1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Bashir awasili Chad kwenye kikao cha CEN-Sad

22 Julai 2010

Serikali ya Chad imemuhakikishia Rais Omar Hassan al-Bashir wa Sudan kwamba hana cha kuogopa akiwa ziarani nchini humo, kutokana na waranti wa kukamatwa kwake uliotolewa mwaka uliopita na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu

https://p.dw.com/p/ORU9
Rais wa Sudan Omar Hassan al BashirPicha: AP Photo


Rais al-Bashir yuko Chad kuhudhuria mkutano wa jumuiya ya mataifa ya Sahel na Sahara,CEN-SAD.

Chad imetoa matamshi hayo baada ya Marekani kuitolea wito nchi hiyo kutekeleza masharti ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu-ICC na kumkamata Rais Omar Hassan al-Bashir wa Sudan. Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani alisema hata hivyo, wanaiachia serikali ya Chad kueleza ni kwa nini haijachukua hatua ya kumkamata kiongozi huyo wa Sudan. Ziara hiyo ya Rais al-Bashir ni ya kwanza kuifanya katika nchi inayoitambua mahakama hiyo ambayo tayari imetoa waranti mbili za kukamatwa kiongozi huyo wa Sudan. Akizungumza katika kituo cha televisheni ya Chad, Rais Idriss Deby wa nchi hiyo alisema kuwa yeye na mgeni wake wamefungua ukurasa mpya katika historia ya nchi hizo mbili kwa maslahi ya wananchi wao na kwamba nchi hiyo haina mpango wa kumkamata.

Nchi huru

Flash-Galerie Internationaler Strafgerichtshof in Den Haag ICC
Majaji wa mahakama ya ICCPicha: AP

Maafisa wa Chad walitetea uamuzi wao wa kutomkamata Rais al-Bashir. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Chad, Ahmat Mahamat Bachir, aliliuliza shirika la habari la AFP iwapo kuna nchi ambayo imewahi kumkamata kiongozi wa nchi aliye madarakani na kuongeza kuwa Rais Bashir hawezi kukamatwa akiwa Chad. Waziri Bachir alisema Chad ni taifa huru na linasimamia shughuli zake bila kuzingatia masharti ya mashirika ya kimataifa. Naye Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Chad, Moussa Faki Mahamat amesema Rais al-Bashir amealikwa Chad kuhudhuria mkutano akiwa kama mwanachama wa jumuiya hiyo ya mataifa ya Sahel na Sahara, hivyo hana chochote cha kuogopa.

Makubaliano ya Roma

Chad imesaini makubaliano ya Roma,hati iliyotumiwa kuanzisha mahakama ya ICC, ambayo inaiwia nchi hiyo kumkamata mtu yeyote anayetakiwa na mahakama hiyo akiwa nchini humo. Waziri Mahamat alisisitiza kuwa Chad inafuata uamuzi wa Umoja wa Afrika unaomruhusu Rais al-Bashir kufanya ziara, uamuzi ambao ulifikiwa na umoja huo baada ya waranti kutolewa. Waranti wa kwanza wa kukamatwa Rais Al-Bashir ulitolewa mwezi Machi mwaka uliopita ukimtuhumu kwa kuhusika na uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu. Hata hivyo, mashitaka hayo yaliongezwa na kuwa mauaji ya halaiki katika waranti wa pili uliotolewa mwanzoni mwa mwezi huu.

Kwa upande wake mahakama ya ICC imesema Chad ina wajibu wa kumkamata Rais al-Bashir. Msemaji wa ICC, Fadi El Abdullah ameiambia AFP kuwa mataifa yote yaliyoridhia mkataba wa Roma yana wajibu wa kushirikiana na mahakama hiyo. Jimbo la Darfur limekuwa likitatizwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 2003 ambavyo vimewaua kiasi watu 300,000 na kuwaacha wengine milioni 2.7 bila makaazi. Takwimu hizo ni kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, ingawa Sudan imekuwa ikisisitiza kuwa ni watu 10,000 tu ndio waliuawa.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFP)

Mhariri:Mwadzaya,Thelma