1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Abbas atimiza miaka 10 madarakani

Josephat Nyiro Charo13 Januari 2015

Rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina Mahmoud Abbas anakamilisha miaka 10 madarakani Alhamisi (15.01.2015) akiipa changamoto kubwa Israel. Atakutana na viongozi wa Jumuiya ya nchi za Kiarabu Cairo, Misri.

https://p.dw.com/p/1EJZk
Porträt Mahmoud Abbas 26. April 2014
Rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina, Mahmoud AbbasPicha: Reuters

Baada ya muongo mmoja uongozini kiongozi huyo hana mengi ya kujivunia kwani bado angali mbali sana kuufikia mkataba wa kuundwa dola huru la Palestina. Abbas ameshindwa kuukomboa Ukanda wa Gaza kutoka kwa wapinzani wake kisiasa, chama cha Hamas, na anaonekana na wengi kama mlinzi wa masilahi ya kiusalama ya Israel katika Ukingo wa Magharibi.

Abbas mwenye umri wa miaka 79 anayejulikana kwa jina la utani "Abu Mazen" alibadili mkondo siku chache kabla kuadhimisha miaka kumi madarakani Alhamisi wiki hii kwa kusaini mkataba wa kutaka kujiunga na mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC. Hatua hiyo yumkini ikaruhusu malalamiko na mashtaka ya uhalifu wa kivita dhidi ya Israel katika kile ambacho wengi wanaamini ni mkakati wa mwisho wa kiongozi huyo.

Hatua ya kujiunga na mahakama ya ICC ni sehemu ya mkakati mpana ambao Wapalestina wanatumai utaleta shinikizo la kimataifa dhidi ya Israel na kuimarisha nafasi yao katika mazungumzo ya kudai taifa lao huru katika siku za usoni. Wapalestina wanasema hatua hiyo imetokana na hali ya kukata tamaa kufuatia miongo miwili ya kushindwa kwa mazungumzo ya kutafuta amani yaliyosimamiwa na mshirika mkubwa wa Israel, Marekani.

Abbas lawamani

Israel inamlaumu Abbas kwa kujaribu kutumia kampeni ya kulifanya taifa la Kiyahudi kuwa lisilo halali badala ya kuendelea na mazungumzo. Hatua hiyo ina athari zisizo mithili, lakini maafisa wa Palestina wanasema rais Abbas alilazimika kuchukua hatua.

Abbas unterzeichnet Statut zum IStGH 31. Dez. 2014
Abbas akisaini mkataba wa Roma ulioiunda ICCPicha: Reuters

"Sisi tuwadhaifu na njia pekee tunayoweza kuitumia ni kurejesha harakati za kuitetea Palestina kwa jumuiya ya kimatiafa," alisema afisa mmoja wa ngazi ya juu aliyezungumza bila kutaka kutajwa jina akielezea maoni binafsi ya rais Abbas.

Wapalestina walio karibu na Abbas wanasema amekuwa chini ya shinikizo nchini kukabiliana na Israel tangu vita vya siku 50 vya msimu wa kiangazi mwaka uliopita katika Ukanda wa Gaza kati ya Israel na kundi la Hamas ambapo zaidi ya Wapalestina 2,200 waliuwawa, wengi wao raia, pamoja na watu 72 upande wa Israel.

Alikuwa na chaguo ima awasikilize watu na uongozi na washauri wake, au ajitenge mwenyewe zaidi," amesema Hanas Ashrawi, afisa mwandamizi wa Chama cha Ukombozi wa Palestina, PLO, ambaye mara kwa mara hupewa taarifa na rais Abbas.

Abbas atakuwa Cairo

Katika siku ya maadhimisho ya miaka 10 madarakani, Abbas aliyeapishwa mnamo Januri 15 mwaka 2005, atakuwa mjini Cairo nchini Misri, kuwasihi viongozi wa Jumuiya ya nchi za Kiarabu watimize ahadi yao kuipa mamlaka ya ndani ya Palestina euro milioni 100 kufidia pengo lililosababisha na hatua ya Israel kuzuia malipo ya kila mwezi ya kiasi cha dola milioni 120 kama kodi inayotozwa na Israel kwa niaba ya Wapalestina, kwa hatua yake ya kujiunga na ICC. Mataifa ya kiarabu yameshawahi kuzivunja ahadi za aina hiyo katika siku za nyuma.

USA Mittlerer Osten Friedensgespräche Benjamin Netanyahu und Mahmoud Abbas
Abbas (kulia) na NetanyahuPicha: CHRIS KLEPONIS/AFP/Getty Images

Iwapo mamlaka ya ndani ya Wapalestina itasambaratika kutokana na matatizo ya kifedha yaliyosababishwa na vikwazo vilivyowekwa na Israel, Israel kama nchi inayoyakalia maeneo ya Wapalestina itakuwa na dhamana ya kutoa huduma kwa Wapalestina, kibarua ambacho kina gharama kubwa. Israel pia itapoteza ushirikiano na Abbas katika masuala ya usalama, ambao umesaidia sana kuepusha mashambulizi ya wanamgambo.

Nathan Thrall mchambuzi wa shirika la kimataifa la kukabiliana na mizozo, ICG, amesema anaamini Israel inataka mamlaka ya ndani ya Palestina kuendelea na shughuli zake na haitamchukulia Abbas hatua kali mno. Kwa kujiunga na mahakama ya ICC, Abbas pia alilitilia maanani suala hilo.

Abbas hajatangaza nia ya kuondoka madarakani. Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu naye kwa upande wake anatafuta kuchaguliwa tena kwa awamu ya tatu katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Machi 17 mwaka huu. Iwapo Netanyahu atashinda, rais Abbas ataimarisha kampeni ya kutaka utambulisho zaidi wa Palestina katika Ukingo wa Magharibi, Ukanda wa Gaza na Jerusalem Mashariki, maeneo yaliyotekwa na Israel mwaka 1967.

Mwandishi: Josephat Charo/APE

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman