1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi wakabiliana na waandamanaji nchini Kenya

Josephat Charo18 Januari 2008

Upinzani wapania kuzigomea biashara zenye mafungamano na serikali ya rais Kibaki

https://p.dw.com/p/CuPB
Polisi nchini Kenya wakabiliana na waandamanaji mjini MombasaPicha: AP

Upinzani nchini Kenya umesema utaanzisha mgomo wa kiuchumi dhidi ya kampuni zilizo na mafungamano na serikali baada ya kuongoza maandamano ya mwisho hii leo kuhusu matokeo ya uchaguzi uliofanyika tarehe 27 mwezi uliopita.

Msemaji wa serikali ya Kenya dakta Alfred Mutua amepuuza njama hiyo ya upinzani akisema kila mkenya ana haki ya kufanya atakavyo lakini mkakati huo hautafaulu.

Polisi wa kupambana na fujo na wanajeshi wa vikosi maalumu wameshika doria mjini Nairobi na katika ngome za upinzani magharibi mwa Kenya.

Duru za polisi zinasema watu wasiopungua 14 wameuwawa katika maandamano ya siku tatu yaliyoiotishwa na upinzani.

Leo wapatanishi wawili wamefanya mazungumzo na viongozi wa upinzani kujaribu kuutanzua mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini Kenya. Kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, amekutana na Graca Machel, mke wa rais wa zamani wa Afrika Kusini, na rais wa zamani wa Tanzania, Benjamin Mkapa, na kuwaeleza matakwa ya chama chake cha ODM kwa rais Kibaki.

Katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, anatarajiwa kuwasili mjini Nairobi Jumanne wiki ijayo.

Polisi nchini Kenya wamewakamata raia wawili wa kigeni, mjerumani na mholanzi kwa tuhuma za kuhusika na vitendo vya ugaidi. Raia hao wawili wanadai ni waandishi wa habari.

Polisi wamewatia mbaroni Andrej Hermlin Leder, mwenye pasi ya kusafiria ya Ujerumani, na Gerduwe Sleur van Dissel, aliyekuwa na pasi ya kusafiria ya Uholanzi, katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi wakati walipokuwa wakijaribu kuondoka nchini humo jana usiku.

Huko mjini Mombasa polisi wamelazimika kutumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya mamia kadhaa ya waandamanaji wa kiislamu wanaopinga ushindi wa rais Mwai Kibaki katika uchaguzi wa Disemba 27 mwaka uliopita.

Mandamanao ya leo yamefanyika baada ya sala ya Ijumaa katika msikiti mkuu mjini humo katika siku ya tatu na ya mwisho ya maandamano yaliyoitishwa na upinzani lakini yakapigwa marufuku na polisi.