1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Jonathan anaongoza katika matokeo ya uchaguzi

Kabogo, Grace Patricia18 Aprili 2011

Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan anaongoza katika matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika mwishoni mwa wiki huku akiwa na zaidi ya kura milioni 22 ambazo tayari zimehesabiwa kutoka kwenye majimbo 35 kati ya 36.

https://p.dw.com/p/10vEn
Rais wa Nigeria aliyeko madarakani, Goodluck JonathanPicha: AP

Taarifa hiyo ni kwa mujibu wa matokeo yaliyotolewa jana Jumapili. Tume huru ya uchaguzi ya Nigeria bado inasubiri matokeo kutoka kwenye jimbo moja na maeneo mengine kadhaa.

Idadi kubwa ya karibu watu milioni 73 na nusu waliojiandikisha kupiga kura walijitokeza katika uchaguzi huo wa rais uliofanyika Jumamosi iliyopita.

Muhammadu Buhari Nigeria Wahl
Mpinzani mkuu wa Rais Goodluck Jonathan, Jenerali Muhammadu BuhariPicha: AP

Mpinzani mkuu wa Rais Jonathan, Muhammadu Buhari ambaye ni kiongozi wa zamani wa kijeshi, amepata kiasi kura milioni 11, nyingi zikiwa zimepigwa katika maeneo ya kaskazini ya nchi hiyo.

Katika taarifa ya awali ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi huo kutoka Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi-ECOWAS umeuelezea uchaguzi huo katika taifa hilo lenye idadi kubwa ya watu barani Afrika kuwa huru, wa haki na kuaminika. Matokeo rasmi ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutangazwa leo.