1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis ataka vita vya Gaza vikomeshwe

Mohammed Khelef
25 Desemba 2023

Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis, ametumia hotuba yake ya Krismasi kuiokosowa vikali sekta ya viwanda vya silaha na "nyenzo zake za mauti" kwa kuchochea vita.

https://p.dw.com/p/4aZ4K
Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis.
Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis.Picha: Tiziana Fabi/AFP/Getty Images

Akizungumza akiwa kwenye Kanisa la Mtakatifu Petero mjini Vatican siku ya Jumatatu (25 Disemba), Papa Francis alisema alifadhaishwa na  mashambulizi mabaya ya Hamas kusini mwa Israel siku ya tarehe 7 Oktoba na alilitolea wito wa kuwaachia mara moja mateka waliowachukuwa.

Kwa upande mwengine, kiongozi huyo wa Wakatoliki wapatao bilioni 1.3 ulimwenguni alitowa wito kwa Israel kukomesha operesheni ya kijeshi kwenye Ukanda wa Gaza na "uvunaji wa kuogofya wa maisha ya raia wasiokuwa na hatia."

Soma zaidi: Mashambulizi ya Israel yauwa 70, yasema wizara ya afya ya Gaza

Papa Francis pia alitaka misaada ya kibinaadamu iachiwe kuwafikia maelfu ya watu walio kwenye mahitaji katika Ukanda huo.

Maelfu ya waumini wa Kanisa Katoliki walikusanyika kwenye uwanja wa Basilika kumsikiliza kiongozi wao huyo akizungumzia madhila yanayowapata wanyonge ulimwenguni, baada ya hapo jana kuendesha misa ya Mkesha wa Krismasi akielezea masikitiko yake kwa majanga hayo.

Waumini wakipeperusha bendera ta Palestina mjini Vatikani wakati hotuba ya Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis.
Waumini wakipeperusha bendera ta Palestina mjini Vatikani wakati hotuba ya Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis.Picha: Yara Nardi/REUTERS

"Usiku huu, nyoyo zetu ziko Bethlehem, ambako Mwanamfalme wa Amani kwa mara nyengine anakataliwa tena kwa mantiki ovyo ya vita, kwa makabiliano ya silaha ambayo hata hivi leo bado yanamzuwia kupata nafasi ulimwenguni," alisema huyo ambaye siku ya Jumatatu alitazamiwa kuongoza misa ya Krismasi.

Bethlehem yaadhimisha kwa maombolezo

Mji wa Bethlehem wenyewe - ulio katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na ambao Wakristo wanaamini ndio alikozaliwa Yesu Kristo zaidi ya miaka 2,000 iliyopita - ulifuta sherehe za kila mwaka za Krismasi ambazo kawaida huhudhuriwa na maelfu ya watalii.

Soma zaidi: Wakristo washerehekea Krismasi ulimwenguni kote

Mji huo umeondosha mti mkubwa wa Krismasi pamoja na mapambo yote yanayoung'arisha na kuacha taa chache tu. 

Wakristo wakiadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo katika mji wake wa Bethlehem.
Wakristo wakiadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo katika mji wake wa Bethlehem.Picha: Mahmoud Illean/dpa/AP/picture alliance

Katikati ya mji huo, bendera kubwa ya Palestina imewekwa ikiwa na bango lililoandikwa: "Kengele za Bethlehem zinalia kwa ajili ya usitishaji mapigano Gaza."

"Watu wengi wanakufa kwa ardhi hii," alisema Nicole Najjar, mwananfunzi mwenye umri wa miaka 18, aliyeongeza kuwa ni shida kusherehekea "wakati watu wetu wanakufa."

Makanisa ya kale yaungana na Palestina

Mkuu wa kanisa la Kilatini la Jerusalem, Pierbattista Pizzaballa, alisema: "Tupo hapa kusali na kuomba sio tu kwa ajili ya usitishaji mapigano, usitishaji mapigano hautoshi, lazima tukomeshe ugomvi huu na tufunuwe ukurasa mpya kwa sababu machafuko huzaa machafuko tu."

Soma zaidi: Mkuu wa Kanisa Katoliki Kongo ahimiza utulivu

Nchini Syria, makanisa yaliamuru sherehe za Krismasi zifanyike kwa maombi ya mshikamano na Wapalestina tu.

Sherehe za Krismasi mjini Damaskas, Syria.
Sherehe za Krismasi mjini Damaskas, Syria.Picha: Omar Sanadiki/AP/picture alliance

Mnamo tarehe 7 Oktoba, kundi la Hamas linalotambuliwa na Israel na mataifa kadhaa ya Magharibi kuwa la kigaidi lilifanya mashambulizi yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 1,140 nchini Israel, wengi wao wakiwa raia kwa mujibu wa takwimu za shirika la habari la AFP zinazotokana na takwimu rasmi za Israel.

Wanamgambo hao wa Kipalestina waliwateka nyara watu wapatao 250, ambapo Israel inasema hadi sasa 129 kati yao wameendelea kusalia Ukanda wa Gaza. 

Israel ilijibu mashambulizi hayo kwa makombora na uvamizi wa ardhini dhidi ya Gaza, ambako watu 20,424 wameshauawa, wengi wao wanawake na watoto, kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni zilizotolewa na wizara ya afya ya Ukanda huo ulio chini ya Hamas.

Ukraine yaachana na Krismasi ya Orthodoksi

Nchini Ukraine, taifa lililo chini ya uvamizi wa Urusi kwa miaka miwili sasa, imeamua kusherehekea Krismasi tarehe 25 Disemba kwa mara ya kwanza, ikijitenga na maadhimisho ya kijadi ya Wakristo wa Orthodoksi ya tarehe 7 Januari yanayofanyika nchini Urusi.

Mti wa Krismasi uking'ara kwa taa mjini Kiev, wakati Ukraine ikiadhimisha sherehe hizo tarehe 25 Disemba kwa mara ya kwanza.
Mti wa Krismasi uking'ara kwa taa mjini Kiev, wakati Ukraine ikiadhimisha sherehe hizo tarehe 25 Disemba kwa mara ya kwanza.Picha: Vladimir Shtanko/Anadolu Agency/picture alliance

"Tunaamini kwamba tunapaswa kusherehekea Krismasi na ulimwengu mzima, mbali sana kabisa na Moscow. Kwangu mimi, huu ni ujumbe mpya sasa," alisema mkuu wa parokia ya Odesa, Olena, ambaye mtoto wake wa kiume anahudumu kwenye mstari wa mbele ya kivita akiwa daktari.

Soma zaidi: Steinmeier awaonya wananchi kutoipa kisogo demokrasia

Mabadiliko ya tarehe, ambayo yanaachana na kalenda ya Julia inayopendelewa na Kanisa la Orthodoksi, ni sehemu ya hatua za kuondosha alama za Urusi na himaya ya Usovieti. 

Katika siku ya mkesha wa Krismasi, jeshi la Ukraine lilisema liliziangusha droni 28 za mashambulizi kati ya 31 zilizorushwa na Urusi. 

Jeshi hilo lilisema hakukuwa na mtu yeyote aliyeuawa wala kujeruhiwa. 

Vyanzo: AFP, dpa, AP