1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi wadhibiti mikutano ya Bobi Wine

Admin.WagnerD24 Februari 2020

Nchini Uganda mtu mmoja ameuwawa kwa kugongwa na gari la polisi waliokuwa kwenye harakati za kuuzima mkutano wa mwanasiasa wa upinzani  Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine.

https://p.dw.com/p/3YKAz
Popsänger Bobi Wine als Oppositionspolitiker der People Power campaign
Picha: picture-alliance/Cover Images/L. Dray/

Mwanasiasa na msanii huyo wa Uganda Robert Kyagulanyi anayefahamika zaidi kwa jina la usanii la Bobi Wine anaendelea kukabiliwa na wakati mgumu kuzindua mikutano yake ya kushauriana na wananchi kuhusu ugombeaji wake wa urais. Hii leo polisi imezuia uzinduzi wa mikutano hiyo iliyopangwa kufanyika katika ukumbi mmoja ikimtaka mwanasiasa huyo kwanza atimize masharti waliomwekea.

Polisi iliweka vizuizi na ulinzi mkali kwenye barabara zote zinazoelekea eneo ambapo Bobi Wine na wafuasi wake walipanga kuzindua mikutano ya mashauriano katika ukumbi kama alivyoagizwa. Licha ya kuwa Bobi Wine na wenzake wanasisitiza  wamekuwa wakiwasiliana na polisi kuhusu mkutano wao, naibu msemaji wa polisi Polly Namaye amewambia waandishi habari  kwamba wamezuia mkutano huo kufanyika kwa sababu kuna vipengele kadhaa katika masharti aliyopewa mwanasiasa huyo  ambayo amekataa kuyatimiza.

Uganda Kampala Festnahme Bobi Wine
Mwanasiasa wa Uganda Bobi Wine akiwa amekabiliwa na polisi walipokuwa wakijaribu kuzuia mikutano yakePicha: Getty Images/AFP/Stringer

Miongoni mwa masharti aliyopewa Bobi Wine ni kuorodhesha jinsi atakavyoendesha mikutano yake bila kukiuka sheria ya mikutano ya hadhara maarufu kama POMA. Lakini Bobi Wine amelezea kuwa huo si wajibu wake kupanga usalama ila ni jukumu la polis kama waliovyoafikiana na tume ya uchaguzi.

Kulingana na sheria na taratibu za uchaguzi, mtu anayetaka kugombea wadhifa wa urais hupewa idhini na tume ya uchaguzi kuendesha mikutano ya mashauriano. Mara ya kwanza Bobi Wine alidaiwa kukosa kufuata maagizo lakini polisi pia wakakosolewa kwa kutumia nguvu za kupindukia kuivunja mikutano yake. Baada ya makubaliano miongoni mwa pande zote tatu, Bobi Wine alianzisha maandalizi ya mikutano. Lakini Poilisi bado haijaonyesha kuridhishwa na mipango yake. 

Aidha siku ya leo, Bobi Wine alifika mahakamani pamoja na wafuasi wake kujibu mashtaka ya mwaka 2018 kuhusiana na kuendesha mikutano isiyo halali. Makundi ya wafuasi wake waliovalia mavazi mekundu walizuiliwa kuingia eneo la mahakama huku wengine wakiendesha maandamano.

Katika kisa kimoja cha makabiliano na polisi waliokuwa wakifyatua risasi na mabomu ya kutoa machozi, mwanamke mfuasi wa Bobi Wine amegongwa na karandinga ya polisi walipokuwa wakiwatimua. Hadi wakati wa kuandaa taarifa hizi makundi ya wafuasi yalikuwa yakielekea hospitali kuu ya Mulago kudai maiti ya marehemu.

Lubega Emmanuel DW Kampala.