1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pence adai China inaingilia Siasa za Marekani

Caro Robi
5 Oktoba 2018

Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence ameishutumu China kwa kumhujumu Rais Donald Trump ikitaka kuona rais tofauti wa Marekani, na pia amekosoa rekodi ya haki za binadamu ya nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/36142
USA, Washington:  Mike Pence
Picha: picture-alliance/dpa/E. Vucci

Pence amesema China imeanzisha njama ya kutaka kushawishi visivyo maoni ya Wamarekani, kuingilia chaguzi za majimbo zinazofanyika hivi karibuni na kuweka mazingira hasi kuelekea uchaguzi wa urais wa mwaka 2020.

Makamu huyo wa Rais wa Marekani ameendelea kusema China inatumia nguvu zake kwa njia isiyokuwa na mfano kuingilia sera na siasa za Marekani.

Akizungumza katika taasisi ya utafiti ya Hudson, Pence amesema utawala wa Trump unafanya kazi na ni jambo ambalo Wachina wamepania kulihujumu kwa kutaka kuwepo Rais mwingine mbali na Trump madarakani kwa kuingilia demokrasia ya nchi hiyo.

Aidha ameishutumu China pia kwa ukiukaji wa haki za binadamu, akigusia suala tete la uhusiano na Taiwan na ukandamizaji dhidi ya Waislamu, Wakristo na Wabudha.

Kauli yake inakuja wiki moja baada ya Rais Donald Trump naye kuishutumu China kuwa inaingilia chaguzi zinazotarajiwa tarehe 6 mwezi Novemba ili kukipa ushindi chama cha Democrats.

Uhusiano wa China na Marekani wazorota

Trump alisema China haitaki ashinde kwasababu ndiye rais wa kwanza wa Marekani kuhoji sera kandamizi za China kuhusu biashara. China imekanusha vikali madai hayo na kuyataja yasiyostahili, yasiyo na msingi wowote na ya kuchekesha.

China USA Donald Trump & Xi Jinping | Große Halle des Volkes
Rais wa Marekani Donald Trump na Rais wa China Xi JinpingPicha: Reuters/D. Sagolj

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Hua Chunying amesema madai ya Marekani ni uvumi unaochanganya ya kweli na ya uongo na kuibuka na mambo yasiyo na msingi, jambo ambalo China inapinga.

Hua ameongeza kusema nchi yake imedumisha sera yake ya kutoingilia siasa za nchi nyingine na badala yake kuinyooshea kidole Marekani kwa kubobea kwa muda mrefu kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine ulimwenguni.

Huku utawala wa Trump ukiishutumu China kwa kuingilia chaguzi na sera za Marekani, bado kuna wingu la mashaka kuhusu ushawishi wa Urusi katika uchaguzi uliopita wa rais nchini Marekani uliompa ushindi Trump dhidi ya Hillary Clinton.

Uchunguzi unaendelea kubaini iwapo Urusi ilimsaidia Trump kushinda uchaguzi wa mwaka 2016 kwa kufanya udukuzi.

Trump mara kwa mara amekanusha madai hayo. Matamshi makali kutoka kwa Rais Trump na makamu wake dhidi ya China yanakuja siku chache kabla ya waziri wa mambo ya nje Mike Pompeo kuizuru China kwa lengo la kutafuta uungwaji mkono kutoka kwa nchi hiyo katika kuutatua mzozo wa kinyuklia wa Korea Kaskazini.

China imejaribu kujizuia kujibizana na Marekani. Balozi wa China nchini Marekani Cui Tiankai amesemakuna haja kubwa ya ushirikiano badala ya ushindani kati ya mataifa hayo mawili.

Mahusiano kati ya China na Marekani, mataifa yenye nguvu kubwa zaidi kiuchumi yamezorota katika kipindi cha hivi karibuni kuhusiana na mzozo wa kibiashara, kila nchi ikiiongeza nyingine kodi za bidhaa za mabilioni ya dola na kutishia kuutumbukiza ulimwengu katika vita vya kibiashara.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters/dpa

Mhariri: Gakuba, Daniel