1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi aliyekabiliana na waandamanaji Marekani, afariki

Lilian Mtono
8 Januari 2021

Afisa mmoja wa polisi nchini Marekani Brian Sicknick, amefariki dunia kufuatia majeraha aliyoyapata wakati akikabiliana na wafuasi wa Rais Donald Trump waliovamia majengo ya bunge.

https://p.dw.com/p/3ngGq
Arizona Phoenix Kapitol | schwerbewaffnete Trump-Anhänger
Picha: Ross D. Franklin/AP/picture alliance

Idadi jumla ya waliofariki kufuatia machafuko hayo sasa imefikia watano. 

Kulingana na taarifa ya jeshi la polisi, afisa huyo Sicknick alijeruhiwa wakati akikabiliana ana kwa ana na waandamanaji waliovamia majengo ya bunge wakati wabunge walipokuwa ndani ya jengo hilo kuthibitisha ushindi wa rais mteule Joe Biden siku ya Jumatano.

Sicknick alikimbizwa hospitalini baada ya kuanguka baada ya kurudi kwenye kituo chake cha kazi akitokea kwenye majengo hayo ya Capitol Hill, lakini hatimaye jana umauti ulimkuta. Kulingana na ripoti Sicknick alipata kuharusi na alikuwa akitumia vifaa vya kumsaidia kupumua kabla ya kifo chake.

Polisi inataraji kufanya uchunguzi zaidi wa kifo chha Sicknick aliyejiunga na kikosi cha polisi cha kulinda majengo hayo ya bunge mwaka 2008.

Tukisalia humo humo kwenye jeshi la polisi, hapo jana mkuu wa jeshi hilo mjini Washington Steven Sund Marekani: Undumilakuwili wa polisi ameandika barua ya kujiuzulu wadhifa huo kuanzia Januari 16.

Spika wa baraza la wawakilishi Nancy Pelosi alimtaka kiongozi kujiuzulu baada ya jeshi la shirikisho linalohusika na ulinzi wa majengo ya bunge kushindwa kuwazuia wafuasi wa Trump kuvamia eneo hilo hiyo juzi.

Trump ambaye awali aliwasifu wavamizi hao, baadaye alilaani hatua hiyo akisemawaandamanaji hao walikinajisi kiti cha demokrasia ya taifa hilo na wanatakiwa kuwajibishwa. Watu wengine wanne wamekufa kufuatia tukio hilo.

US-Bildungsministerin Betsy DeVos
Waziri wa elimu Betsy DeVos ni miongoni mwa mawaziri waliojizulu kufuatia kadhia hiyo ya waandamanaji.Picha: Alex Wong/Getty Images

Hali ya sintofahamu imeendelea kuigubuka serikali ya Trump inayoelekea ukingoni mwa utawala wake, baada ya mawaziri wawili nao kujiuzulu. Waziri wa masuala ya usafirishaji Elaine Chao na waziri wa elimu Betsy DeVos wameachia nyadhifa zao hapo jana na kujiunga na msururu wa washauri wa Trump wanaojiengua kwenye serikali yake baada ya tukio hilo.

Awali, washauri wengine wanne katika Baraza la Usalama wa Taifa katika ikulu ya Marekani wamejiuzulu. Kulingana na shirika la habari la Reuters washauri hao  Erin Walsh, mkurugenzi mwandamizi wa maswala ya Afrika, Mark Vandroff mkurugenzi mwandamizi wa sera ya ulinzi, Anthony Rugierro, mkurugenzi mwandamizi wa maswala ya silaha za maangamizi na Rob Greenway, mkurugenzi mwandamizi wa maswala ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.

Tizama:

Viongozi duniani walaumu uvamizi wa majengo ya bunge na seneti nchini Marekani

Wakati viongozi kutoka chama cha Democratic wakishinikiza kuondolewa kwa Trump, rais huyo mtata jana jioni alichapisha video akilihakikishia taifa hilo kwamba mabadilishano ya madaraka yatafanyika kwa amani ifikapo Januari 20.

"Bunge limethibitisha matokeo na serikali mpya itaapishwa Januari 20. Ninachokipa umuhimu sasa ni kuhakikisha ubadilishanaji wa amani wa madaraka.” alisema Trump.

Siku hizi chache zilizosalia kwa Trump hazionekani kuwa rahisi hata kidogo hasa wakati ambapo hii leo wabunge wa chama cha Democratic wakiangazia kuanza mchakato wa pili wa kumshitaki, siku mbili tu baada ya madai yake yasiyo ya ukweli ya kuibiwa kura yaliyowachochea waandamanaji hao kuvamia majengo ya Capitol Hill.

Mashirika: RTRE