1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa awasili Jamhuri ya Afrika ya Kati akitokea Uganda

29 Novemba 2015

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis amekamilisha ziara yake nchini Uganda na asubuhi ya leo (29.11.2015) alielekea Jamhuri ya afrika ya kati alikowasili muda mfupi uliopita.

https://p.dw.com/p/1HEDP
Papa alipowasili katika madhabahu ya Namugongo Uganda kwa sala maalum
Papa alipowasili katika madhabahu ya Namugongo Uganda kwa sala maalumPicha: Reuters/J. Akena

Papa Francis aliwasili mapema leo(29.11.2015) katika jamhuri ya Afrika ya Kati alikopokelewa kwa shangwe na jamii zote za waislamu na wakristo katika mji mkuu Bangui.Ni ziara ya kwanza ya kiongozi huyo wa kidini katika nchi inayokabiliwa na mgogoro na vita.

Papa anatarajiwa kutoa ujumbe wa maridhiano na mshikamano kwa watu wa taifa hilo wanaoendelea kushuhudia hali ya mgogoro unaosababisha umwagikaji wa damu.

Ukarimu wa Waganda

Amkkiwa nchini Uganda katika ziara ya siku tatu, papa alitoa mwito kwa jamii na viongozi wa nchi hiyo kujenga mazingira bora ya umoja,haki kwa wote na kuwezesha kila mtu kunufaika kutokana na raslimali za nchi.

Akitoa tathmini ya ziara hiyo ya siku tatu, msemaji wa papa Kasisi Federico Lombardi amefahamisha kuwa papa amefurahia mapokezi na ukarimu waliomwonyesha waganda pamoja na hali nzuri ya hewa iliyokuwepo.

Papa alipokutana na watawa na mapadiri nchini Uganda
Papa alipokutana na watawa na mapadiri nchini UgandaPicha: Reuters/J. Akena

''Papa alishangazwa na dhati ya waganda waliomlaki na aliguswa sana na jinsi vijana waliomshangilia hivyo anaweza kushawishiwa kuzuru nchi hii tena''

Kumbukumbu

Kwa mujibu wa msemaji huyo, papa Francis hatasahau kiwango cha juu cha imani alichoshuhudia miongoni mwa waganda na ndiyo maana anashangaa kwa nini viongozi wa taifa hilo wasitumie imani hiyo kuwa fursa ya kujenga mazingira ya umoja, maridhiani na haki kwa wote kisiasa, kijamii na kiuchumi.

''Papa amefahamisha kuwa mafunzo ya kikatoliki ni kichochezi kikubwa kwa maadili hivyo anawahimiza viongozi wote kuwa na wajibu wa kujenga mazingira bora kwa watu wao, kuhakikisha amani, haki na kuwajali hasa masikini ili tume na jamii inayozingatia maridhiano iwe katika mazingira bora''

Kwa mtazamo wa waganda wengi, papa Francis ameacha si tu kumbukumbu za daima miongoni mwao bali nasaha muhimu kila mtu kuwa na matumaini licha ya changamoto za maisha na kuwajali wasiobahatika katika jamii. Hapo jana alipozuru makao ya wakongwe wasiojiweza katika eneo la Nalukolongo papa alifikia hadi kuwabusu wale wote walioshindwa kutoka nje ya mabweni yao kuja kumlaki.

Aidha, jana jumamosi jioni papa alikutana na kufanya mazungumzo ya faragha pia na mfalme wa jamii ya Baganda Ronald Muwenda Mutebi.Hii imefasiliwa kuwa ishara kuwa viongozi wa tabaka mbalimbali wana imani kwamba kiongozi huyo wa kanisa katoliki ana ushawishi mkubwa duniani na anaweza kuvutia jamii ya ulimwengu kuchangia kwa mipango ya kutatua mizozo ya kivita, kisiasa na kijamii.

Papa akipokelewa alipowasili kukutana na rais wa Uganda Yoweri Museveni ikulu,Kampala
Papa akipokelewa alipowasili kukutana na rais wa Uganda Yoweri Museveni ikulu,KampalaPicha: Reuters/S. Rellandini

Msemaji wa papa ana mtazamo kuwa ni kwa ajili hii ndipo papa anataraji kuanzisha harakati mpya kuleta amani na maridhiano katika jamhuri ya afrika ya kati ambako atatembelea kambi za wakimbizi pamoja na msikiti mmoja.

''Kama ilivyo ada kwake papa anataka kujihusisha moja kwa moja na watu wa nchi hiyo kuwahakikishia kwamba anawajali na kuwapenda wanaoteseka''

Ikumbukwe kuwa papa Francis alianza ziara yake ya kwanza barani afrika kwa kuitembelea Kenya siku ya jumatano na ataondoka jamhuri ya afrika ya kati baada ya muda wa masaa 33 kurudi Vatican.

Mwandishi: Emmanuel Lubega

Mhariri Yusuf Saumu