1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Urusi Dmitry Medvedev asaini mkataba wa kusitisha mapigano Georgia

Nijimbere, Gregoire16 Agosti 2008

Urusi imesaini mkataba wa kusitisha mapigano huku shinikizo zikizidi kuitaka iyaondowe majeshi yake kutoka Georgia.

https://p.dw.com/p/Eyas
Rais wa Urusi Dmitry MedvedevPicha: AP

Rais wa Urusi, Dmitry Medvedev, amesaini mkataba wa kusitisha mapigano ambao ni mpango wenye vifungo 6 uliopendekezwa na Umoja wa Ulaya. Rais wa Georgia, Mikhail Saakashvili, aliusaini mkataba huo ijumaa. Lakini majeshi ya Urusi bado yako nchini Georgia. Kuna taaruifa za kutatanisha juu ya majeshi hayo ya Urusi nchini Georgia. Baadhi ya taarifa zinasema majeshi hayo ya Urusi yamezidi kusonga mbele kuelekea mji mkuu wa Georgia wa Tbilisi licha ya kusainiwa mkataba huo wa kusitisha mapigano huku taarifa nyingine zikisema kuwa majeshi yameanza kurudi nyuma mara tu baada ya rais wa Urusi, dmitry Medvedev kutangaza kusitisha mapigano nchini Georgia. Urusi imekanusha taarifa kwamba imevunja daraja kwenye njia ya reli magharibi mwa Georgia. Mbali na hayo, hali ya kibinaadamu ndio inatia wasi wasi zaidi kutokana na ongezeko la watu waliolazimishwa na mapigano kuyahama maskani yao na ambao wanahitaji misaada ya dharura.

Peter Nicolaus wa Shirika la Umoja wa mataifa linalowahudumia wakimbizi la UNHCR, alisema:´´Hali yaonyesha imeanza kuboreka kwenye uwanja wa kisiasa lakini hali ya kibinaadamu imezidi kuwa mbaya. Sasa Tumehesabu wakimbizi wapya wa ndani laki 1 na alfu 15 ambao wameongezeka juu ya wale laki 2 na alfu 75 waliyokutwa kutokana na mizozo iliyopita. Mbali na hayo, uwezo wetu wa kutoa misaada umetatizwa na hali ya usalama na hatuwezi kutoka Tbilisi´´.

Mbali na mahitajio hayo ya kibinaadamu, raia kwenye maeneo yaliyokumbwa na mapigano wanakabiliwa na makundi ya wanamgambo wanaowaibia mali na kuwatesa raia kukiripotiwa hata vitendo vya ubakaji.

Marekani na Ujerumani zimesema Urusi ilitumia nguvu kupita kiasi na kuitaka iyaondowe majeshi yake kutoka Georgia. Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov, amesema hakuna ratiba ya kuwaondoa wanajeshi wao kutoka Georgia.

Wakati mzozo huo wa Georgia juu ya hatima ya majimbo ya Ossetia ya kusini na Abkhazia yanayopigania kujitenga na Urusi haujatulia kabisa, kumezuka suala jingine la makombora ambapo Poland imesaini mkataba na Marekani. Katika mkataba huo, marekani imeruhusiwa kuweka makombora 10 ya kunasa na kuteketeza makombora mengine kwenye mwambao wa Bahari ya Baltic. Na baada ya Poland, Ukraini nayo, imetangaza utayarifu wake wa kushirikiana na nchi za magharibi katika fani hiyo. Huenda suala hilo la makombora likazidisha mgogoro uliyopo sasa katika eneo zima.