1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pwani ya Kenya kukombolewa kiuchumi

Sudi Mnette
16 Agosti 2018

Huko Mjini Mombasa nchini Kenya , Viongozi wa kisiasa kutoka ukanda wa Pwani wanataka kukomesha kasumba ya siasa za ufuasi na  badala yake kutafuta mustakabali wa maendeleo ya kisiasa na kichumi ya Kanda hiyo .

https://p.dw.com/p/33GGy
Wahlen in Kenia 2017 - Governor von Mombasa Joho
Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho akihutubia wajumbe wa mkutano NairobiPicha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Wakati wa kongamano lililowaleta pamoja waakilishi wa Wadi kutoka majimbo yote sita ya  Pwani, viongozi hao wameazimia kuunda Jumuiya ya Watu wa pwani, Kauli Mbiu ikiwa "Pwani Kwanza” na lengo kubwa likiwa ni kupeleka mbele maendeleo ya kiuchumi na kisiasa kupitia jumuiya hiyo.

Pwani kwanza ni kauli mbiu ya wajumbe waliokusanyika mjini Mombasa kutafuta mstabali wa maendeleo kisiasa na Uchumi wa ukanda huu wa Pwani. Kileleni mwa kongamano hilo chini ya uongozi wake Gavana wa Jimbo la Mombasa Ali Hassan Joho na Mwenzake wa Jimbo la Kilifi Amason Kingi, limetoa maazimio matatu yanayoashiria mstakabali huo wa Kisiasa na hata kiuchumi.

Viongozi wa Pwani ya Kenya kiini cha matatizo

Kenia - Muslime in Mombasa
Wakazi wa Mombasa katika viunga vya jijiPicha: picture-alliance/dpa/A. Gebert

Kwanza kabisa mkutano huu ulijadili kwa kina mshikamano wa kisiasa miongoni mwa viongozi wake ambao wanatajwa kuwa pingamizi kubwa na chanzo cha masaibu yanayowakumba wakaazi wake. Ajenda ya pili iliyochochea hisia za washiriki wengi ni kiwango cha umaskini na jinsi ya kulikomboa eneo hili la Ukanda wa Pwani kiuchumi huku Gavana wa Jimbo la Mombasa Hassan Joho akiweka bayana kwamba adui mkubwa wa matatizo haya ni viongozi wenyewe.

Maazimio hayo matatu yaliyofikiwa mwishoni mwa mkutano huo sasa yanalenga kubuni Jumuiya itakayoyaleta sio umoja tu wa wapwani bali kutafuta mbinu za kuleta pamoja rasilimali na kubuni soko kubwa kwa waekezaji wa ndani na hata kutoka nje ya Ukanda huo.

Kuundwa chombo cha utatuzi wa matatizo

Ili kuafikia hayo, kongamano hili limekubali kwa kauli moja kuunda jopo la Wataalam litakaloshughulikia masuala haya ingawa mbali na maazimio hayo, siasa pia zilitawala kongamano hilo. Joho alikosoa vikali kile alichotaja kuwa siasa za ufuasi miaka nenda miaka rudi akimlenga Naibu wa Rais William Ruto ambaye kagtika siku za hivi karibuni amekuwa akizuru ukanda wa Pwani katika ziara zake ambazo zimekuja kufahamika na Wakenya wengi kwa jina "Tangatanga”, kutaka uungwaji Mkono katika juhudi zake za kuwa mgombea urais mwaka wa 2022.

Katika siku za hivi karibuni Gavana wa jimbo hilo la Mombasa na mwenzake kutoka jimbo la Kilifi Amason Kingi wametangaza azma yao ya kuwania Urais ifikapo uchaguzi mkuu mwaka wa 2022. Na ili kupata uungwaji mkono katika siasa za kitaifa, kuna umuhimu mkubwa kwanza kupata uungwaji mkono katika ngazi za mashinani anasema Gavana Amason Kingi.

Mkutano huu ulihudhuriwa na waakilishi wa Wadi kutoka mirengo yote mikuu ya kisiasa, ukiwa ule wa Jubilee unaoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na ule wa Orange Democratic unaoongozwa na Raila Odinga, Joho akiwa Naibu wake. Hii si mara ya Kwanza eneo hilo la  Pwani kutangaza mipango hiyo, Na tayari wachanganuzi wa masuala ya siasa wanasema kuwa, hatua hiyo inatarajiwa Zaidi kutoa muelekeo wa kisiasa kwa ukanda huo wa Pwani, ifikapo uchaguzi mkuu mwaka wa 2022.

Mwandishi: Eric Ponda
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman