1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis akanusha kuwa anapanga kujiuzulu hivi karibuni

Iddi Ssessanga
4 Julai 2022

Papa Francis amekanusha ripoti kwamba anapanga kujiuzulu hivi karibuni, akisema yuko njiani kuizuru Canada mwezi huu na anatumai kuweza kwenda Moscow na Kyiv haraka iwezekanavyo baada ya hapo.

https://p.dw.com/p/4DcsR
Vatikan l Papst Franziskus im Rollstuhl
Picha: Stefano Spaziani/picture alliance

Katika mahojiano maalumu kwenye makazi yake mjini Vatican, Papa Francis pia alikanusha uvumi kwamba ana ugonjwa wa saratani, na kutania kwamba madaktari wake "hawakuniambia chochote kuhusu hilo", na kwa mara ya kwanza alitoa ufafanuzi kuhusu hali ya goti lake ambalo limemuziwia kutekeleza baadhi ya majukumu yake.

Katika mazungumzo ya dakika 90 Jumamosi mchana, yaliofanyika kwa lugha ya kitaliana bila kuwepo wasaidizi, kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani mwenye umri wa miaka 85, pia alirudia ukosoaji wake wa utoaji mimba kufuatia hukumu ya mahakama ya juu ya Marekani mwezi uliopita.

Soma pia: Watu 920 wafa kwa tetemko la ardhi Afghanistan

Uvumi umeenea katika vyombo vya habari kwamba mfululizo wa matukio yanayopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Agosti, ikiwemo mikutano na makadinali wa dunia kujadili katiba mpya ya Vatican, sherehe ya kuwasimika makadinali wapya, na ziara katika mji wa Italia wa L'Aquila, vinaweza kugubika tangazo la kujiuzulu.

Vatikan Papst Franziskus mit Christen aus dem Kongo im Petersdom
Papa Francis akiongoza misa mjini Vatican Julai 3. 2022.Picha: Evandro Inetti/ZUMA Wire/IMAGO

Mji wa L'Aquila linahusishwa na papa Celestine V, aliejiuzulu upapa mnamo mwaka 1294. Papa Benedict XVI alizuru mji huo miaka minne iliyopita kabla ya kujiuzulu mwaka 2013, akiwa papa wa kwanza kufanya hivyo katika kipindi cha miaka 600.

Lakini Francis, akiwa makini na mtulivu wakati wote na mahojiano huku akijadili masuala kadhaa ya kimataifa na kanisa alipuuza wazo hilo. "Matukio hayo yote yaliwafanya baadhi wadhani kuwa liturujia sawa itatokea," alisema. "Lakini haikuingia akilini mwangu. Kwa sasa hapana, kwa sasa, hapana. Kwa kweli!"

Hata hivyo Papa Francis alirudia msimamo wake kwamba huenda akajiuzulu siku moja iwapo hali yake ya afya itafanya kuwa vigumu kwake kuliendesha kanisa - jambo ambalo lilikuwa halifikiriki kabisaa kabla ya Benedict XVI. Alipoulizwa lini anadhani hilo linaweza kutokea, alisema: "Hatujui. Mungu atasema."

Majeraha ya goti

Mahojiano hayo yalifanyika katika siku ambayo Papa alipaswa kuwa ameondoka kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Sudan Kusini, ziara ambayo alilaazimika kuifuta kwa sababu madaktari walisema angeweza kukosa hata ziara ya nchini Canada kuanzia Julai 24-30 isipokuwa akubali kupata matibabu kwa siku 20 zaidi na kupumzika kwa ajili ya goti lake la kulia.

Soma pia: Papa afuta ratiba zake za kazi kufuatia maumivu ya goti

Alisema uamuzi wa kufuta ziara ya Afrika ulimsababishia "mateso makubwa", hasa kwa sababu alitaka kupigia chapuo amani katika mataifa yote mawili. Francis alitumia fimbo kuingia chumba cha mapokezi kwenye gorofa ya kwanza ya nyumba ya wageni ya Santa Martha ambako ameishi tangu kuchaguliwa kwake mwaka 2013, na kuepukana na makazi ya papa yaliotumiwa na matangulizi wake.

