1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais mpya wa Lebanon amechaguliwa

Othman, Miraji27 Mei 2008

Jumapili iliopita, kwa mara ya kwanza baada ya kupita zaidi ya miezi 18, bunge la Lebanon lilikutana na kumchagua aliyekuwa mkuu wa majeshi, Michel Suleiman, kuwa rais wa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/E73n
Rais mpya wa Lebanon, Michel SuleimanPicha: AP


Kwa muda wote huo, nchi hiyo ilikuwa haina rais kwa vile pande mbili zilizokuwa zinapingana- ule wa serekali, ukiungwa mkono na Marekani na nchi za Kiarabu, kama vile Saudi Arabia, na ule wa upinzani, ukiongozwa na Chama cha Hizbullah na kuungwa mkono na Syria na Iran, zilikuwa hazijaafikiana katika mambo kadhaa juu ya katiba ya nchi hiyo, huku spika wa bunge, Nabih Berri, akiahirisha zaidi ya mara 19 kuitisha kikao cha bunge. Sherehe zilizokuwa pamoja na kufyetua risasi hewani zilisheheni katika mji mkuu wa Beirut pale spika wa bunge alipotangaza matokeo ya uchaguzi wa urais bungeni:


+Michel Suleiman amepata kura 118, kura tisa zimempinga.+


Na baada ya hapo Michel Suleiman alikula kiapo:


+Ninakula kiapo kwa jina la Mwenyezi Mungu Mtukufu kwamba nitailinda katiba ya Lebanon na sheria zake na nitalinda uhuru wa taifa la Lebanon na usalama wa ardhi yake.+


Nikimnukuu tena rais huyo mpya:


+Leo nikila kiapo cha kuilinda katiba, natoa mwito kwenu nyinyi nyote, makundi ya kisiasa na wananchi, tuanze kipindi kipya, jina la kipindi hicho ni Lebanon na Wa-Lebanon. Tujiambatanishe na mpango wa kitaifa tutakaofikia ili tupate maendeleo na ili tuyafikie yale yenye kulifaidia taifa na maslahi yake, kama kipa umbele, kuliko maslahi yetu ya kibinafsi na makundi yetu.+


Spika wa bunge, Nabih Berri, alikielezea kikao hicho kuwa ni kitendo cha masikilizano. Pia wawakilishi wa madola ya kigeni ambayo hayajachoka kujiingiza katika mzozo wa Libanon, ikiwa kwa heri au kwa shari, walisafiri hadi nchi hiyo, wakiwemo mawaziri wa mambo ya kigeni wa Saudi Arabia, Ufaransa, Syria na Iran.


Uchaguzi huo ulikuwa sehemu ya mapatano yaliosimamiwa na Qatar wiki iliopita huko Doha ili kuutuliza mzozo ambao uliisukuma Lebanon hadi katika ukingo wa vita vya kienyeji. Ilifika hadi wanamgambo wa Chama cha Kishia cha Hizbullah, kwa muda mfupi, kuzishikilia sehemu za Beirut na kuwashinda wafuasi wa serekali. Si chini ya watu 81 walikufa katika mapigano hayo.


Mapatano ya Doha yalionekana sana kama pigo kwa Marekani na washirika wake ambao walisisitiza kwamba wanamgambo wa Hizbullah wavuliwe silaha. Chama cha Hizbullah kimepinga hatua zozote zitakazopelekea wanamgambo wake wavuliwe silaha, kikishikilia kwamba silaha zao zinahitajika ili kuyazuwia mashambulio yeyote yale kutokea Israel. Lakini upande wa serekalki huko Beirut ulikariri wito wake kwa Washia hao wavuliwe silaha, ukitilia maanani mashambulio yaliofanywa Beirut mwezi huu.


Katika hotuba yake juu ya maudhui hayo, Rais Michel Suleiman alisema hivi:


+Bunduki itaelekezwa tu kwa adui na sisi hatutoruhusu kwamba bunduki hiyo ielekezwe upande mwengine.+


Mapatano hayo yametaja juu ya haja ya kuweko sheria mpya ya uchaguzi itakayofanya kazi katika uchaguzi wa bunge hapo mwakani. Angalau kundi la upinzani linaloongozwa na Hizbullah limepata mafanikio, hasa kwa vile sasa lina kura ya turufu katika maamuzi ya serekali mpya. Waziri mkuu wa Qatar, al-Thani, akiutangaza muwafaka wa Doha:


