1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

PARIS : Chirac kutangaza kun’gatuka

11 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCKG

Rais Jaques Chirac wa Ufaransa leo hii anatazamiwa kutangaza kwamba hatogombania urais katika uchaguzi wa mwezi ujao kwa kuthibitisha kwamba anapanga kustaafu hapo mwezi wa Mei baada ya kuwa katika siasa kwa zaidi ya miaka 40.

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 74 ambaye amekuwa madarakani tokea mwaka 1995 anatarajiwa kutowa ujumbe huo kwa taifa hapo jioni kuwa kupitia radio na televisheni.

Maudhui ya ujumbe huo yamefanywa kuwa siri na Ikulu ya Elysee lakini karibu kile kinachotegemewa na dunia nzima ni kwamba rais huyo atasema hatogombea kipindi cha tatu madarakani.

Wakati uteuzi rasmi wa wagombea unatarajiwa hapo Ijumaa ijayo Chirac ameweka wazi hadi dakika za mwisho uwezekano wa kuwania tena wadhifa huo wa urais licha ya uchunguzi wa maoni kuonyesha kwamba hangelikuwa na nafasi ya kushinda tena.

Hata hivyo hivi karibuni alidokeza mara kadhaa kwamba anakusudia kun’gatuka kwa kusema katika mahojiano ya televisheni kwamba kuna maisha baada ya siasa na kwamba anatumai kuitumikia Ufaransa katika nafasi nyengine.