1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel na Sarkozy wanataka kuepuka mgawanyiko.

Kitojo, Sekione9 Juni 2008
https://p.dw.com/p/EGU3
Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy na kansela wa Ujerumani Angela Merkel wakitabasamu baada ya kukaribishwa kwa gwaride la kijeshi katika mji wa Straubing nchini Ujerumani kabla ya kuanza mazungumzo yao..Picha: AP



Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy wameanza kikao chao cha siku moja katika mji wa Traubing , kusini mwa Ujerumani wakati mataifa hayo mawili yakijaribu kuepuka mgawanyiko baina yao.



Ujerumani imekiri kabla ya mkutano huo katika mji ulioko kusini mwa Ujerumani wa Straubing kuwa hakuna matumaini kwa wakati huu ya kutatua mzozo mkubwa kuhusiana na mipango ya umoja wa Ulaya ya upunguzaji utoaji wa gesi zinazochafua mazingira kutoka katika magari.

Umoja wa Ulaya unataka kuweka kiwango cha mwisho cha utoaji wa gesi ya carbon cha gram 120 kwa kilometa moja kwa gari zote mpya katika umoja huo ifikapo 2012 kama sehemu ya juhudi za kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Serikali ya Merkel inapinga vikali mipango hiyo kwa kuwa magari yaliyotengenezwa na makampuni makubwa ya Ujerumani kama BMW, Daimler na Porsche yanaonekana kuwa makubwa zaidi, na ya kifahari na yanayotoa gesi hizo kwa wingi.

Ufaransa hata hivyo inaunga mkono sheria hiyo kwa kuwa makampuni makubwa ya uundaji wa magari nchini humo kama Peugeot na Renault yanaonekana kuunda magari madogo ambayo yanatoa gesi hizo kwa kiasi kidogo.

Msemaji wa serikali ya Ujerumani amesema kuwa ripoti iliyotolewa siku ya Ijumaa kuwa mzozo huo umepatiwa ufumbuzi si za kweli na kudokeza kuwa kuna majadiliano yanayoendelea , na ambayo ni magumu na yenye utata. Suala hilo ni moja kati ya mengi yaliyoathiri uhusiano baina ya Merkel na Sarkozy tangu alipoingia madarakani mwaka jana na kujumuisha mzozo wao kuhusiana na pendekezo la Sarkozy la muungano na mataifa yanayopakana na bahari ya Mediterranean. Hata hivyo Sarkozy anamsifu sana Merkel.

Amesema kuwa kwake yeye anaona ni bahati , kwamba ameweza kufanyakazi mkono kwa mkono na Angela Merkel. Ni mwanamke ambaye namuheshimu. Ni jasiri, mwerevu, na ambaye katika muda wa miezi 12 nimeweza kukutana nae mara 12.

Kuhusu suala la kujumuika na mataifa yanayopakana na bahari ya Mediterranian , Merkel anaona kuwa hizo ni juhudi za kuitenga Ujerumani , na Sarkozy hatimaye alipendekeza kulifungua eneo hilo kwa mataifa yote ya Ulaya. Lakini wachunguzi wa mambo wanasema kuwa mkutano kuhusiana na mradi huo utakaofanyika mwezi Julai utaonyesha iwapo muafaka bado upo.

Suala lingine muhimu linaloleta mvutano katika mkutano wa leo litakuwa pendekezo la hivi karibuni la Sarkozy kuweka ukomo wa kodi ya thamani ya mauzo kwa mafuta katika eneo lote la umoja wa Ulaya ili kuzisaidia nchi hizo kupambana na ongezeko la bei ya mafuta. Pendekezo hilo lilipokelewa bila shauku na Merkel.

Nakubaliana na pendekezo la kufanyakazi kwa pamoja , amesema Merkel. Lakini inategemea na hatua zenyewe ambazo zinaelezwa. Tunapaswa kuona iwapo tunaweza kukubaliana katika jambo ambalo linaelekeza katika lengo letu.

Inaeleweka kwamba baina yetu sisi wawili, kila mara tunakubaliana wakati karata zinapokuwa mezani.

Ufaransa itachukua urais wa mataifa ya umoja wa Ulaya kutoka Slovenia ifikapo Julai mosi, ambapo Ujerumani imesema kuwa itaunga mkono kwa kadri ya uwezo wake urais huo wa miezi sita , wakati wote wa kipindi hicho cha uongozi wa Ufaransa.

Katika mahojiano na gazeti la mjini Straubing, ameikaribisha nia ya Sarkozy ya kutaka kupatikana kwa mkataba miongoni mwa mataifa 27 wanachama wa umoja wa Ulaya kuhusiana na uhamiaji na hifadhi ya kisiasa. Pia amedokeza kuwa Ufaransa itakuwa na kazi ya kuongoza juhudi za umoja wa Ulaya dhidi ya ongezeko la ujoto duniani na kusema kuwa kunahitajika mgawanyo sawa wa jukumu hilo.


►◄