1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa zamani wa Catalonia kufikishwa mahakamani

Grace Kabogo
26 Machi 2018

Rais wa zamani wa Catalonia, Carles Puigdemont anafikishwa mahakamani Ujerumani baada ya kukamatwa Jumapili hatua iliyozusha maandamano jimboni humo. Maelfu ya wafuasi wake wanaotaka kujitenga walipambana na polisi.

https://p.dw.com/p/2uyKS
Carles Puigdemont
Picha: Reuters/E. Vidal

Rais wa zamani wa jimbo la Catalonia, Carles Puigdemont leo anafikishwa mahakamani nchini Ujerumani, baada ya kukamatwa jana hatua iliyozusha maandamano katika jimbo hilo, ambako maelfu ya wafuasi wa wake wanaotaka  kujitenga walipambana na polisi.

Mahakama ya Ujerumani itaamua iwapo Puigdemont aendelee kubakia kizuizini wakati wakisubiri maamuzi mengine kuhusu mchakato wa kumrudisha Uhispania. Waendesha mashtaka wa mji wa Schleswig, hawajaelezea ni wapi kesi hiyo itakayokuwa ya faragha itafanyika, na haijabainika muda kamili wa kusikilizwa.

Maafisa wa Ujerumani wamesisitiza kwamba kesi hiyo inafanyika kwa misingi ya mfumo wa mahakama. Shirika la Ujerumani, DPA liliripoti kuwa Puigdemont alipelekwa katika gereza moja katika mji wa Neumuenster.

Neumünster JVA Carles Puigdemont inhaftiert
Gereza la Neumuenster anakoshikiliwa PuigdemontPicha: picture alliance/AP Photo/F. Moöter

Polisi wa Ujerumani walimkamata Puigdemont jana, baada ya kuvuka mpaka kutoka Dernmark kwa kuzingatia waranti wa kukamatwa kiongozi huyo akiwa popote barani Ulaya uliotolewa na Uhispania.

Kukamatwa kwa Puigdemont kumefanyika miezi mitano baada ya kiongozi huyo kuwakimbia waendesha mashtaka wa Uhispania ambao wanataka kumfungulia mashtaka ya uhaini na uasi kutokana na kura iliyopigwa na bunge la Catalonia ya kujitangazia uhuru wa jimbo hilo.

Kwa mujibu wa wakili wa Puigdemont, Jaume Alonso-Cuevillas, kiongozi huyo alikuwa njiani kuelekea Ubelgiji, ambako alikimbilia baada ya serikali kuu ya Uhispania kutangaza kuwa itachukua udhibiti kamili wa Catalonia.

Maelfu waandamana

Kesi hiyo inasikilizwa wakati ambapo maelfu ya watu waliandamana jana mjini Barcelona na kwenye miji mingine ya Catalonia, huku baadhi ya waandamanaji wakipambana na polisi. Mmoja wa waandamanaji Anna Jordi anasema hali ya kisiasa inazidi kuwa mbaya.

''Nadhani umefika muda muafaka wa kufanya mapinduzi ya kweli. Tunahitaji kuifanya nchi isimame kabisa. Tunapaswa kuzuia barabara na kuwafanya watu wabakie tu nyumbani, ili tuweze kuchukua udhibiti. Ni jukumu letu,'' alifafanua Anna. Zaidi ya raia 50 na polisi kadhaa walijeruhiwa katika maandamano hayo.

Wakati huo huo, makamu rais wa bunge la Catalonia, Josep Costa amelaani vikali hatua ya Ujerumani kumkamata Puigdemont. Akizungumza katika mahojiano na DW, Costa amesema kukamatwa kwake kumechochewa kisiasa na ana matumaini kwamba mahakama za Ujerumani zitayaona mashtaka dhidi yake yaliyochochewa kisiasa.

Spanien Barcelona Demonstration nach Inhaftierung von Puigdemont
Wananchi wakiandamana Barcelona kupinga kukamatwa PuigdemontPicha: Reuters/A. Gea

Costa amesema ilikuwa ni haki ya wananchi kuichagua serikali yao, na sio kuhusu uhuru. Amefafanua kwamba kwa sasa wana bunge ambalo lilichaguliwa mwezi Desemba na linajaribu kuichagua serikali. Amesema serikali kuu ya Uhispania inauingilia mchakato wa demokrasia wa Catalonia wakati ambapo inajaribu kuunda serikali.

Hata hivyo, Puigdemont alikuwa yuko huru kufanya ziara nchini Denmark, Uswisi na Finland, kama sehemu ya juhudi zake za kutafuta kuungwa mkono kutokana na harakati za kujitenga kwa jimbo la Catalonia.

Waranti wa kimataifa wa kukamatwa Puigdemont ulitolewa upya Ijumaa iliyopita, wakati kiongozi huyo akizuru Finland. Uhispania imetoa pia waranti wa kukamatwa kwa watu wengine watano wanaounga mkono harakati za kujitenga, ambao wameikimbia nchi hiyo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP, AFP, DPA, DW https://bit.ly/2pHl5lJ
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman