1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Senegal ashinda muhula wa pili madarakani

Sylvia Mwehozi
28 Februari 2019

Rais Macky Sall wa Senegal ameibuka mshindi kwa kupata asilimia 58 ya kura katika uchaguzi wa rais uliofanyika tarehe 24 mwezi huu, na kuwapiku wapinzani wake wakuu.

https://p.dw.com/p/3EGgz
Senegal Präsidentschaftswahlen | Macky Sall
Picha: picture-alliance/Xinhua News Agency/D. Gueye

Ushindi huo wa zaidi ya asilimia 50 unampa Sall muhula wa pili madarakani bila ya kufanyika duru ya pili ya uchaguzi. Haikuwa wazi ikiwa wapinzani wake wa karibu watakubali matokeo hayo au watayapinga mahakamani. Kwa mujibu wa matokeo yaliyotolewa na tume ya uchaguzi, mpinzani wa karibu Idrissa Seck ambaye ni waziri mkuu wa zamani wa Senegal amepata asilimia 20.5 ya kura na Ousmane Sonko akipata asilimia 16 ya kura.

Tangu siku ya Jumapili wagombea wa upinzani walikataa ripoti za ushindi wa Sall, wakisema matokeo waliyo nayo yanaelekea katika raundi ya pili ya kura.

Seck na Sonko hadi sasa hawajatoa tamko juu ya matokeo yaliyotolewa na tume ambayo ni ya awali kabla hayajadhibitishwa na baraza la kikatiba. Wagombea hao wana masaa 72 ya kukata shauri mahakamani.

Senegal Präsidentschaftswahlen
Mpiga kura akitimiza haki ya msingi ya kupiga kura Picha: picture-alliance/AA/A. Dogru

Sall mwenye miaka 57 alikuwa akitafuta kuchaguliwa muhula wa pili ili kuendeleza rekodi yake ya ujenzi wa barabara na kutengeneza ajira.

Senegal imekuwa nchi ya kuigwa mfano katika demokrasia magharibi mwa Afrika. Waangalizi wa uchaguzi wameripoti kuwa hapakuwa na kasoro kubwa katika uchaguzi uliofanyika siku ya Jumapili.

Hata hivyo kura ya mwaka huu iligubikwa na madai ya kwamba rais aliwazuia wanasiasa wawili wakubwa wa upinzani kushiriki uchaguzi huo, ambao ni meya wa zamani wa mji mkuu wa Dakar na mtoto wa rais wa zamani Abdoulaye Wade.

Sall ambaye makundi ya kutetea haki za binadamu yanamshutumu kwa kuwakandamiza wapinzani wake alikuwa amepigiwa upatu kuibuka mshindi kwa kuuoboresha uchumi wa Senegal katika awamu ya kwanza madarakani kwa asilimia 6, ikitajwa kuwa miongoni mwa ukuaji mkubwa barani Afrika. Zaidi ya asilimia 66 ya wapiga kura milioni 6.7 waliojiandikisha walishiriki uchaguzi wa Jumapili.