1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Ujerumani ziarani China

17 Mei 2010

Rais wa Ujerumani Horst Köhler, ameanza ziara yake ya siku nne nchini China ambako atakutana na rais mwenzake, Hu Jintao na Waziri Mkuu Wen Jiabao mjini Beijing,kabla ya kutembelea Expo 2010 mjini Shanghai.

https://p.dw.com/p/NQFS
Ankunft Bundespräsident Köhler in Beijing 17.05.2010 Beginn 2. Staatsbesuch Köhlers in China
Rais wa Ujerumani,Horst Koehler akiwasili Beijing, kwa ziara yake rasmi ya pili nchini China.Picha: DW

Kilele cha ziara ya Rais Köhler nchini China ni maonyesho ya kimataifa ya Expo 2010 mjini Shanghai ambako atatembelea banda la kitaifa la Ujerumani na mabanda manne mengine ya miji ya Hamburg, Bremen, Düsseldorf na Freiburg. Vile vile atatembelea banda la pamoja la Ujerumani na China.Lakini Rais Köhler anaifungua ziara yake mjini Beijing kwa kukutana na rais mwenzake wa China, Hu Jintao, na Waziri Mkuu Wen Jiabao.

Kwa mujibu wa duru za serikali, Rais Köhler vile vile atakutana na Rais wa Benki Kuu ya China, Zhou Xiaochuan. Kwenye mkutano huo, Rais Köhler aliewahi kuwa mwenyekiti wa Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, anatazamiwa kujadili mzozo wa fedha na suala la kupandishwa thamani ya sarafu ya China, Yuan. Kwani China inaiacha chini, thamani ya sarafu hiyo, kinyume na thamani yake halisi. Kwa kufanya hivyo, China inanufaika kiuchumi kwani inaweza kuuza bidhaa zake kwa bei nafuu katika masoko ya kimataifa. Licha ya kushinikizwa na nchi za magharibi na hasa Marekani,China inakataa kupandisha thamani ya sarafu yake.

Katika ziara yake hiyo nchini China, Rais Köhler amefuatana na ujumbe wa wafanya biashara na mameneja wa makampuni makubwa ya Kijerumani, kama Siemens. Wajerumani hao watakutana na waakilishi wa sekta ya kiuchumi ya China katika Wizara ya Viwanda na Teknolojia ya Mawasiliano.

Miaka ya hivi karibuni, Ujerumani na China ziliudhiana kidiplomasia. Mwaka 2007 China ilikasirishwa sana na uamuzi wa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kumpokea kiongozi wa kidini wa Tibet, Dalai Lama, katika ofisi yake mjini Berlin. Serikali ya Ujerumani pia mara kwa mara huikosoa China kuhusu hali ya haki za binadamu.

Mashirika yanayotetea haki za binadamu-"Amnesty International" na "Maripota wasiojali Mipaka", yameitumia ziara ya Rais Köhler kusisitiza hali mbaya ya haki za binadamu nchini China. Verena Harpe wa Amnesty International katika mahojiano yake na kituo cha redio cha Deutschlandfunk amesema, "adhabu ya kifo ingali ikitumika na inatolewa sana. Watu waliozuiliwa huendelea kuteswa na makundi ya wachache na vyombo vya habari vinakandamizwa."

Ziara hii ya Rais Köhler inapalilia uhusiano mwema kati ya Ujerumani na China kwani yeye anawavutia zaidi Wachina kuliko Kansela Merkel anaeikosoa China.

Mwandishi:Ricking,Christoph/ZPR/P.Martin

Mhariri:Othman,Miraji