+Kwanza pande zimekubaliana kutoa mwito kwa spika aitishe bunge likutane kuchaguzi mtetezi aliyekubalika, Michel Suleiman, kuwa rais wa nchi. Ilikubaliwa kwamba hiyo ndio njia ilio bora kabisa kwa upande wa kikatiba kumchagua rais katika hali hii ya sasa isiokuwa ya kawaida. Pili: Iundwe serekali ya Umoja wa Taifa ikiwa na mawaziri 30, mgawo ukiwa mawaziri 16 kutoka upande wa walio wengi, na 11 kutoka upinzani, na watatu wateuliwe na rais.+


Kuchaguliwa rais mpya ina maana serekali iliokuweko chini ya waziri mkuu Fuad Siniora imejiuzulu. Fuad Siniora anabaki kuwa waziri mkuu wa kujishikiza.


Kiongozi wa wabunge wengi, Saad al-Hariri, mtoto wa yule waziri mkuu aliyeuliwa mwaka 2005, Rafiq al-Hariri, ndiye mtu anayetazamiwa sana kuwa waziri mkuu mpya.Lakini magazeti ya mjini Beirut yanakisia kwamba Fuad Siniora huenda ikambidi akamate tena wadhifa huo, kwani hiyo serekali ijayo itakuwa ya kujishikiza pia, mwaka mmoja kutoka sasa kutafanyika uchaguzi wa bunge.


Chini ya mfumo mgumu wa kugawana madaraka huko Lebanon, rais wa nchi huwa wa kutoka madhehebu ya Kikristo ya Maronite, waziri mkuu wa madhehebu ya Kiislamu ya Sunni, na spika wa bunge ni wa kutoka madhehebu ya Kiislamu ya Shia. Michel Suleiman anakamata nafasi iliokuwa inashikiliwa na Emile Lahoud ambaye alikuwa mshirika wa Syria.


Hilal Khashan, mtaalamu wa siasa katika Chuo Kikuu cha Kimarekani cha mjini Beirut, anamtathmini Rais Suleiman kama hivi:


+Ukiangalia tabia yake katika miaka iliopita, yeye hanivutii kama mwanasiasa. Ni taabu kwa afisa wa jeshi kuvuka na kuwa mwanasiasa. Marehemu Hafidh al-Asad alikuwa mtu mwengine+


Lakini maoni haya yanapingwa na Elias Hanna, jenerali wa zamani wa jeshi la Lebanon, akisema:


+Kwamba ana mtandao wa mawasiliano na makundi yote, Hizbullah na pia serekali, inafanya awe mtu anayeweza kubinya ili kuweko na wizani katika mambo yote.+


Angalau sasa yaonesha malumbano ya kisiasa huko Lebanon yatahama kutoka mabarabarani na kurejea katika taasisi za dola. Hivyo, msingi muhimu wa suluhisho la mwenendo wa kisiasa utajengwa.


Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi za Kiarabu, Arab League, uliotoa mchango mkubwa katika kufikiwa mapatano haya, Amr Musa, alikuw ana haya ya kusema:


+Nataka kuashiria na kuhakikisha kwamba ttumefikia katika suluhisho ambalo hakuna aliyeshinda wala aliyeshindwa. Na jambo hili ni muhimu. Tumehakikisha kwamba mfumo wa kihistoria wa Lebanon ambao umejengeka kwa kutokuweko aliyeshinda na aliyeshindwa ndio mfano mzuri pekee ambao utatuwezesha tusonge mbele.+


Wachunguzi wa mambo wanataja jambo jingine muhimu, nalo ni kwamba mapatano ya Doha yasingefikiwa bila ya kutolewa ishara kutoka Syria na Iran, wafadhili wakubwa wa Chama cha Hizbullah.


Nayo Marekani, japokuwa imetangaza inakaribisha uchaguzi wa Michel Suleiman, lakini inajulikana kwamba watawala wa Washington hawajafurahi Wa-Hizbullah, watu waliowapiga mhuri kuwa magaidi na walio wakorofi, watakuwemo ndani ya serekali mpya ya Beirut, na kwamba Hassan Nasrallah, kiongozi wa Hizbullah, amechomoza kama mshindi katika sakata hili.


Nao ufalme mdogo wa Qatar, ulioko katika Ghuba la Uajemi na ulio na utajiri wa nishati, umepata umaarufu kwa kuwa mpatanishi. Umeonesha vipi unavoweza kujisogeza mbele katika majukwaa ya kimataifa, licha ya udogo wake.