1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Jamhuri ya Afrika ya Kati

29 Novemba 2015

Papa Francis ametoa mwito wa amani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati Jumapili (29.11.2015) alipotembelea kambi za watu walioachwa bila makaazi

https://p.dw.com/p/1HELs
Papa Francis alipowasili uwanja wa Kimataifa wa Bangui
Papa Francis alipowasili uwanja wa Kimataifa wa BanguiPicha: Reuters/S. Modola

Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani papa Francis ametoa mwito wa amani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati Jumapili(29.11.2015) alipotembelea kambi za watu walioachwa bila makaazi kutokana na vita vya kidini vilivyoikumba nchi hiyo koloni la zamani la Ufaransa.

Katika ujumbe wake papa aliwaambia mamia ya wakaazi katika kambi hizo wanakoishi watu 7,000 kwamba bila ya kuvumiliana,kusameheana ni jambo lisilowezekana.Wakaazi hao walimuimbia papa huku wakionesha mabango yaliyoandikwa maneno Tunakupenda na tunafuraha huku wakijipanga kusalimiana kwa mikono na kiongozi huyo wa kiroho.

Kambi ya wakimbizi wa ndani wa vita vya kidini kati ya waislamu na wakristo iko nje kidogo na mji mkuu Bangui.Maelfu ya watu wameuwawa na kiasi cha robo ya watu milioni 4.7 wameachwa bila makaazi ya kuishi tangu waasi wa Seleka ambao wengi ni waislamu walipomuondoa kwa nguvu madarakani rais Francoise Bozize ambaye ni mkristo mnamo mwezi March mwaka 2013.

Papa Francis akiwa katika kambi ya wakimbizi ya Saint Sauveur
Papa Francis akiwa katika kambi ya wakimbizi ya Saint SauveurPicha: Reuters/S. Rellandini

Papa ni Baraka

Mapema Jumapili,Papa Francis alizungumza na rais wa mpito Catherine Samba Panza pamoja na viongozi wengine wa kisiasa nchini humo akiwatolea mwito wa kuzikana chuki za kidini. Umoja ni kuishi na kujengwa chini ya misingi ya kuwakubali walioko kwenye mazingira yetu na kuepuka vishawishi au kujenga khofu kwa wengine,tusiowajua,au wenye kufuata kile ambacho sio sehemu ya kinachofuatwa na jamii zetu''alisema Papa Francis.Akijieleza kama nguzo ya amani Papa alisema kanisa Katoliki nchini humo litafanya kazi kuleta maridhiano Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Kwa upande mwingine rais wa mpito Catherine Samba Panza ameitaja ziara ya Papa kuwa ni baraka kutoka mbinguni na kwamba kiongozi huyo wa kidini anaweza kuisadia Jamhuri ya Afrika ya Kati kuushinda mgawanyiko unaosababishwa na shetani,pamoja na chuki na mkanganyiko.

Akaribishwa na wote

Papa Francis,Muargentina,mwenye umri wa miaka 78 alikaribishwa na jamii ya waislamu na wajumbe wa kanisa katoliki mara alipowasili katika nchi hiyo Jumapili ikiwa ni kituo cha mwisho cha ziara yake ya siku sita ya barani Afrika iliyomfikisha pia Kenya na Uganda.

El-Hajji Tchakpabrede ambaye anaiwakilisha jamii ya waislamu nchini humo amesema Papa Francis hakwenda nchini humo kwa ajili ya wakatoliki pekee bali kwa wana jamhuri ya Afrika ya kati kwa ujumla na hiyo ni ishara nzuri ya maridhiano kati ya waislamu na watu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Papa akimpa baraka mtoto katika kambi ya wakimbizi wa ndani
Papa akimpa baraka mtoto katika kambi ya wakimbizi wa ndaniPicha: Reuters/S. Rellandini

Kulikuwepo na wasiwasi kwamba makundi ya itikadi kali kutoka pande zote za mgogoro wa nchi hiyo huenda wakaitumia nafasi hii ya ziara ya Papa kuchochea vurugu katika taifa hilo ambako ghasia zimeua kiasi watu 90 tangu mwishoni mwa mwezi Septemba.

Hata hivyo Papa alitumia gari la wazi katika ziara hiyo licha ya wasiwasi kwamba maafisa wa nchi hiyo huenda wangeshindwa kumhakikishia usalama wake.

Ziara ya Papa barani Afrika ni ziara ya 11 ya kiongozi huyo katika nchi za nje tangu alipochukua nafasi hiyo ya kiroho mwaka 2013.Kuna wakatoliki kiasi milioni 180 katika bara hilo la Afrika na idadi hiyo inaongezeka kwa kasi zaidi kuliko ilivyo kwenye eneo jingine lolote duniani.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Amina Abubakar