1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Qatar ina saa 48 zaidi kutimiza masharti ya nchi za kiarabu

Caro Robi
3 Julai 2017

Nchi za kiarabu ambazo zimesitisha uhusiano wa kidiplomasia na Qatar zimekubali kurefusha muda wa Qatar kutimiza masharti iliyowekewa. Kuwait ambayo ni mpatanishi katika mzozo huo, ilipendekeza Qatar ipewe muda zaidi.

https://p.dw.com/p/2fnyL
Katar Außenminister
Picha: Getty Images/AFP/K. Jaafar

Qatar sasa ina saa 48 kutimiza masharti iliyowekewa la sivyo huenda ikawekewa vikwazo zaidi. Waziri wa mambo ya nje wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani anatarajiwa kutoa tamko rasmi leo kuhusu hatua hiyo ya hivi punde kuhusiana na mzozo huo.

Qatar imesema leo itamueleza Mfalme wa Kuwait Sheikh Sabah al Hamad Al Sabah ambaye ndiye mpatanishi wa mzozo huo wa ghuba msimamo wake kuhusu masharti dhidi yake kupitia barua itakayowasilishwa na Sheikh Mohammed.

Hatma ya Qatar itakuwa ipi?

Mawaziri wa mambo ya nje wa Misri, Umoja wa falme za kiarabu, Bahrain na Saudi Arabia watakutana Cairo Jumatano wiki hii kujadili ni hatua zipi zaidi watazichukua dhidi ya Qatar.

USA Saudi Arabien Donald Trump mit König Salman bin Abdulazi
Mfalme Salman wa Saudi Arabia(kushoto) na Rais wa Marekani Donald Trump(kulia)Picha: Imago/ZUMA Press/S. Craighead

Miongoni mwa masharti 13 ambayo Qatar imeekewa ni kukoma kuunga mkono udugu wa Kiislamu, kufunga kituo cha televisheni cha Al Jazeera, kupunguza uhusiano wa kidiplomasia na Iran na kuifunga kambi ya kijeshi ya Uturuki iliyoko Qatar.

Mbali na kitisho cha kufurushwa kutoka baraza la ushirikiano wa nchi za ghuba lenye nchi wanachama sita, haijabainika wazi ni vikwazo gani zaidi Qatar huenda ikawekewa iwapo itashindwa kutimiza matakwa ya nchi hizo.

Rais wa Marekani Donald Trump amezungumza kwa njia ya simu na viongozi kadhaa wa nchi za ghuba leo kuhusu mzozo huo unaoendelea kati ya Qatar na baadhi ya majirani zake akiwemo mfalme wa Saudi Arabia Salman bin Abdulaziz Al Saud, mwana wa mfalme wa Abu Dhabi Mohamed bin Zayed all Nahyan na mfalme wa Qatar Tamin bin Hamad Al Thani.

Marekani imesema inasisitiza umuhimu wa kuwepo umoja katika kanda hiyo ya ghuba ili kuweza kufikia lengo la kuushinda ugaidi na kuimarisha uthabiti katika kanda hiyo. Hata hivyo Trump ametaka kusitishwa ufadhili wa vitendo vya kigaidi na itikadi kali.


Ujerumani yahimiza umoja

China Außenminister Sigmar Gabriel
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar GabrielPicha: Getty Images/L. Zhang

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel ambaye leo anaanza ziara ya siku tatu katika mataifa kadhaa ya kiarabu ametoa wito wa kufanyika mazungumzo ya kina kuumaliza mzozo uliopo akisisitiza Ujerumani haiegemii upande wowote katika mzozo huo.

Gabriel amesema wanatiwa wasiwasi na kutoaminiana na kutokuwepo umoja, mambo ambayo huenda yakaliyumbisha eneo zima la ghuba na kuathiri sio tu nchi za kiarabu bali pia maslahi ya Ujerumani na nchi nyingine.

Waziri huyo wa Ujerumani leo anaizuru kwanza Saudi Arabia, kisha Umoja wa Falme za nchi za kiarabu, kabla ya hapo kesho kuelekea Qatar. Jumatano ataizuru Kuwait.

 

Mwandishi: Caro Robi/afp/ap/dpa

Mhariri:Iddi Ssessanga