gbagbo walifyatua mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya wafuasi wa Ouattara.

Cote d'Ivoire imegawika mara mbili - eneo la Kaskazini lenye idadi kubwa ya Waislamu na Kusini wanakokaa Wakristo wengi, tangu jaribio la kumuondoa madarakani Laurent Gbagbo kukosa kufaulu mwaka wa 2002. Sasa mgogoro kati ya Gbagbo anayetokea kusini na Ouattara kutoka Kaskazini umechochea zaidi uhasama nchini humo.

Katika taarifa yake aliyoitoa katika hoteli anayoishi na ambayo ameigeuza kuwa afisi ya serikali yake mbadala, inayolindwa na Umoja wa Mataifa, Ouattara amewataka wafuasi wake kesho kuandamana hadi katika makao ya televisheni ya kitaifa RTI na baadaye siku ya Ijumaa iwe zamu ya kuandamana hadi katika afisi za mawaziri wa mpinzani wake Gbagbo.

Elfenbeinküste Präsident Laurent Gbagbo
Rais Laurent Gbagbo wa Cote d´IvoirePicha: AP

Taarifa hiyo iliotiwa saini na chama cha Ouattara pamoja na chama cha waasi wa zamani New Forces, FN, kiliwataka wananchi wa Cote d'Ivoire kuandamana na serikali hiyo ya Ouattara hadi katika afisi ya Waziri Mkuu nchini Cote d'Ivoire ili waanze kazi. Afisi hiyo ya Waziri Mkuu mjini Abidjan iko chini ya utawala wa wanajeshi wanaomuunga mkono Gbgabo na kwa sasa inamilikiwa na Ake N'Gbo, chaguo la Gbagbo la Waziri Mkuu wa Cote d'Ivoire.

Chaguo la Ouattara la Waziri Mkuu, kamanda wa FN Guillaume Soro amesema anapanga kuitisha mkutano wa baraza la mawaziri katika afisi hizo za Waziri Mkuu siku ya Ijumaa. Soro lakini hayasema bayana iwapo atatumia nguvu endapo wanajeshi wanaomuunga mkono Gbagbo watakataa aingie katika afisi hizo.

Wakati huo huo, Waziri wa mambo ya nje katika serikali ya Gbgabo amesema wapatanishi wa Kiafrika watawasili nchini humo hivi karibuni kujaribu kuutanzua mkwamo huo wa kisiasa. Kulingana na Waziri huyo uamuzi huo ulipendekezwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, bwana Ban Ki Moon, na Umoja wa Afrika unapanga kutuma ujumbe wa upatanishi Cote d'Ivoire.

Mwandishi: Munira Muhammad/AFPE; rtre

Mhariri: Josephat Charo