1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa amaliza ziara ya Uingereza kwa mafanikio

20 Septemba 2010

Ziara ya Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Benedikt wa 16, nchini Uingereza imekuwa ya mafanikio zaidi kuliko vile vyombo vingi vya habari vya nchi hiyo vilivyokuwa vimekisia hapo mwanzoni.

https://p.dw.com/p/PHUh
Papa Benedict XVI akiwapungia mkono waumini waliokusanyika mjini Birmingham, Uingereza, kumpokea
Papa Benedict XVI akiwapungia mkono waumini waliokusanyika mjini Birmingham, Uingereza, kumpokeaPicha: AP

Picha ya Awali

Picha ambayo vyombo vya habari vya Uingereza ilikuwa inajaribu kuichora kabla ya ziara ya Papa Benedikt wa 16 nchini humo, ilikuwa inaonesha kila dalili ya woga. Picha hii ilikuwa imemuonesha Mkuu huyu wa Kanisa la Kikatoliki duniani, kama mtu anayekwenda kuitembelea nchi ambayo hapendwi na anachukiwa sana.

Ziara ikapewa kila jina la kuvunja moyo. Wengine waliita "ziara ngumu kabisa" kuwahi kufanywa na kiongozi huyo ambayo ingelikuwa na makaribisho yaliyojaa shaka kutoka kwa wenyeji wake. Picha hii ikawafanya watu wajiulize, kwa nini Papa anajilazimisha kuzuru nchi hii badala ya kubakia tu kwenye makaazi yake ya Vatican?

Papa Benedict XVI na Malkia Elizabeth II wa Uingereza wakiwa Edinburgh Scotland
Papa Benedict XVI na Malkia Elizabeth II wa Uingereza wakiwa Edinburgh, ScotlandPicha: AP

Maoni Yabadilika

Lakini sasa Papa amethibitisha kwamba, ziara yake inaweza kuwa na matunda tafauti na yale ambayo vyombo vingi vya habari viliyatazamia. Maelfu ya Waingereza walijitokeza kumpokea, kumkaribisha na kusali naye pamoja katika mitaa mbalimbali ya miji ya London, Edinburgh, Glasgow na Birmingham.

Picha za waumini wanaosali na kuimba pamoja na Papa katika vyombo vya habari zilikuwa nyingi zaidi kuliko zile za waandamanaji wanaompinga. Waingereza wengi wanaweza kuwa waliridhishwa na namna ambavyo Papa aliiendesha na kuimaliza ziara yake, katika nchi ambayo anajua vyema kwamba baadhi ya mafundisho ya Kanisa lake yanapingwa vikali. Ziara hii, kwa vyovyote, imeonesha kiwango kikubwa cha uhuru wa mawazo na kuvumiliana kutoka pande zote.

Msimamo wa Papa Kuhusu Kashfa za Udhalilishaji wa Watoto

Ni katika ziara hii, ndipo ambapo kwa mara kwa kwanza, Papa amezungumzia wazi msimamo wake juu ya kashfa zinazoliandama Kanisa lake juu kuhusu vitendo vya udhalilishaji watoto vinavyodaiwa kufanywa na viongozi wa Kanisa hilo. Ameelezea masikitiko yake kwa kashfa hizo na akaitaka sheria ichukue mkondo wake. Hii ni hatua kubwa sana, hasa kama maneno haya yatafuatiwa na vitendo.

Ujumbe wa Papa

Ujumbe wa Papa kwa watu wa Uingereza ulikuwa wazi, kwamba jukumu la waumini halipo kwenye kuishi maisha ya ukwasi, kutakiana kheri za Krismas na za sikukuu tu, bali lipo kwenye kushiriki na kusimamia mwenendo mzima wa maisha.

Kabla ya ziara hii, Waingereza wengi walikuwa wana shaka na msimamo wa Papa, lakini sasa wengi wao wamepata uelewa mpya kwa kiongozi huyu. Sasa huyu ni Papa ambaye anatafuta suluhu na Kanisa la Kianglikana. Sasa huyu ni Papa ambaye anatokea Ujerumani ambayo Uingereza iliipiga vita vya kupambana na Unazi.

Mafanikio Makubwa

Papa Benedikt ameweza kujithibitisha, pasi na tone la shaka, kwamba yeye si mkuu wa chombo cha utawala chenye nguvu na kikandamizaji, kama wapinzani wake wengine wanavyoona, bali ni kiongozi mkuu wa Kanisa ambalo lina makosa na mapungufu yake.

Papa amemaliza ziara yake akiwa amejikusanyia sifa na heshima ya hali ya juu, kiasi ya kwamba anaweza kuiweka ziara hii kwenye kitabu cha historia ya mafanikio.

Mwandishi: Lochner,Stefan/ZR/Mohamed Khelef

Mpitiaji: Mohammed Abdul-Rahman