1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi Ufaransa wafanya misako baada ya mwalimu kuchinjwa

John Juma
19 Oktoba 2020

Maafisa wa polisi Ufaransa wafanya misako katika majumba ya wanamgambo wenye itikadi kali za kiislamu, baada ya mwalimu kuchinjwa kwa kuwaonyesha wanafunzi vibonzo vya Mtume Mohammed.

https://p.dw.com/p/3k7yL
Frankreich Paris | Trauer um getöteten Lehrer Samuel Paty
Picha: Michel Euler/AP/picture-alliance

Kulingana na Waziri wa ndani wa Ufaransa Gerald Darmanin, misako hiyo imeendelea hadi asubuhi ya leo na itaendelea kwa siku kadhaa zijazo.

Ameongeza kuwa wanawalenga watu kadhaa wenye itikadi kali za Kiislamu, na kwamba wiki hii operesheni hiyo itawaandama pia washirika kadhaa. 

Darmanin amesema wameanzisha zaidi ya chunguzi 80 kuhusu matamshi ya chuki mitandaoni, kufuatia kuuawa kwa mwalimu huyo, ambaye awali alikuwa akilengwa na kushambuliwa mitandaoni kwa maneno ya chuki. 

Juhudi za kukabili matamshi ya chuki mitandaoni

Frankreich | Paris | Emmanuel Macron spricht nach einer brutalen Messerattacke
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron Picha: Abdulmonam Eassa/Pool/Reuters

Kwenye mkutano wa Baraza la Ulinzi, ulioongozwa na Rais Emmanuel Macron usiku wa kuamkia leo, iliamuliwa kwamba hatua kali zichukuliwe nchini humo dhidi ya itikadi kali na pia juhudi zaidi kuelekezwa dhidi ya matamshi ya chuki mitandaoni. 

Waziri wa mambo ya ndani amesema tangu kisa cha kuuawa kwa mwalimu huyo siku ya Ijumaa, takriban malalamiko 80 yamewasilishwa kuhusu chuki inayoenezwa mitandaoni inayokisifu kitendo hicho. 

Awali, mshukiwa mkuu wa uchinjaji huo mwenye umri wa miaka 18, alijigamba mitandaoni na kuandika kwamba mwalimu huyo alimdhalilisha Mtume Mohammed. 

Wenye itikadi kali watangaza ‘fatwa‘

Darmanin amesema baba wa mwanafunzi mmoja katika shule, pamoja na wenzake wengine waliendeleza kampeni ya mitandaoni dhidi ya mwalimu huyo, na kutangaza “Fatwa“ dhidi yake. 

Katika Uislamu, fatwa ni uamuzi unaotolewa na mamlaka inayotambuliwa kuhusu jambo linalohusu sheria ya kidini. 

Lakini mnamo mwaka 1989, watu walichukua maana potofu ya neno hilo pale kiongozi wa kidini wa Iran Ayatollah Khomeini alipotangaza waranti wa kifo dhidi ya mwandishi wa Uingereza Salman Rushdie kwa kukufuru. 

Mwalimu huyo wa Historia kwa jina Samuel Paty mwenye umri wa miaka 47, aliuawa Ijumaa iliyopita, viungani mwa mji wa Paris. 

Kisa charejesha kumbukumbu ya shambulizi la Charlie Hebdo

Frankreich Charlie Hebdo | Tout ca, pour ca
Gazeti la Charlie Hebdo |Picha: Getty Images/AFP

Aliyemuua mwalimu huyo alitambuliwa kuwa na mizizi ya Chechnia na alizaliwa Urusi. Aliuawa kwa kupigwa risasi na polisi. 

Inadaiwa kuwa mapema mwezi huu, Paty aliwaonyesha wanafunzi vibonzo vyenye utata vya Mtume Mohammed darasani wakati akifundisha kuhusu uhuru wa kujieleza.

Kuuawa kwa mwalimu huyo kumeishtua Ufaransa na kukumbusha shambulizi la miaka mitano iliyopita katika ofisi ya jarida la Charlie Hebdo, lililotokea baada ya kuchapisha vibonzo vya Mtume Mohammed. 

Chanzo: AFPE, DPAE