1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Bush awasili Saudi Arabia

Josephat Charo14 Januari 2008

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy akamilisha ziara yake nchini Saudi Arabia

https://p.dw.com/p/CpXg
Rais Bush (kushoto) na mwanamfalme wa Abu Dhabi Sheik Mohamed Bin Zayed Al Nahyan alipokuwa Abu DhabiPicha: AP

Rais George W Bush wa Marekani amewasili nchini Saudi Arabia ambako anatarajiwa kukutana na mfalme Abdullah Abdel Aziz mjini Riyadh. Rais Bush amewasili mjini Riyadh akitokea Dubai, kituo cha mwisho cha ziara yake ya mataifa ya jumuiya ya falme za kiarabu. Wakati huo huo rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy amekamilisha ziara yake nchini Saudi Arabia na ameelekea Qatar.

Swala la Iran, amani ya Mashariki ya Kati na demokrasia katika eneo hilo yamekuwa maswala muhimu katika ajenda ya rais Bush wakati wa mazungumzo yake na viongozi wa Saudi Arabia. Ziara ya kwanza ya rais Bush nchini humo inafanyika wakati utawala wake ukiwasilisha pendekezo bungeni la kutaka kuiuzia Saudi Arabia silaha za thamani ya dola bilioni 20 za kimarekani, ikiwa ni pamoja na mabomu ya kuvurumishwa kutumia vifaa vya kisasa.

Tangazo hilo limetangazwa kuenda sambamba na kuwasili kwa rais Bush mjini Riyadh. Mshauri wa maswala ya usalama wa kitafa wa Marekani, Stephen Hadley, amewaambia waandishi wa habari waliokuwa katika ndege iliyombeba rais Bush, Air Force One, kwamba uuzaji wa silaha hizo ni mkakati wa Marekani kuimarisha ulinzi wa washirika wake nchini Saudi Arabia na mataifa mengine yanayotoa mafuta katika eneo la ghuba dhidi ya kitisho cha Iran.

Rais Bush amesema Iran ni nchi inayoongoza duniani katika kudhamini ugaidi.

Alipokuwa Abu Dhabi, rais Bush ameisifu nchi hiyo hivyo kuendeleza sifa zake kwa nchi za ghuba na kuendelea kuikosoa Iran. Akifanya ziara yake ya kwanza Mashariki ya Kati tangu alipochukua madaraka nchini Marekani rais Bush anafanya juhudi za kutafuta uungwaji mkono kwa mazungumzo ya kutafauta amani kati ya Israel na Palestina na kuitenga Iran. Amelilaumu kundi la al Qaeda kwa kuvuruga demokrasia katika eneo hilo.

Iran ni taifa ambalo si la kiarabu lakini lina ushawishi mkubwa katika eneo hilo, ulioongoezeka baada ya mazungumzo ya kirafiki kati yake na Saudi Arabia na makubaliano ya kibiashara yaliyosainiwa kati ya nchi hizo mbili. Rais Bush amesema Marekani inaziongezea nguvu mpya juhudi zake za kuwalinda washirika wake katika eneo la ghuba na kuwaleta pamoja marafiki wa Marekani duniani kote kukabiliana na kitisho cha Iran.

Wakati wa ziara yake ya siku mbili nchini Saudi Arabia, rais Bush leo atakula chakula cha jioni na mfalme Abdulah na kufanya mazungumzo katika ikulu ya mjini Riyadh ambayo pia ni makazi binafsi ya mfalme huyo. Hapo kesho viongozi hao watakutana katika shamba la kifalme la Janadriyah, karibu na mji mkuu Riyadh, kabla rais Bush kuondoka kuelekea nchini Misri.

Wakati rais Bush akiwasili mjini Riyadh, rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy amekamilisha ziara yake nchini Saudi Arabia hii leo. Kiongozi huyo ameondoka mjini Riyadh kuelekea mjini Doha nchini Qatar. Rais Sarkozy amesema makampuni ya Ufaransa yatasaini mikataba mikubwa na serikali ya mjini Riyadh yenye thamani ya euro bilioni 40 lakini bila kufaulu kusaini mikataba kuhusu usalama.

´Ni mikataba mikubwa ya kiraia na kijeshi,´ amesema rais Sarkozy wakati alipozungumza na waandishi wa habari mjini Riyadh. Aidha kiongozi huyo akiwa katika ziara yake ya kwanza katika eneo la Ghuba tangu alipoingia madarakani mnamo mwezi Mei mwaka jana, amesema mikataba yote itasainiwa majuma au miezi michache ijayo.

Wajumbe wa Ufaransa na Saudi Arabia wamesaini mikataba minne ya ushirikiano katika maswala ya kisiasa na nishati na kuwasilisha mikataba mingine kuhusu miundombinu na maswala ya kijeshi ya gharama karibu euro bilioni 40.

Rais Sarkozy aliwasili nchini Saudi Arabia jana na kuzungumza na mfalme Abdullah ambaye leo amesema ana wasiwasi kuhusu kupanda kwa kasi kwa bei za mafuta ambazo zinaathiri ukuaji wa kiuchumi na uwezo wa kununua bidhaa.

Rais Sarkozy amekuwa rais wa pili wa Ufaransa kulihutubia baraza la Shura la Saudi Arabia lenye wanachama 150 wanaume watupu. Ameliambia baraza hilo kwamba Ufaransa inataka kuwa rafiki wa dhati wa Saudi Arabia sio tu wa kusema maneno matupu bali atakayesema ukweli. Ingawa ameisifu Saudi Arabia kwa kupiga hatua katika maswala kuhusu hali ya wanawake na uhuru wa kujieleza, rais Sarkozy amekiri kwamba bado kuna mengi yanayohitaji kufanywa.