1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

RAMALLAH : Matumaini kufikiwa makubaliano ya amani

5 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/C79j

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleezza Rice na Rais Mahmoud Abbas wa Wapalestina leo hii wameelezea matumaini yao kwamba makubaliano ya amani ya Mashariki ya Kati yanaweza kufikiwa kabla ya Rais George W. Bush wa Marekani kuondoka madarakani.

Rice amelezea matumaini yake kwamba mkutano ujao wa amani ya Mashariki ya Kati utakaofanyika nchini Marekani utakuwa jukwaa la kuzinduwa mazungumzo kati ya Israel na Wapalestina yatakayopelekea kuundwa kwa taifa la Palestina.

Rice alikuwa anazungumza mjini Ramallah kufuatia mkutano wake na Abbas na viongozi wengine waandamizi wa Wapalestina katika ziara yake ya nane Mashariki ya Kati mwaka huu katika jaribio la kuendeleza juhudi za kufufuwa mazungumzo kamili ya amani baada ya mazungumzo hayo kukwama kwa miaka saba.

Abbas amepongeza kujizatiti kwa Bush na Rice kufikia makubaliano ya amani kabla ya kumalizika kwa utawala wa sasa wa Marekani wa Rais Bush hapo Januari mwaka 2009.