1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa zamani waBotswana Mongae ashinda tuzo ya Mo Ibrahim

Liongo, Aboubakary Jumaa20 Oktoba 2008

Rais wa zamani wa Botswana Festus Mongae leo hii ametangazwa kuwa mshindi wa tuzo ya uongozi bora barani Afrika iitwayo Mo Ibrahim.

https://p.dw.com/p/Fddw

Tuzo hiyo iliyoanzishwa mwaka jana na bilionea wa kisudan Mo Ibrahim inaendena na kitiota cha dola millioni tano, kiwango ambacho ni kikubwa kabisa kwa tuzo yoyote inayotolewa kwa mtu binafsi duniani.


Mbali ya kitita hicho cha fedha mshindi wa tuzo hiyo pia hupata kiasi cha dola laki mbili kwa kipindi cha maisha yake yote.


Festus Mongae mwenye umri wa miaka 69 ambaye aling´atuka kutoka katika uongozi mwezi April mwaka huu baada ya kumaliza kipindi chake kwa mujibu wa katiba, anasifika kwa kutumia vizuri mapato ya Almasi kuwaneemesha wananchi wa nchi yake.


Botswana ambayo ukubwa wake ni sawa na Ufaransa inaongoza kwa utoaji wa Almas duniani na ni nchi yenye kiwango cha juu cha pato la ndani barani Afrika.


Akitangaza ushindi wa Rais huyo wa zamani wa Botswana, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Koffi Annan ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya uteuzi wa washindi wa tuzo hiyo alimpongeza pia kwa juhudi kubwa za kupambana na maradhi ya ukimwi katika nchi hiyo.


Botswana ni miongoni mwa nchi ambazo zimeathirika sana na ukimwi duniani, lakini kutokana na uongozi wa Festus Mongae kiwango cha madhara kimeshuka sana.


Hii ni mara ya pili kwa tuzo hiyo kutolewa, mara ya kwanza ikiwa mwaka jana ambapo,Rais wa zamani wa Msumbiji Joachim Chissano ndiye aliyeshinda.


Kuteuliwa kwa Chissano kulitokana na juhudi zake za kurejesha amani na maendeleo nchini Msumbiji, nchi ambayo ilikuwa katika mika 16 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kuanzia mwaka 1976 hadi mwaka 1992.


Tajiri raia wa Sudan mwenye kumiliki makampuni ya mawasilino, Mo Ibrahim ameiweka tuzo hiyo kwa ajili ya viongozi wastaafu wa Afrika ambao wameheshimu na kutumia vyema madaraka yao katika kuwatumikia wananchi wao.


Mbali ya Koffi Annan ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya uteuzi, wajumbe wengine katika kamati hiyo ni pamoja na Rais wa zamani wa Finland Martti Ahatisaari ambaye ni mshindi wa mwaka huu wa nishani ya amani ya Nobel,Aicha Bah Diallo ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika la Elimu la Umoja wa Mataifa UNESCO, Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomic, Mohamed El Baradei, Rais wa zamani wa Ireland Mary Robinson na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja Nchi za Kiafrika OAU Dr Salim Ahmed Salim.