1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi aliyemuua Mmarekani Mweusi kushitakiwa Atlanta

Mohammed Khelef
15 Juni 2020

Maandamano yamezuka tena Marekani baada ya Mmarekani mwengine mwenye asili ya Afrika kuuawa na polisi, huku jeshi la polisi likichukuwa hatua za kumfuta kazi afisa wake aliyehusika na mauaji hayo.

https://p.dw.com/p/3dmIl
USA I Polizeigewalt in Atlanta
Picha: Reuters/E. Nouvelage

Afisa wa polisi aliyempiga risasi na kumuuwa Rayshard Brooks, Mmarekani mwenye asili ya Kiafrika mwenye umri wa miaka 27, huenda akafunguliwa mashitaka katikati ya wiki hii, kwa mujibu wa mwendesha mashitaka mkuu wa Kaunti ya Fulton, Paul Howard.

Howard alisema kuwa kabla ya kuchukuwa uamuzi wa kufunguwa rasmi mashitaka hayo dhidi ya Garret Rolfe, ofisi yake itawahoji mashahidi wengine wawili, akiongeza kwamba hadi sasa wanakumbana na tatizo la kutokupatiwa picha zote za kamera wanazovaa polisi kutoka kwa Idara ya Polisi ya Atlanta.

Katika hatua za awali, afisa aliyefyatua risasi zilizomuua Brooks amefutwa kazi, huku mwenzake aliyehusika na tukio hilo, Devin Brosnan, akisimamishwa kazi na kuwekwa chini ya uangalizi, na Mkuu wa Polisi wa Atlanta, Erika Shields, amejiuzulu.

Usiku wa kuamkia Jumamosi, afisa huyo wa polisi alimpiga risasi Brooks nje ya mkahawa mmoja, baada ya kijana huyo kukataa kukamatwa na kuwaoteza polisi kifaa cha kushitua misuli ambacho alikikwapua kwa maafisa hao wa polisi.

Mauaji ya kukusudia?

USA I Polizeigewalt in Atlanta
Maandamano ya kupinga mauaji ya Rayshard Brooks mjini Atlanta katika jimbo la Georgia.Picha: Reuters/E. Nouvelage

Kwa mujibu wa madaktari, Brooks alikufa baadaye kutokana na majeraha ya risasi mbili zilizovunja viungo vyake na kuvuja damu kwa wingi.

Kwenye mahojiano yake na kituo cha CNN, mwanasheria Howard alisema kwamba kijana huyo hakuonekana kuwa kitisho mbele ya polisi hao na inastaajabisha sana kwamba tukio hili lilisababisha mauti yake.

Kwa mpaka sasa, mamlaka za uchunguzi zinalichukulia tukio hili kuwa ni mauaji ya kukusudia. 

Mauaji haya yamechochea wimbi jipya la maandamano na  machafuko dhidi ya ukatili wa polisi na ubaguzi wa rangi mjini Atlanta, siku chache tu baada ya hali kuanza kupowa kufuatia mauaji mengine ya Mmarekani mwenye asili ya Afrika, George Floyd, akiwa mikononi mwa polisi ya Minneapolis mwezi uliopita. 

Kama alivyokuwa kwa Floyd, Brooks naye alikuwa baba wa watoto wanne ambaye alikuwa ametoka kusherehekea miaka minane ya kuzaliwa kwa binti yake mapema siku ya Ijumaa. Kifo chake ni tukio la 48 kuwahusisha maafisa wa polisi ambalo Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu, GBI, imeombwa kufanyia uchunguzi ndani ya mwaka huu. Matukio 15 katika hayo, yalikuwa ya mauaji dhidi ya raia wasiokuwa na silaha.