1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais mpya wa Ivory Coast kuapishwa leo

Kabogo Grace Patricia4 Desemba 2010

Rais huyo mpya wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo anaapishwa licha ya jumuiya ya kimataifa kutotambua ushindi wake.

https://p.dw.com/p/QPaz
Rais mpya wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo.Picha: AP

Ivory Coast inatarajia kuendelea na shughuli za kumuapisha rais mpya wa nchi hiyo, Laurent Gbagbo, licha ya kuwepo shinikizo kutoka jumuiya ya kimataifa. Rais Gbagbo aliyeko madarakani ataapishwa hii leo kwa ajili ya kuiongoza nchi hiyo.

Jana Ijumaa, Baraza la Kikatiba la Ivory Coast lilimtangaza Gbagbo kama mshindi wa uchaguzi wa rais nchini humo, ingawa tume ya uchaguzi ilimtangaza mpinzani wake Alassane Outtara kuwa mshindi wa uchaguzi huo.

Bado kuna hofu kuwa mgawanyiko wa kisiasa Ivory Coast huenda ukairejesha nchi hiyo katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoikumba nchi hiyo mwanzoni mwa muongo huu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa na Rais Barack Obama wa Marekani wamemtaka Gbagbo kukubali kuwa ameshindwa katika uchaguzi huo.

Rais Sarkozy amesema kuwa uchaguzi huo umeonyesha wazi ushindi kwa Ouattara na kwamba uamuazi wa tume ya uchaguzi unatambuliwa na jumuiya ya kimataifa na Umoja wa Mataifa.

Kiongozi huyo ya Ufaransa amewataka maafisa na viongozi wa kijeshi na kiraia nchini Ivory Coast kuheshimu matakwa ya wananchi na kuepukana na matukio yoyote ambayo yanaweza kuchochea vurugu.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo(AFP,RTR,DPA)

Mhariri: Mohamed Dahman