1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa China Xi Jinping ziarani Ujerumani

28 Machi 2014

Rais wa jamhuri ya umma wa China Xi Jinping amewasili mjini Berlin kwa ziara rasmi ya siku tatu itakayomfikisha pia katika jimbo lenye wakaazi wengi zaidi la Ujerumani North Rhine Westphalia.

https://p.dw.com/p/1BXgt
Rais wa China Xi Jinping na mkewe akikaribishwa na rais wa Ujerumani Joachim Gauck(kulia) na mpenzi wake Daniela Schadt (kushoto)Picha: Reuters

Rais Xi Jinping anaefuatana na mkewe Peng Liyuan na ujumbe wa mawaziri 20 na wakuu 200 wa makampuni ya kiuchumi ya jamhuri ya umma wa China amepokelewa kwa heshima za kijeshi na rais Joachim Gauck na kukaribishwa katika kasri la Bellevue.Kwa mara ya kwanza kabisa suala la haki za binaadam litajadiliwa wakati wa mazungumzo kati ya rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Joachim Gauck na mgeni wake wa kutoka China.

Leo jioni rais Xi Jinping amepangiwa kukutana na kansela Angela Merkel ambapo migogoro ya kimataifa inatazamiwa kugubika mazungumzo yao sawa na masuala ya kiuchumi.

Sebastian Heilmann wa taasisi ya mjini Berlin inayoshughulikia mafunzo kuhusu China-Merics anahisi kipeo cha mazungumzo atakayokuwa nayo rais wa jamhuri ya umma wa China nchini Ujerumani ni cha aina mpya."Hivi sasa imechomoza hali ambayo masuala ya siasa ya usalama na siasa ya dunia yanazingatiwa.Na jambo hili ni jipya katika mikutano ya kilele kama hii kuzungumzia masuala muhimu yanayohusiana na usalama.Na katika uhusiano kati ya Ujerumani na China pia hili ni jambo jipya."Anasema Sebastian Heilmann wa taasisi ya Merics.

Masuala ya biashara na uchumi yatazingatiwa pia

Licha ya masuala yanayohusiana na siasa za kimataifa,yale ya kiuchumi na biashara pia yatapewa umbelepia wakati wa mazungumzo kati ya rais wa jamhuri ya umma wa China Xi Jinping na kansela Angela Merkel.

Deutschland China Xi Jinping zum Staatsbesuch in Berlin
Rais Xi Jinping akipokea heshimu za kijeshi alipowasili katika uwanja wa ndege wa Tegel mjini BerlinPicha: picture-alliance/dpa

Biashara kati ya nchi hizi mbili inakadiriwa kufikia Euro bilioni 150,takriban thuluthi moja ya biashara jumla ya China pamoja na umoja wa ulaya.

Uhusiano kati ya Ujerumani na China ni imara kwa namna ambayo umefikia daraja ya "Ushirikiano wa kimkakati".Ujerumani inasifiwa nchini China kuwa mshirika wa kutegemewa na mlango wa kuingia Ulaya.

Northrhine Westphalia Kitovu cha Ushirikiano wa kiuchumi na China

Katika ziara hii ya kwanza nchini Ujerumani tangu achaguliwe,rais Xi Jinping na ujumbe wake atalitembelea pia jimbo lenye wakaazi wengi la North Rhine Westphalia, kitovu cha ushirikiano wa kiuchumi kati ya China na Ujerumani kama waziri mkuu wa jimbo hilo bibi Hannelore Kraft anavyosema.

Hannelore Kraft SPD
Waziri mkuu wa jimbo la North Rhine Westphalia bibi Hannelore Kraft wa chama cha SPDPicha: Reuters

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/AFP

MhaririYusuf Saumu