1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi yawaondoa watu kupisha uteguaji bomu Berlin

Lilian Mtono
20 Aprili 2018

Mamlaka za hapa Ujerumani zimeanza mchakato wa kulitegua bomu la uzito wa kilogram 500, lililoangushwa na Uingereza wakati wa vita vya pili vya dunia, lililogundulika wakati shughuli za ujenzi zikiendelea.

https://p.dw.com/p/2wO03
Deutschland Bombenentschärfung in Berlin
Picha: Reuters/A. Schmidt

Mamlaka za hapa Ujerumani zimeanza mchakato wa kulitegua bomu la uzito wa kilogram 500, lililoangushwa na Uingereza wakati wa vita vya pili vya dunia, lililogundulika wakati shughuli za ujenzi zikiendelea mnamo siku ya Jumatano. Zaidi ya wakaazi 10,000 pamoja na wafanyakazi watalazimika kuondoka kwenye eneo hilo kupisha shughuli hiyo ya uteguaji. 

Shughuli ya kuwaondoa watu kwenye majengo yaliyoko mita 800 kutoka eneo lilikokutikana bomu hilo imeanza majira ya saa tatu asubuhi ya leo ili kuruhusu shughuli ya kulitegua bomu hilo kuanza. Kituo kikuu cha treni cha mjini Berlin ni miongoni mwa maeneo ambayo watu waliondolewa, na kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa 8 mchana kituo hicho hakitakuwa na shughuli yoyote.

Uteguaji wa bomu hilo ulipangwa kufanyika majira ya saa 5.30 asubuhi, lakini ilitegemea kumalizika kwa shughuli hiyo ya kuwaondoa watu kwanza.

Idadi ya watu walioondolewa mjini Berlin ni kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika miaka ya hivi karibuni, kwa kuwa eneo lilikogundulika bomu hilo liko karibu sana na maeneo yalipo majengo ya serikali, hivyo maeneo yatakayoguswa ni pamoja na wizara ya kilimo, sehemu ya wizara ya usafirishaji na idara ya ujasusi ya taifa pia itaguswa. Maeneo mengine yatakayoguswa na hatua hiyo ni wizara ya uchumi na jengo la makumbusho kubwa ya kihistoria.

Mwandishi wa shirika la habari la Ujerumani la DW, Rebecca Ritters aliyekuwa kwenye eneo hilo mjini Berlin amesema kugundulika kwa mabomu ambayo hayakulipuka si jambo geni kwa hapa Ujerumani, ambapo zaidi ya tani 2,000 za mabomu na silaha zilizochimbiwa ardhini kote nchini hapa zikichimbuliwa kila mwaka, ikiwa ni zaidi ya miongo saba baada ya kumalizika kwa vita vya pili vya dunia. 

Berlin Entschärfung einer Fliegerbombe aus dem Zweiten Weltkrieg
Wataalamu wa mabomu mjini Berlin wakiwa katika shughuli ya uteguaji wa bomu hilo.Picha: picture-alliance/dpa

Hii si mara ya kwanza kwa matukio kama haya kujitokeza Ujerumani.

Ritters ameripoti akisema, na hapa namnukuu "hii ni kawaida kutokea hapa Berlin, kawaida kuna mabomu mengi ambayo hayajateguliwa hapa..lakini kwa ujumla huwa si karibu na katikati ya mji. tuko mita 300-400 kutoka kituo kikuu cha treni, na kituo hicho kitafungwa kabisa, na safari zote za treni zitahamishwa," mwisho wa kumnukuu. Safari zote zitaishia kwenye vituo vingine vya treni vya Berlin.

Huduma za usafiri wa mabasi na treni za chini ya ardhi pia umeathirika mjini Berlin, na barabara ambazo ambazo zinaunganika na eneo ambako bomu hilo la Kiingereza liligundulika pia zimefungwa.

Polisi iliandika kwenye ukurasa wake wa twitter hapo jana kwamba bomu hilo lilikuwa katika hali nzuri, na halikuonyesha kuwa lingeweza kuwa na madhara.

Zaidi ya mamilioni ya tani za mabomu yaliyoangushwa ardhini wakati wa vita vya pili vya dunia, na zaidi ya moja ya kumi ya mabomu hayo yanasemekana kuwa bado hayajateguka.

Mtaalamu wa masuala ya mabomu katika eneo hilo, amemwambia mwandishi huyo wa habari kwamba mabomu kama haya yasipohamishwa huwa hayana madhara kama hayatahamishwa, lakini mara yanapoanza kuhamishwa yanaweza kuwa si salama, na ndio maana mamlaka inachukua tahadhari kubwa. 

Mwaka jana, takriban watu 60,000 walihamishwa kutoka kwenye makaazi yao mjini Frankfurt ili kupisha shughuli ya kuchimbua bomu kubwa lililoangushwa na ndege za kijeshi za Uingereza.

Mwezi Mei mwaka jana, zaidi ya watu 50,000 pia walihamishwa kutoka katika maeneo ya mji wa kaskazini mwa Ujerumani wa Hannover ili kupisha shughuli kama hiyo ya uteguaji wa bmu lililoangushwa katika enzi ya vita vya pili vya dunia.

Mwandishi: Lilian Mtono/APE/RTRE/DW

Mhariri: Mohammed Khelef