1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pambano la der Klassiker Bayern na BVB lapoteza ladha yake

Admin.WagnerD11 Novemba 2019

Pambano  linalojulikana  kama  Der Klassiker nchini  Ujerumani kati ya  Bayern na Borussia  Dortmund lageuka  kuwa  la  upande mmoja.

https://p.dw.com/p/3SqTK
Fußball Bundesliga FC Bayern München - Borussia Dortmund
Picha: picture-alliance/dpa/S. Hoppe

Ligi  ya  Ujerumani  Bundesliga  imeendelea  wiki  hii  ikitimiza mchezo wake  wa  11, ambapo  hadi sasa  vinara  ni Borussia Moenchengladbach, ambayo  hapo  jana  jioni  iliizaba  Werder Bremen  kwa  mabao 3-1 na  kufungua  mwanya  wa  pointi 4 wakiwa na  pointi 25 wakiitangulia  RB Leipzig inayoshika  nafasi ya  pili ikiwa  na  pointi 21.

Mlinda  mlango wa Gladbach  Yann Sommer anasifu  mafanikio  ya timu  yake hadi sasa.

Fußball Bundesliga Bayer 04 Leverkusen - Borussia Mönchengladbach Torwart Yann Sommer
Mlinda mlango wa Borussia Moenchengladbach Yann SommerPicha: Imago Images/Sven Simon/A. Waelischmiller

"Bila shaka inapendeza, wakati  juhudi  zetu zimefanikiwa na  kwa kuwa tumeonesha  juhudi  katika  uwanja  wetu wa  nyumbani  wa  Borrusia Park. Tunawekeza nguvu  nyingi sana,katika  mchezo. Tuna uwezo mkubwa  wa  kumalizia. Nafikiri , kwa  hivi  sasa  pia  kuwa  ndio ufunguo wa  mafanikio. Tunahitaji  magoli, kwa  kuwa  tunacheza  mpira, ambao una kaa  katika  miguu  yetu. Na iwapo katika  hali  hii  tunapata mafanikio, tunaweza  kila  mara  kupumzika  wakati mchezo ukiendelea. Kwa hivi  sasa  kila  kitu kinakwenda  vizuri."

Mabingwa watetezi Bayern Munich wanashika  nafasi  ya  tatu  katika msimamo wa ligi, baada  ya  kuirarua  Borussia  Dortmund  siku ya Jumamosi kwa  mabao 4-0. Mchezo  ambao unaangaliwa  hapa Ujerumani kama  mchezo wa  mafahali wawili  der Klassiker ulimalizika, kwa  aina ya mpambano wa kati ya  mbuzi na  ng'ombe kwani Borussia  Dortmund  kwa mara ya  tano sasa wanachezea  kichapo cha  hali  ya  juu  katika  uwanja wa  Allianz Arena  nyumbani  kwa  Bayern. Nini  tatizo  la  Borussia Dortmund wakutanapo  na  Bayern katika  uwanja  wa  Allianz Arena: Swali hiyo  analijibu mshambuliaji  wa  Bayern Munich  Thomas Mueller.

Fußball Bundesliga FC Bayern München - Borussia Dortmund
Thomas Mueller wa Bayern akiwaelekeza wenzake uwanjaniPicha: Getty Images/Bongarts/A. Hassenstein

„Ndivyo walivyo, kwa  kweli wakati BVB wanakutana  na  timu  yetu, wana watu wengi wataalamu, ambao kimbinu ni wazuri sana, lakini nafikiri , mchanganyiko  huo unaleta tu sura ya kimwili na unadhifu. Ni lazima  uwe na  kikosi chenye mshikamano katika  uwanja na  leo mtu anaweza  kusema,  tulikuwa na kikosi kilichochangamka na kufanya juhudi tukiwa na  mpira, lakini  pia  bila  mpira na  hatukuwapa  Dortmund nafasi ya  kupumua."

Hayo ndio masaibu  yaliyowakuta  Borussia  Dortmund mjini  Munich mwishoni  mwa  juma, ambapo wangependa kusahau  haraka. Dortmund iko hivi  sasa  katika  nafasi ya 6 ikiwa  na  pointi 19 na  mchezo wao  na bayern haukuwapendeza  mashabiki  na  pia  viongozi  wa  timu  hiyo. Huyu  hapa  mkurugenzi wa  spoti  wa  Borussia  Dortmund Michael Zorc:

„Tumefanya makosa mengi kirahisi katika mchezo wetu wa kumiliki mpira, tumewarahisishia  sana Bayern. Na hatukuwamo  katika mchezo kabisa. Mwishowe  waweza kusema, hatukuonesha juhudi. Hakukuwapo na juhudi yoyote katika mchezo wetu hii  leo."

timu iliyofaidika  sana  na  mchezo  huu  wa  11  katika  Bundesliga  ni pamoja  na SC Freiburg ambayo  iliiangusha  Eintracht Frankfurt nyumbani kwa  bao 1-0  na  kujikingia  pointi 21  katika  michezo 11 hatua  ambayo ni  mafanikio  makubwa  ya  kwanza  ya  Freiburg  katika  muda  wa  miaka zaidi ya  20. Freiburg imepanda  hadi  nafasi ya 4  ya  msimamo wa  ligi na huyu  hapa  ni  kocha  wa  timu  hiyo Christian Streich:

SC Freiburg - Eintracht Frankfurt
Kocha wa timu ya SC Freiburg Christian Streich akiwa amelala chini baada ya kuangushwa na mchezaji wa Frankfurt David Abraham Picha: picture-alliance/dpa/P. Seeger

"Huwezi  kuamini , tumefurahi  kiasi  gani. Tuna  pointi 21 baada  ya michezo 11. Kwetu sisi  hilo ni  jambo la ajabu, na  hivyo ndivyo  ilivyo, kwamba , pointi  hizo  hatukuiba. Tuna timu yenye kujielewa. Leo tulikuwa  sawa. Pengine Frankfurt walipata  nafasi  bora  zaidi  za  kupata mabao, lakini  sisi  ndio tulifunga goli. Ndivyo ilivyo ilishawahi  kutokea."

Wakati  huo  huo  nahodha  wa  Eintracht Frankfurt David Abraham anakabiliwa  na  adhabu  kali  kutoka  katika  shirikisho  la  kandanda  la Ujerumani  DFB baada  ya  kumwangusha  chini kocha  wa  Freburg Christian Streich  katika  pambano  lao  la  jana  Jumapili  la  Bundesliga. Abraham  alioneshwa  kadi  nyekundu  na  mwamuzi  kwa  tukio  hilo katika  dakika  za  mwisho  za  mchezo huo ambao Freiburg  ilishinda  kwa bao 1-0. Abraham  anaweza  kukabiliwa  na kukaa  nje  ya  uwanja  kwa muda  mrefu.