1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis awahimiza Wakristo kutopoteza tumaini

John Juma Mhariri: Rashid Chilumba
4 Aprili 2021

Kiongozi mkuu wa kanisa Katoliki ulimwenguni Papa Francis, amewahimiza waumini kutopoteza tumaini kufuatia janga la muda mrefu la virusi vya corona.

https://p.dw.com/p/3rZDY
Vatikan I Papst feiert Osternacht
Picha: Remo Casilli/AFP

Mamilioni ya waumini wa dini ya Kikristo duniani wanashehekea leo sikukuu ya Pasaka chini ya vizuizi vikali vya kukabiliana na virusi vya corona ambavyo maambukizi yake bado yanaongezeka kwenye mataifa mengi ulimwenguni.

”Katika saa ya giza wakati binadamu anapambana na janga la Corona pamoja na magonjwa mengine, Wakristo wanapaswa kuzingatia ujumbe wa malaika wakati wa Pasaka wa kutoogopa”.

Papa Francis mwenye umri wa miaka 84 ameyasema hayo usiku wa Jumamosi Takatifu katika kanisa la Mtakatifu Petero mjini Roma Italia, wakati wa mkesha wa Pasaka.

Kwenye ujumbe wake mmoja wa Pasaka, Papa Francis amesema inawezekana kila wakati kuanza upya. Hata kwenye historia ya vurugu ya mwanadamu, Mungu ameumba kitu kipya.

Idadi ndogo ya waumini ndio waliruhusiwa kuhudhuria misa ya mkesha wa Pasaka katika kanisa la Mtakatifu Petero mjini Vatican.
Idadi ndogo ya waumini ndio waliruhusiwa kuhudhuria misa ya mkesha wa Pasaka katika kanisa la Mtakatifu Petero mjini Vatican.Picha: Remo Casilli/AFP

”Kutoka kwenye vipande vya mioyo yetu, Mungu anaweza kuumba kazi ya sanaa; kutokana na mabaki ya ubinadamu, Mungu anaweza kutengeneza historia mpya,” amesema Papa na kuongeza kuwa ”katika miezi hii ya giza la janga… msikilize Yesu Aliyefufuka. Anatualika tuanze upya na tusipoteze tumaini”.

Mikakati ya kuzuia virusi vya corona kusambaa

Takriban waumini 200 wakiwemo viongozi wa kidini ndio walihudhuria misa hiyo ya mkesha wa Pasaka mjini Vatican. Idadi ndogo ya watu ndio waliruhusiwa kuhudhuria, ikiwa ni hatua ya tahadhari kuepusha kusambaa kwa virusi vya corona.

Kwa mwaka wa pili mfulilizo makao makuu ya kanisa katoliki duniani mjini Vatican yamelazimika kupunguza matukio ya kidini yanayoambatana na shehere za pasaka ili kuondoa uwezekano wa kusambaa virusi vya corona.

Waumini wengi wameshauriwa kushiriki maombi na sherehe za Pasaka majumbani.

Papa Francis: Kuwa tayari kushangazwa na Yesu

Francis pia alisisitiza kwamba Kristo yuko hai hapa na sasa. "Imani si albamu ya kumbukumbu za zamani; Yesu hajapitwa na wakati. Hutembea kando yako kila siku, katika kila jaribio unalokumbana nalo, katika matumaini yako makubwa na ndoto zako. Hata ukihisi umepoteza kila kitu, kuwa tayari kushangazwa na jinsi Yesu huleta mambo mapya. Bila shaka atakushangaza”

Waumini wa Kikristo huadhimisha kufufuka kwa Yesu katika Wikendi ya Pasaka. Kwa baadhi ya wakereketwa wa imani hiyo, Pasaka ndiyo sherehe muhimu zaidi kila mwaka miongoni mwa sherehe za Kikristo.

Pasaka kuashiria nuru ya Yesu

Papa Francis akiwasha mshumaa kuashiria nuru ya Yesu
Papa Francis akiwasha mshumaa kuashiria nuru ya YesuPicha: Remo Casilli/AFP

Katika misa ya Jumamosi Takatifu, Papa Francis aliwasha mshumaa wa Pasaka kwenye kanisa lililokuwa na kiza la Mtakatifu Petero, kuashiria nuru ya Yesu.

Baadaye leo, Papa Francis anatarajiwa kuongoza waumini katika misa ya sherehe ya Pasaka katika kanisa la Mtakatifu Petero, kuashiria kufufuka kwa Yesu Kristo.

Kabla ya janga la corona,  maadhimisho hayo yaliandaliwa katika viwanja vya kanisa la Mtakatifu Petero na kuhudhuriwa na maelfu ya waumini.

(DPA)