1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pittsburgh: Aliyeuwa 11 katika hekalu la Kiyahudi akamatwa

Daniel Gakuba
28 Oktoba 2018

Mwanamme mmoja ametiwa mbaroni kuhusiana na shambulizi la bunduki liliouwa watu 11 katika hekalu la Wayahudi mjini Pittsburgh, Marekani.

https://p.dw.com/p/37H8s

Mtu huyo alilivamia hekalu la Wayahudi la ''Mti wa Uzima'' mjini Pittsburgh na kuwamiminia risasi waumini waliokuwa katika sherehe ya kumpa mtoto jina, na kuuwa 11 miongoni mwao. Mtu huyo aleyetambulishwa kama Robert Bowers mwenye umri wa miaka zaidi ya 40, aliwajeruhi pia watu wengine 6, wakiwemo maafisa 4 wa polisi.

Wizara ya sheria ya Marekani imesema mauaji hayo yaliyotokea Jumamosi alasiri yanachunguzwa kama uhalifu wa chuki dhidi ya Wayahudi.

Hekalu liloshambuliwa liko katika kitongoji chenye wakazi wengi wa Kiyahudi katika mji wa Pittsburgh jimboni Pennsylvania.

Waziri wa mambo ya ndani wa Marekani Jeff Sessions amesema uhalifu uliofanywa na mtu huyo, aliyetajwa na kituo kimoja cha redio cha KDKA kuwa ''mwanamme mzungu mwenye mwili uliojaza'' ni ya kuchukiza na ni kinyume na maadili ya Kimarekani.

Mashahidi wamesema mshambuliaji huyo alipokuwa akifyatua risasi, alitamka maneno ya kuunga mkono maangamizi dhidi ya Wayahudi.

Rais Donald Trump pia ameyalaani mauaji hayo, na kusifu vyombo vya usalama kwa 'kazi nzuri', na ameamuru bendera zote kupepea nusu mlingoti kwa heshima ya wahanga wa mashambulizi hayo.

Mwandishi: Daniel Gakuba/ dpae, rtre

Mhariri: Yusra Buwayhid