1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Karzai azindua mpango wa kuwalipa wapiganaji wa Taliban

Josephat Nyiro Charo22 Januari 2010

Mpango kutangazwa kwenye mkutano wa London wiki ijayo

https://p.dw.com/p/LeO8
Rais Hamid Karzai wa AfghanistanPicha: Picture-alliance/dpa

Rais wa Afghanistan Hamid Karzai amezindua mpango unaodhaminiwa na nchi za magharibi wa kuwalipa fedha na kuwapa ajira wapiganaji wa kundi la Taliban ili kuwashawishi waweke silaha zao chini na warudi katika maisha ya kawaida. Mpango huo umezinduliwa wakati Ujerumani ikitafakari kupeleka wanajeshi zaidi Aghanistan.

Rais wa Afghanistan Hamid Karzai amesema kwenye hotuba yake iliyoonyeshwa kwenye runinga hii leo kwamba raia Waafghanistan wanastahili amani kwa vyovyote vile. Huku mkutano wa kimataifa utakaojadili Afghanistan ukikaribia kufanyika mjini London Uingereza wiki ijayo, rais Karzai amesema wapiganaji wa kundi la Taliban watakaokubali kuwasilisha silaha zao na kuachana na mapigano watalipwa fedha, kupewa ajira, kulindwa na kuruhusiwa kuishi pamoja na jamii zao.

Hata hivyo chini ya mpango huo wafuasi wa kundi la Taliban wenye msimamo mkali wa kidini, na ambao zamani walikuwa wanachama wa kundi la al Qaeda au makundi mengine ya kigaidi, hawatakubaliwa.

Rais Karzai ameongeza kusema kuwa mpango huo unatarajiwa kutangazwa kwenye mkutano wa mjini London nchini Uingereza Alhamisi ijayo. Uongozi wa kundi la Taliban huwalipa mishahara minono wapiganaji wake wanaojitolea kuliko mishahara ambayo serikali ya Afghanistan inaweza kuwalipa wanajeshi wake. Rais Karzai amesema mpango wake mpya utaungwa mkono na jumuiya ya kimataifa kiasi cha kupata udhamini wa kutosha.

Viongozi wa kundi la Taliban mara kwa mara wamekataa kushiriki kwenye mazungumzo ya kusaka amani mpaka masharti yao yatimizwe. Mbabe wa kivita Gulbuddin Hekmatyar amesema leo kwamba yuko tayari kwa mazungumzo pamoja na serikali ya Afghanistan na wapatanishi kutoka Marekani, lakini kwa sharti kwamba wanajeshi wote wa kigeni walio nchini Afghanistan waondoke nchini humo.

Hii leo waandamanaji wamezifunga barabara na kupiga kelele kuilaumu Marekani na serikali ya Afghanistan kwa siku ya pili mfululizo kusini magharibi mwa mji mkuu Kabul, huku hasira ikiongezeka kufuatia mauaji ya watu wanne yaliyofanywa na jeshi la jumuiya ya kujihami ya NATO katika kijiji kimoja mkoani Ghazni.

Wakati haya yakijiri, serikali ya Ujerumani inatafakari kuongeza wanajeshi zaidi kwenda Afghanistan. Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Karl-Theodor zu Guttenberg, amesema leo kwamba hawezi kufutilia mbali uwezekano wa kuongeza wanajeshi zaidi kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa polisi ya Irak na kusaidia juhudi za kutoa misaada kwa Waafghanistan.

Bundestag Guttenberg Haushaltsdebatte
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Karl-Theodor zu GuttenbergPicha: picture alliance / dpa

Waziri huyo amesema idadi ya wanajeshi wa ziada watakaokwenda Afghanistan itatangazwa wiki ijayo, lakini maafisa wa ngazi ya juu katika wizara ya ulinzi wamenukuliwa wakisema idadi ya wanajeshi wa Ujerumani nchini Afghanistan itaongezeka kutoka 4,500 hadi 6,000.

Kura ya maoni hapa Ujerumani inadhihirisha wazi kuwa Wajerumani wengi wanaitaka serikali ya kansela Angela Merkel iwaondoe wanajeshi wa Ujerumani kutoka Afghanistan. Lakini serikali hiyo mjini Berlin imekuwa chini ya shinikizo la Marekani na uongozi wa jumuiya ya kujihami ya NATO.

Sambamba na hayo Finnland leo imesema itapeleka wanajeshi 50 zaidi kwenda Afghanistan hivyo kuoingeza idadi ya wanajeshi wake nchini humo kufikia 195.

Mwandishi:Josephat Charo/RTRE/AFPE/DPA

Mhariri: Othman Miraji