1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Chiluba wa Zambia afariki

20 Juni 2011

Rais wa zamani wa Zambia, Frederick Chiluba, amefariki dunia usiku wa kuamkia Jumamosi nyumbani kwake, Lusaka akiwa na umri wa miaka 68.

https://p.dw.com/p/11fgo
Frederick Chiluba alikuwa Rais wa pili wa Zambia.Picha: AP

Serikali ya Zambia imetangaza kwamba Chiluba atazikwa tarehe 27 Juni katika mji mkuu wa Zambia, Lusaka. Katika tamko rasmi serikali pia ilitangaza wiki ya maombolezi ya kitaifa kuanzia Juni 20 hadi Juni 27. Katika kipindi hicho bendera zitapepea nusu mlingoti na shughuli zote za burudani na mapumziko zitaahirishwa. Vituo vya redio vya Zambia vimeagizwa kupiga nyimbo za taratibu tu katika juma hilo la maombolezi.

Chiluba alikuwa Rais wa Zambia kuanzia 1991 hadi 2001. Alipokea madaraka kutoka kwa Rais wa kwanza wa Zambia, Kenneth Kaunda, aliyeiongoza nchi hiyo kwa miaka 27. Alikuwa Rais wa kwanza wa Zambia kuingia madarakani kwa uchaguzi wa kidemokrasia. Kabla ya kuwa Rais, Chiluba alikuwa kiongozi wa chama cha wafanyakazi.

Baada ya kuapishwa kuwa Rais, Chiluba aliahidi kukuza demokrasia na kuendeleza juhudi za kutetea haki za binadamu nchini kwake. Chiluba pia alinia kuifanya serikali yake kuwa wazi zaidi. Lakini baada ya ya kukaa madarakani kwa muda, kiongozi huyo aliandamwa na shutuma za ubadhirifu wa mali ya umma. Chiluba alishtakiwa kwa madai ya kuiba fedha za serikali kiasi cha dola za Kimarekani 500,000 katika kipindi chake cha utawala.

Hata hivyo, mwaka 2008 alifutiwa mashtaka yote dhidi yake. Mwaka 2010 mahakama moja ya jijini London, Uingereza, ilimhukumu Chiluba na washauri wake kwa kujichukulia dola za Kimarekani 46 kutoka kwenye akiba za serikali. Mashtaka hayo pia yalifutwa na mahakama ya Zambia. Kama Chiluba angehukumiwa, ingempasa kuzirejesha fedha hizo.

Frederick Chiluba alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya moyo na figo kwa muda mrefu. Amemwacha mke aitwaye Regina, mke wake wa zamani Vera Tembo na watoto tisa. Kenneth Kaunda alikuwa miongoni mwa watu waliokuja kuomboleza nyumbani kwa Chiluba baada ya kifo chake. "Chiluba alikuwa kiongozi mzuri wa chama cha wafanyakazi na amefariki akiwa na umri mdogo," alisema Rais huyo wa zamani wa Zambia.  Marehemu Chiluba amefariki akiwa na umri wa miaka 68

Mwandishi: Elizabeth Shoo/AFPE

Mhariri: M.Abdul-Rahman