1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pirika pirika za kisiasa baada ya uchaguzi mkuu

Oumilkher Hamidou1 Oktoba 2009

Katika wakati ambapo washirika wa serikali mpya ya muungano wananoa bongo,wale wa SPD wanatafakari

https://p.dw.com/p/JvQF
Kansela Angela Merkel na anaetarajiwa kua makamo wake Guido WesterwellePicha: picture alliance/dpa

Mazungumzo ya kuunda serikali mpya ya muungano ya vyama vya CDU/CSU na manjano, na mkondo wa aina gani utafuatwa na chama cha SPD baada ya pigo la uchaguzi mkuu ni miongoni mwa mada zilizohanikiza magazetini hii leo.

Tuanze basi na mazungumzo ya kuunda serikali mpya ya muungano.Gazeti la "Der neue Tag" la Weiden linaandika:

Mwenyeji wa mazungumzo hayo,Jürgen Rüttgers atawahudumia ipasavyo wageni wake,seuze tena yeye ndie atakaekua wa mwanzo miongoni mwa wakuu wa vyama ndugu vya CDU/CSU kutegemea natija ya mshirika mpya serikalini.Waziri mkuu huyo wa serikali ya jimbo la North Rhine Westfalia atalazimika kutetea wadhifa wake uchaguzi wa bunge utakapoitishwa msimu wa kiangazi mwakani.Uchaguzi huo utaangaliwa pia kama kipimo cha ufanisi wa serikali ya muungano ya nyeusi na manjano.Wakishindwa katika uchaguzi wa jimbo hilo lenye wakaazi wengi kupita kwengineko humu nchini,basi madhara yake hayatamalizikia pekee katika kudhoofisha hadhi ya serikali ya muungano,bali yatasababisha pia kulega lega wingi wa viti vinavyoshikiliwa na vyama vya Merkel na Westerwelle katika baraza la wawakilishi wa majimbo-Bundesrat.

Gazeti la "BRAUNSCHWEIGER ZEITUNG" linazungumzia kuhusu soko la ajira.Gazeti linaandika:

Serikali mpya ya Nyeusi na Manjano itajipatia fursa ya kutosha kudhihirisha werevu na moyo wao katika masuala ya jamii.Cha kutia moyo ni kwamba CDU/CSU,wameshakwenda na wameona kwa hivyo si wageni katika shughuli za serikali.Sie lakini tusikubali kudanganywa kua ni ufanisi wao,idadi ya wasiokua na ajira itakapopungua na kua chini ya watu milioni tatu na laki tano.Ingawa katika enzi za migogoro,hali hiyo inakubalika,lakini kwa mtazamo wa muda mrefu,hatua nyengine zitahitajika.

Flashgalerie Die Woche in Bildern 40_09
Wanaotazamiwa kukiongoza chama cha SPD-kutoka kushoto Andrea Nahles,Sigmar Gabriel na kulia Frank-Walter SteinmeierPicha: picture-alliance/ dpa

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamejishughulisha pia na pirika pirika za kubadilisha uongozi na mkondo wa siasa ndani ya chama cha Social Democratic-SPD kilichoshindwa vibaya sana katika uchaguzi mkuu wa September 27 iliyopita.Gazeti la "FLENSBURGER TAGEBLATT linaandika:

Olaf Scholz,mara nyingi anazungumzia kinaga ubaga juu kile ambacho wanasiasa wengi wa ngazi ya juu wa SPD wamekua wakikizungumzia kichini chini:Wanasocial Democratic wanataka kushirikiana na waafuasi wa mrengo wa shoto -Di Linke sio tuu katika daraja ya kimkoa,bali pia ya shirikisho.Lakini mbinu hizo za kisiasa zina madhara yake:Chama cha SPD kimepoteza sauti milioni sita katika uchaguzi mkuu uliopita.Sauti milioni moja na laki tatu kati ya hizo zimeviendeya vyama vya CDU/CSU na waliberali.Kila wakati ambapo wanasocial Democratic watapanua milango kuelekea kushoto ndipo watakapozidi pia kupoteza kura za wafuasi wa mrengo mpya wa kati ulioanzishwa na Gerhard Schröder mnamo mwaka 1998.

Karata zimeshaanza kuchanganywa upya katika chama cha SPD, linaandika gazeti la "DARMSTÄDTER ECHO" na kuendelea:

Picha ya uongozi haimaanishi mwenye uwezo ndie anaekabidhiwa wadhifa fulani.Hasha imelengwa zaidi kukidhi masilahi ya makundi mbali mbali chamani au angalao kuyafumba midomo kwa muda. Sigmar Gabriel anawakilisha mrengo wa kati,Andrea Nahles mrengo wa shoto na mrengo wa kulia unawakilishwa na Steinmeier.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/DPA

Mhariri:Sekione Kitojo