1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi ya Charlotte yatoa vidio ya mauaji ya Scott

Mohammed Khelef
25 Septemba 2016

Polisi mjini Charlotte imetoa vidio za kupigwa risasi na kuuawa Keith Lamont Scott, baada ya siku kadhaa za maandamano na machafuko, huku ikiendelea kudai kuwa Mmarekani huyo mweusi alikuwa na silaha.

https://p.dw.com/p/2QZ9a
USA Proteste in Charlotte
Maandamano ya kudai kutolewa kwa vidio ya polisi wakati wakimpiga risasi na kumuua Mmarekani Mweusi, Keith Lamont Scott, katika mji wa Charlotte-Mecklenburg.Picha: picture-alliance/AP Photo/D. Laird/The Charlotte Observer

Kipande cha kwanza cha vidio hiyo iliyotolewa leo (Septemba 25) kwa vyombo kadhaa vya habari nchini Marekani na pia kutumwa mitandaoni, kinamuonesha Keith Lamont Scott akitoka kwenye gari moja na kurudi nyuma kwa miguu, wakati polisi wakimrushia risasi mara nne, lakini haiko wazi ikiwa alikuwa na silaha mkononi. Kipande cha pili kinamuonesha Scott akiwa amelala chini baada ya kupigwa risasi, huku maafisa wa polisi wakiwa wamemzunguka.

Awali, polisi ilikuwa imekataa kutoa vidio hiyo, huku ikidai kuwa Scott, mwenye umri wa miaka 43, alikuwa kitisho kwa maafisa wake. Lakini baadaye, mkuu wa polisi wa Charlotte-Mecklenburg, Kerry Putney, alibadilisha kauli yake, akiwaambia waandishi wa habari kwamba watu "wanataka kuuona ukweli, ukweli halisi. Na ndicho tunachowasilisha hapa."

"Watu wanaweza kutafsiri chochote wanachotaka kutokana na kipande kimoja cha ushahidi, na naweza kuwaambieni, nashuku watafanya hivyo, kwa kutegemea picha hii ya vidio. Lakini ninachosema ni kuwa munapaswa kuvikusanya vipande vyote pamoja," alisema.

"Scott alikuwa na bunduki na bangi" - Polisi

USA Polizei erschießt Afro-Amerikaner in North Carolina - Pressekonferenz
Mkuu wa Polisi wa Charlotte/Mecklenburg, Kerry Putney, akizungumzia kutolewa kwa vidio za mauaji ya Keith Lamont Scott.Picha: picture-alliance/AP Photo/C. Burton

Putney alisisitiza kuwa Scott alikuwa na bunduki ndogo na kuongeza pia kuwa alikuwa na bangi. "Maafisa wa polisi wanapoona silaha na wakaona pia bangi, huwa wanasema: 'ohoo, hili ni suala la usalama wetu na wa raia," alisema Putney. 

Polisi pia wameonesha picha ya bunduki ambayo wanasema alikuwa nayo Scott na pia msokoto mmoja wa bangi. Kwenye mkutano wake huo na waandishi wa habari, Putney alisema vipimo vya vinasaba pia vitatolewa baadaye.

Aliwaambia waandishi wa habari kwamba alitoa wito wa kutolewa kwa vidio hizo na taarifa nyengine, baada tu ya kuthibitisha kuwa "nikitoa nitakachotoa, hakutakuwa na athari mbaya dhidi ya uchunguzi wa Idara ya Upelelezi. Na sasa nina uhakika."

Katika taarifa yake, Gavana Pat McCrory alisema, akiwa kama gavana wa North Carolina, anakubaliana na uamuzi huo wa polisi kuzitoa vidio hizo. "Nimehakikishiwa na Idara ya Upelelezi kwamba kutolewa kwake hakutakuwa na athari za moja kwa moja kwa uchunguzi huru." Kufuatia siku kadhaa za machafuko, tayari gavana huyo alikuwa ameshatangaza amri ya kutotoka nje nyakati za usiku kwenye mji huo. 

Familia bado yataka majibu

USA Polizei erschießt Afro-Amerikaner in North Carolina - Proteste
Maandamano dhidi ya mauaji ya Wamarekani Weusi yanayofanywa na Marekani katika mji wa Charlotte Picha: picture-alliance/AP Photo/G. Broome

Awali, familia ya Scott ilikuwa imetoa vidio ya dakika mbili iliyopigwa na mkewe kwa simu ya mkononi, ambayo haioneshi upigwaji risasi wenyewe na ambayo haijibu moja kwa moja suali la endapo mumewe alikuwa na bunduki mkononi.

"Lengo letu tangu awali limekuwa ni kupata ukweli usiochujwa, na njia pekee ya kuupata ni kwa polisi kutoa vidio ambazo wametoa leo. Kwa bahati mbaya, tumeachwa na maswali zaidi kuliko majibu yake," Ray Dotch, kaka wa mkewe Scott, aliwaambia waandishi wa habari.

"Hatupaswi kumuonesha kama mwanaadamu sana ili atendewe haki, lakini alikuwa raia wa Marekani aliyestahili jambo jema zaidi ya hili. Huo ndio msimamo wetu. Na unapaswa pia kuwa wenu."

Mwanasheria wa familia ya Scott, Justin Bamberg, aliwaambia waandishi wa habari kwamba licha ya kutolewa kwa picha hizo mpya za vidio, bado haiwezekani "kutambua waziwazi kitu alichokuwanacho mkononi, kama kweli alikuwa nacho, na ukweli huo haujabadilika." 

Mauaji ya Scott yaliyotokea siku ya Jumanne (Septemba 20) yamesababisha machafuko kwenye mji huo wa kusini mwa Marekani, ambako waandamanaji wameingia mitaani kuilazimisha polisi kutoa vidio hiyo.

Scott alipigwa risasi na kuuawa kwenye eneo moja mjini Charlotte wakati wa makabiliano na polisi waliokuwa wakimsaka mtu mwengine waliyetaka kumkamata. Polisi inasema alikuwa na bastola mkononi, lakini familia yake inasema alikuwa amekamata kitabu. 

Kifo cha Scott ni sehemu tu ya mauaji kadhaa dhidi ya Wamarekani Weusi yakitendwa na polisi, na ambayo yamezua ghadhabu kote nchini Marekani.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP
Mhariri: Isaac Gamba