1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Padri Christian Führer na mapinduzi ya amani.

3 Novemba 2009

Kanisa la Nikolaikirche -Leipzig-miaka 20 iliopita.

https://p.dw.com/p/KCkq
Padri Christian Führer (Nikolaikirche)Picha: picture-alliance/ ZB

Padri Christian Führer,ni mmoja kati ya "mashujaa wakubwa" wa mapinduzi ya amani katika ile iliokua Ujerumani Mashariki. Waziri wa usafiri na mawasiliano wa Ujerumani, Wolfgang Tiefensee, meya wa zamani wa jiji la Leipzig, alimuita hivyo padri Christian Führer, wakati anatunzwa nishani ya "HANS-BÖCKLER MEDAILLE" hata ikiwa binafsi, hangependa kuitwa hivyo.

Maandamano ya kila Jumatatu mjini Leipzig,ambayo padri huyo wa madhehebu ya kiinjili alichangia mno kuyaandaa,yalipalilia mno mapinduzi baridi yaliopelekea kuporomoka kwa ile iliokuwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujerumani (GDR).

Padri Christian Führer,aliezaliwa 1943,alikulia katika Jumba la mapadri huko Sachsen na hakukawia kuamua kwamba ,shabaha yake ni kujifunza dini tena katika nchi ambayo ikiangalia dini kama "kasumba ya wanadamu"

Kwa muda wa miaka 28,Christian Führer,alikuwa padri katika Kanisa la NIKOLAIKIRCHE,mjini Leipzig, hadi alipostaafu Machi, mwaka jana.

"Padri alietoka mitaani analiacha zizi lake la historia"-Hivyo, ndivyo gazeti la NEW YORK TIMES liliandika wakati ule.Nae Padri Christian Führer, alisema:

"Nikihisi nimevutwa upande huo wa kuwatetea wanyonge."Mdomo wa wasio na sauti ndio lililokuwa jukumu langu .Hatufuati kile wote wanachofanya,bali tunaamua kile kinachohitajika kufanywa.Hili ndilo darasa nililojifunza kutoka kwa Yesu.Yesu angesema nini ? Nini tufanye katika hali hii ? Kwa maoni yangu ,Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujerumani (GDR) ilikuwa kambi ya miaka 40 ya mtihani kushikamana na dini."Padri-mstaafu Christian Führer akaongeza:

"Wakati wa mafunzo yangu katika chuo kikuu na kama mwanafunzi majira ya kiangazi nikifanya kazi katika viwanda mbali mbali, na mara nyingi , nikitembea kwa mguu.Kila mara ,watu wakisikia ninajifunza dini na nina azma ya kuwa padri ,yakianza mazungumzo.Mazungumzo hayo na watu wa kawaida,ndio yameathiri mno maisha yangu na pia yakageuka "chuo kikuu changu" cha kujifunza.

1986,padri Christiian Führer,alitundika biramu katika kanisa lake lililosema: "Kanisa la Nikolai limefungua mlango wake kwa wote."

Baada ya muda ,watu wakaitikia mwito wake : vijana ambao hawakuridhika na hali za maisha,wapinzani wa utawala na wale waliotaka kuihama nchi.Yeyote aliefika hapo,alisikilizwa kilio chake,akatulizwa moyo,bila kujali alikuwa mkristo au la.

Deutschland DDR Jahrestag Leipzig Montagsdemonstration Nikolaikirche 1989
Umma wa watu ulijikusanya katika kanisa la Nikolai kirche,Leipzig hapo Oktoba 9,1989Picha: AP

Anakumbusha Padri Führer kwamba kila kitu kilichojengwa na serikali wakati ule kilikuwa na shabaha ya kupalilia woga na hofu kwa raia ili wachunge wafanyao .Lakini imani ya dini daima ilikuwa kubwa zaidi kuliko hofu zao.Hivyo, zikavuka mipaka iliowekwa isivukwe.

Kanisa hii leo ,asema padri huyo , limewasaidia raia wa Ujerumani Mashariki wakati ule kujiamini .Liliwapatia nguvu za kuthubutu kuandamana kwa amani bila kujali hatari ya kupoteza maisha yao . Oktoba 9, 1989, umma wa watu 70.000 ukajikusanya katika Kanisa hilo la Nikolai-kirche mjini Leipzig, kwa maandamano makubwa mno kuanzisha hayo "mapinduzi ya amani" yaliopelekea kuanguka kwa utawala wa iliokuwa Ujerumani Mashariki .

Mtayarishi: Ramadhan Ali

Mhariri:Othman,Miraji