Alitoa ufafanuzi kuhusu ugonjwa wake kwa mara ya kwanza hadharani, akisema alipata mvunjiko mdogo kwenye goti wakati alipoteleza na msuli kuvimba. "Sijambi, naendelea kupona taratibu," alisema, na kuongeza kwamba mvunjiko ulikuwa unaunga, akisaidiwa na matatibu madogo ya sumaku.

Vatikan Papst Franziskus mit Christen aus dem Kongo im Petersdom
Raia wa Congo waishio Rome wakiwa katika Kanisa la Mt. Peter wakati wa misa ilioyongozwa na Papa Francis, Julai 3, 2022.Picha: Giuseppe Lami/ZUMA Wire/IMAGO

Francis pia alitupilia mbali uvumi kwamba aligunduliwa na saratani mwaka moja uliyopita alipofanyiwa upasuaji wa masaa sita kuondoa utumbo wake mpana kwa sababu ya tatizo la diverticulitis, ambayo ni hali inayokutikana hasa miongoni mwa watu wenye umri mkubwa.

Soma pia: Papa Francis apanga kuzuru DR Congo na Sudan Kusini

"Operesheni hiyo ilikuwa na mafanikio makubwa," alisema na kuongeza kwa kicheko kwamba "hawakuniambia chochote" kuhusu saratani, ambayo alipuuza kama "umbea." Lakini alisema hakutana upasuaji kwenye goti lake kwa sababu nusukaputi ya upasuaji wa mwaka jana ilikuwa na athari hasi.

Ziara ya Papa Moscow

Akizungumzia hali nchini Ukraine, Francis alibanisha kwamba kumekuwepo na mawasiliano kati ya waziri wa mambo ya nje wa Vatican Pietro Parolin na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov kuhusu uwezekano wa ziara mjini Moscow.

Ishara za awali hazikuwa nzuri. Hakuna papa aliwahi kuizuru Moscow, na Francis amelaani mara kwa mara uvamizi wa Urusi nchini Ukraine; Alhamisi iliyopita, aliituhumu kwa kuanzia vita vya "kikatili na visivyo na msingi vya uvamizi."

Wakati Vatican ilipouliza kwa mara ya kwanza kuhusu ziara hiyo miezi kadhaa iliyopita, Francis alisema Moscow ilijibu kwamba haukuwa wakati sahihi. Lakini alidokeza kwamba huenda kuna kitu kimebadilika hivi sasa.

"Ningependa kwenda Ukraine, na nilitaka kwenda Moscow kwanza. Tunabadilisha ujumbe kuhusu hili kwa sababu nilidhani kwamba ikiwa rais wa Urusi angenipa fursa ndogo kuhudumia sababu ya amani...

"Na sasa inawezekana, baada ya kurejea kutoka Canada, inawezekana kwamba naweza kwenda Ukraine," alisema. "Jambo la kwanza ni kwenda Urusi kujaribu kusaidia kwa namna fulani, lakini ningependa kwenda miji mikuu yote."

Hukumu ya utoaji mimba
 

Alipoulizwa kuhusu hukumu ya mahaka ya juu ya Marekani iliyobatilisha hukumu ya kihistoria ya Roe v. Wade iliyoweka haki za wanawake kutoa mimba, Francis alisema anaheshimu uamuzi huo lakini hakuwa na taarifa za kutosha kuweza kulizungumzia kwa mtazamo wa kisheria.

Soma pia:Papa Francis abadilisha idara za mafundisho ya kiimani 

Lakini alilaani vikali utoaji mimba, na kuulinganisha na "kumuajiri muuaji". Kanisa Katoliki linafundisha kwamba maisha yanaanzia wakati mimba inavyotungwa. "Nauliza: Ni halali, ni sahihi, kuondoa maisha ya mwaandamu ili kutatua tatizo?"

Francis aliulizwa kuhusu mjadala nchini Marekani juu ya iwapo mwanasiasa Mkatoliki binafsi anapinga utoaji mimba lakini anaunga mkono haki za wengine kuchagua anapaswa kuruhusiwa kupokea sakaramenti hiyo katika parokia ya mjini Washington D.C. Wiki iliyopita, Pelosi alipokea sakramenti kwenye misa ya papa mjini Vatican.

"Kanisa linapopoteza hali yake ya uchungaji, padri anapopoteza hali yake ya uchungaji, inasabisha tatizo la kisiasa," alisema Papa. "Hilo ndiyo naweza kusema."

Chanzo: RTRE