1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Yemen ashinikizwa kungátuka madarakani

30 Mei 2011

Nchini Yemen jeshi limeshambulia mji wa Zanjibar uliotekwa na wafuasi wa al-Qaedai.Na katika mji mwingine,wakaazi wamesema, wanajeshi waliwafyatulia risasi waandamanaji na watu 20 waliuawa baada ya kupondwa na mabuldoza.

https://p.dw.com/p/RQsx
Yemeni President Ali Abdullah Saleh, attends an interview with selected media in Sanaa, Yemen, Wednesday, May 25, 2011. Yemen's embattled President Ali Abdullah Saleh issued messages of hard-line defiance Wednesday even as intense battles raged in the heart of the capital for a third day, saying he will not step down or allow the country to become a "failed state." (AP Photo/Mohammed Hamoud)
Rais Ali Abdullah Saleh wa Yemen akataa kujiuzuluPicha: dapd

Wasiwasi unazidi kuwa Yemen, iliyo jirani na Saudi Arabia, inaelekea katika vita vya wenyewe kwa wenyewe. Hofu hiyo imezuka baada ya wanajeshi sita kuuawa katika kile kinachodhaniwa kuwa ni shambulio la uvamizi. Shambulio hilo limetokea karibu na mji wa pwani wa Zinjibar uliotekwa na wanamgambo wa al-Qaeda siku chache zilizopita. Wakaazi wa mji huo wanasema, kufuatia mauaji hayo, vituo vya wanamgambo katika eneo hilo vilishambuliwa na ndege za kijeshi. Wakaazi wengi wa mji huo wa pwani,wanakimbia makwao ili kujiepusha na mapambano yaliyozuka kati ya wanamgambo wa al-Qaeda na wenyeji wa mji huo na vikosi vya serikali. Wakaazi wanasema mji huo hauna maji wala umeme.

epa02589801 Yemeni anti-riot forces hold back anti-government protesters during a protest in the capital Sana_a, Yemen, on 18 February 2011. Thousands of government opponents clashed with supporters of Yemen's longtime President Ali Abdullah Saleh. At least four anti-government protesters were reportedly wounded in Sana'a, a day after three protesters were allegedly killed by Yemeni police in the southern port city of Aden. EPA/YAHYA ARHAB +++(c) dpa - Bildfunk+++
Vikosi vya usalama vyazuia maandamano ya wapinzani wa serikaliPicha: Picture-Alliance/dpa

Na katika mji wa Taiz, kusini ya mji mkuu Sanaa, vikosi vya usalama jana usiku vilifyatua risasi na mabomu ya kutoa machozi ili kuwatawanya wapinzani wa serikali. Kwa mujibu wa mpinzani mmoja, hadi waandamanaji 20 waliuawa katika mapambano hayo. Wapinzani wa serikali wamepiga kambi kwenye Uwanja wa Uhuru tangu mwezi wa Januari wakimtaka Rais Saleh an'gatuke madarakani. Miezi hii iliyopita, takriban watu 300 wameuawa katika maandamano ya kumshinikiza Saleh kuondoka madarakani baada ya kutawala kwa takriban miaka 33.

Katika tukio jingine,afisa mmoja katika wilaya ya Hadramawt kusini mashariki ya Yemen, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa vikosi vya usalama vya Yemen vinasaidia kuwatafuta wafanyakazi 3 wa Kifaransa wa mashirika ya misaada wanaokosekana tangu Jumamaosi iliyopita. Lakini hakuthibitisha iwapo wametekwa nyara. Lakini mjini Paris msemaji wa wizara ya mambo ya nje Bernard Valero amesema, sasa inazidi kuhofiwa kuwa watu hao wametekwa nyara.

Mataifa makuu yana wasiwasi kuwa Yemen iliyo na matatizo ya kifedha na inayotumiwa kama mahala pakujificha wanamgambo wa al-Qaeda, sasa huenda ikaishia kuwa nchi isiyoweza kutawaliwa na hivyo kuhatarisha eneo hilo lenye utajiri wa mafuta pamoja na Saudi Arabia-muuzaji mkubwa kabisa wa mafuta duniani. Wakati huo huo, viongozi wa upinzani wanamshutumu Rais Ali Abdullah Saleh wa Yemen kuwa kiongozi huyo, kwa makusudi, aliwaachilia wanamgambo wa al-Qaeda kuuteka mji wa Zinjibar ulio kwenye Ghuba ya Aden. Wanasema, lengo lake ni kuzusha wasiwasi katika kanda hiyo kwa matumaini kuwa ataungwa mkono kupiga vita ugaidi.

Mwandishi: Martin,Prema/rtre

Mhariri: Miraji Othman