1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Vladimir Putin afanya ziara China

Abdu Said Mtullya20 Mei 2014

Rais Vladimir Putin wa Urusi ameanza ziara nchini China. Putin anaifanya ziara hiyo wakati wizara ya ulinzi ya Urusi imefahamisha kwamba vikosi vya nchi hiyo vilivyowekwa karibu na mpaka wa Ukraine vimeanza kuondoka.

https://p.dw.com/p/1C30z
Rais wa Vladimir Putin wa Urusi na Rais Xi Jinping wa China
Rais Vladimir Putin wa Urusi na Rais Xi Jinping wa ChinaPicha: Reuters

Ziara ya Rais Putin nchini China inazingatiwa kuwa ni ishara kwa nchi za maghairibi kwamba Urusi inaziimarisha juhudi za kuwatafuta washirika wengine.Katika ziara hiyo Putin atakutana na Rais Xi -Jinping wa China .Baada ya mazungumzo ya muda mrefu Urusi na China zinadhamiria hatimaye kufikia mapatano juu ya Urusi kuiuzia China gesi kwa kipindi cha muda mrefu.

Mikataba ya biashara zaidi ya 40

Rais Putin leo pia anatarajiwa kukutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ambae pia yupo mjini Shanghai kuhudhuria mkutano wa nchi za Asia juu ya masuala ya usalama. Katika ziara yake nchini China Rais Putin atatiliana saini mikataba 43 na China.Pamoja na miradi mingine itakayotekelezwa na nchi mbili hizo ni uundaji wa pamoja wa Helikopta na ndege za abiria.

Majeshi ya Urusi yaondolewa

Wakati huo huo nchini Urusi wizara ya ulinzi imefahamisha kwamba wanajeshi wa nchi hiyo waliowekwa karibu na mpaka wa Ukraine wameanza kuondoka. Agizo la kuondolewa kwa wanajeshi hao lilitolewa hapo jana na Rais Putin.

Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema askari wa nchi hiyo waliowekwa katika majimbo ya Bryansk,Belgorod na Rostov wameanza kuondoka na kurejea katika kambi zao za nyumbani. Hata hivyo Marekani na Nato zinazokadiria kwamba Urusi imewaweka wanajeshi alfu 40 karibu na mpaka wa Ukraine hazijathibitisha iwapo Urusi imewaondoa wanajeshi wake.

Mwito wa kuwakabili wanaharakati wanaotaka kujitenga

Katika kadhia nyingine tajiri mkubwa kabisa wa Ukraine Rinat Achmetov ametoa mwito kwa watu wa kulikabili vuguvugu la wanaotaka kujitenga nchini kote .Tajiri huyo aliewahi kuwa mshirika mkubwa wa Rais alieondolewa madarakani V.Yanukovich amezishutumu hatua zinazochukuliwa na wanaotaka kujitenga na amewataka watu katika majimbo husika wajihami wenyewe.

Mfanyabiashara huyo anaemiliki viwanda vya chuma na migodi katika jimbo la Donbas hivi karibuni aliwapeleka wafanyakazi wake ili kuwasaidia polisi katika mapambano ya kuyarejesha mamlaka ya jimbo hilo katika mikono ya Ukraine. Amewataka watu wa mashariki mwa Ukraine waachane na matendo ya uasi. Lakini waharakati wanaoegemea Urusi wameendelea kupambana na majeshi ya serikali ya Ukraine katika vitongoji vya jimbo la Slavyansk.

Mwandishi:Mtullya Abdu.ape/dpa

Mhariri:Yusuf Saumu