1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Yanukovich asakwa kwa mauaji

24 Februari 2014

Ukraine imetowa waranti wa kukamatwa kwa Rais aliyeondolewa madarakani Viktor Yanukovich kwa kuhusika na mauaji ya wananchi wakati nchi hiyo ikikabiliwa na jukumu la dharura kuuda serikali mpya na kumteuwa waziri mkuu.

https://p.dw.com/p/1BEN0
Rais aliyeondolewa madarakani wa Ukraine Viktor Yanukovich.
Rais aliyeondolewa madarakani wa Ukraine Viktor Yanukovich.Picha: picture-alliance/dpa

Kaimu waziri wa mambo ya ndani wa Ukraine Arsen Avakov amesema leo hii kwenye mtandao wake wa Facebook kwamba kesi imefunguliwa rasmi kwa mauaji ya raia waliokuwa wakiandamana kwa amani na kwamba Yanukovich na watu wengine wanaohusika na mauaji hayo wanasakwa.

Asasi za usalama za Ukraine zimesema leo hii kwamba hazina taarifa juu ya mahali alipo Rais Yanukovich ambaye imeripotiwa kuwa alionekana huko Sevastopol mji wa bandari ulioko katika Rasi ya Crimea nchini Ukraine.

Baada ya kusaini makubaliano na upinzani ya kumaliza mzozo huo wa nchi hiyo uliosababisha maafa Yanukovich alikimbilia mashariki ya Ukraine kutoka mji mkuu wa Kiev.Maafisa wa forodha walimzuwiya wakati alipojaribu kuondoka nchini kwa ndege katika mji wa Donetsk hapo Jumamosi.

Mahali alipo Yanukovich kitendawili

Mbunge wa upinzani Volodymm Kurennoy amesema kwenye ukurasa wake wa Facebook kwamba alikuwa na taarifa zisizothibitishwa kwamba rais huyo amekamatwa huko Crimea.

Mtandao wa habari wa Ukraine wa portal liga umeripoti kwamba wakaazi wa Sevastopol wamemuona Yanukovich akiwa pamoja na wanamaji wa Urusi.Madai hayo hayakuweza kuyakinishwa.

Hali ya mvutano imekuwa ikizidi kuongezeka huko Crimea ambapo wanasiasa wanaoiunga mkono Urusi wamekuwa wakiandaa maandamano na kuunda vikosi vya kuandamana na kudai mamlaka ya kujiamulia mambo yao kutoka serikali ya Ukraine.Urusi ina kambi kubwa ya wanajeshi wa majini huko Crimea ambayo imeimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili kwa miongo miwili.

Rais wa mpito wa Ukraine Alexander Turtschinow.
Rais wa mpito wa Ukraine Alexander Turtschinow.Picha: picture-alliance/Itar-Tass/Maxim Nikitin

Rais wa mpito Oleksander Turchynov amewahimiza wabunge kukubaliana juu ya baraza la mawaziri litakaloaminika na taifa na serikali ya mseto kufikia Jumanne.

Wakati uongozi wa mpitio nchini humo ukiahidi kuirudisha tena nchi hiyo kwenye mkondo wa kujiunga na Umoja wa Ulaya baada ya kumuondowa Yanukovich aliyekuwa akipendelea mahusiano na Urusi,Marekani imeoinya Urusi dhidi ya kutuma vikosi vyake nchini humo.

Kaimu rais wa nchi hiyo amesema viongozi wapya wa Ukraine wanataka uhusiano mpya na Urusi uzingatie usawa na ujirani mwema na pamoja na chaguo la Ukraine.

Msaada wa uchumi

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton leo anatazamiwa kwenda Ukraine ambapo anatarajiwa kujadili hatua za kuimarisha uchumi wa nchi hiyo unaozorota.

Kijana aliyejifunika bendera ya Ukraine wakati wa maombolezo ya watu waliouwawa katika ghasia Kiev.(23.02.2014).
Kijana aliyejifunika bendera ya Ukraine wakati wa maombolezo ya watu waliouwawa katika ghasia Kiev.(23.02.2014).Picha: picture alliance / AP Photo

Maafisa wa Umoja wa Ulaya wamependekeza kutowa msaada wa kifedha kwa serikali mpya na kufufuwa makubaliano ya biashara ambayo Yanukovich aliyakacha kutokana na shinikizo la Urusi na ndio yaliosababisha maandamano yaliopelekea kuanguka kwake. Marekani pia imesema itaisaidia nchi hiyo kupitia shirika la Fedha la Kimataifa IMF.

Urusi hapo jana imesema imemwita nyumbani balozi wake kutoka Ukraine kwa mashauriano juu ya hali kuendelea kuwa mbaya mjini Kiev.

Inahofiwa kwamba ombwe la madaraka nchini humo linaweza kuepelekea kugawika nchi hiyo kati ya upande unaounga mkono Umoja wa Ulaya na unounga mkono Urusi.

Mwandishi: Mohamed Dahman/Reuters/AP/dpa

Mhariri:Yusuf Saumu