1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Obama na mkakati mpya kuhusu hali nchini Afghanistan

30 Septemba 2009

<p>Rais Barack Obama wa Marekani leo atakutana na washauri wake wakuu, kubadilishana mawazo iwapo mkakati mpya nchini Afghanistan unahitaji mabadiliko.

https://p.dw.com/p/JuRg
Rais Barack Obama wa MarekaniPicha: AP
Kamanda mkuu wa majeshi ya Marekani nchini Afghanistan, Generali Stanley McChrystal aliwasha moto pale ripoti yake ya siri ilipofichuka akionya kuna uwezekano mkubwa wa Marekani kushindwa nchini Afghanistan, katika mwaka mmoja ujao, iwapo hawataongeza idadi ya wanajeshi.

Ishara ya umuhimu wa mkutano, huo na usiri wake inajitokeza wazi, ukiangalia orodha ya waliopata mualiko na eneo mkutano huo unafanyika. Eneo ni chumba chenye usalama mkuu katika Ikulu ya Marekani.

Mkutano huo unaolenga kutathmini mkakati wa Marekani nchini Afghanistan, na wapi panapohitajika mabadiliko, hasa kuhusiana na swala la kuongezwa kwa idadi ya wanajeshi, maamuzi yake yatachangia iwapo Marekani itakuwepo Afghanistan kwa muda mrefu.

Rais Obama atakaa mezani na washauri wake wakuu, ikiwemo, Makamu wa rais Joe Biden, Waziri wa mambo ya nchi za nje Hillary Clinton, na Robert Gates anayesimamia wizara ya ulinzi.  Generali Stanley McChrystal, kamanda mkuu wa majeshi ya Marekani Afghanistan, pia anasemekana atahudhuria au kama sivyo atashiriki katika majadiliano hayo kwa njia ye video.

Hillary Clinton
Waziri wa mambo ya nchi za nje Bibi. Hillary ClintonPicha: picture alliance / abaca

Rais Obama amekuwa na shinikizo nyingi, kubadili mweleko nchini Afghanistan, na hasa baada ya ripoti ya McChrystal kufichuka. McChrystal alikuwa anaonya katika muda wa mwaka mmoja ujao, Marekani huenda ikashindwa huko Afghanistan iwapo haitaongeza idadi ya wanajeshi. McChrystal anasemekana ameitisha wanajeshi wengine kiasi cha elfu 40 kukabiliana na uasi wa Taliban unaozidi.

Mkakati Afghanistan pia ulikuwa ndio ajenda katika mkutano wa Rais Obama na katibu mkuu wa Nato, Anders Rasmussen katika ikulu ya Marekani- alipoashiria kuwa Marekani inahitaji ushirikiano zaidi kutoka nchi za Ulaya.

NATO-Generalsekretär Anders Fogh Rasmussen
Katibu Mkuu wa NATO Jenerali Anders Fogh RasmussenPicha: AP

Washirika wakuu wa Marekani Ulaya bado wana shaka, hasa kuhusiana na kuongeza idadi ya wanajeshi, Afghanistan. Jana Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Franz Josef Jung, alisema  washirika wa NATO barani Ulaya wanafaa, kusubiri hadi pale Marekani itakapotoa mpango rasmi wa kuongezwa kwa wanajeshi Afghanistan.

Deutschland Bundesverteidigungsminister Franz Josef Jung
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Franz Josef JungPicha: AP

Anders Rasmussen lakini alimhakikishia rais Obama kuwa majeshi ya NATO Afghanistan yataendelea kuwepo , hadi watakapokamilisha kazi iliyowapeleka nchini humo.

Kura ya maoni nchini Marekani zinaashiria kuwa Wamarekani wengi wamepoteza imani na vita hivyo Afghanistan. Ni changamoto hizi ndizo Rais Obama ataendelea kupima kabla ya kufanya maamuzi, wa mkakati ufaao nchini Afghanistan.

Mwandishi: Munira Muhammad/AFPE

Mhariri: Abdul-Rahman