1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rene Ngongo wa Kongo ameshinda zawadi mbadala ya Nobel

Oumilkher Hamidou13 Oktoba 2009

Zawadi mbadala ya Nobel wametunukiwa wanaharakati wanne,wa kutoka jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo,New-Zealand,Australia na Canada

https://p.dw.com/p/K5Mq
Muanzilishi wa tuzo ya "Haki ya kuendelea kuishi" Jakob von UexkullPicha: AP

Wanaharakati wanne akiwemo René Ngongo wa Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo wametunukiwa kwa pamoja zawadi mbadala ya Nobel kwa mwaka huu 2009-ijukanayo kama "haki ya maisha bora".

Sababu kuu iliyotangulizwa mbele katika kuteuliwa washindi wa tuzo ya zawadi mbadala ya Nobel kwa mwaka huu wa 2009 ni "juhudi za kuendeleza maisha" amesema mkurugenzi wa wakfu wa pamoja wa Ujerumani na Sweeden wa haki ya kuendelea kuishi, Ole von Uexkull.

Alyn Ware wa Nezealand,Rene Ngongo wa jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo na David Suzuki wa Canada watagawana zawadi hiyo pamoja na mtaalam wa fizikia aliyezaliwa Australia Catherine Hamlin.Wametuzwa zawadi hiyo mbadala ya Nobel kwa kampeni zao dhidi ya silaha za kinuklea,hifadhi ya misitu ya mvua katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo, kuwatanabahisha watu juu ya hatari ya mabadiliko ya hali ya hewa na kampeni kwaajili ya afya ya wakinamama.

Ware,Ngongo na Hamlin,kila mmoja atapokea kitita cha Yuro 50 elfu (sawa na dala 73 elfu za kimarekani) huku David Suzuki akikabidhiwa tuzo ya heshma kwa mchango wake mkubwa katika kuwatanabahisha watu watambue hatari za kuchafuliwa hali ya hewa na jinsi ya kupambana na hali hiyo.

Akitangaza majina ya washindi wa tuzo mbadala ya Nobel kwa mwaka huu wa 2009 mkurugenzi wa wakfu wa "Haki ya kuendelea kuishi" Ole von Uexkull amesema:

"Hasa mshindi wa kutoka Kongo ambae kwasasa anazidi kutiwa vishindo tangu na wanaviwanda wanaotengeneza mbao mpaka na serikali,anaamini hii ni hatua muhimu katika kuunga mkono juhudi zake na ni kinga pia kwake yeye binafsi."

Alternative Nobelpreise für Klimaschützer
Mwanaharakati wa mazingira René NgongoPicha: DPA

Rene Ngongo,aliyezaliwa mwaka 1961, ametunukiwa kutokana na moyo wake wa kijasiri katika kukabiliana na wale wanaovuruga misitu ya joto katika jamahuri ya kidemokrasi ya Kongo na pia kutokana na juhudi zake za kupigania uungaji mkono wa kisiasa katika kuilinda na kuihifadhi misitu.

Alyn Ware amesifiwa kwa mchango wake wa kuimarisha amani nchini New-Zealand ikiwa ni pamoja na kuratibu muongozo wa mafunzo ya amani unaotumika shuleni nchini humo.

David Suzuki wa Canada amesifiwa kwa kuhimiza watu watambue hatari za mabadiliko ya hali ya hewa.

Na mzaliwa wa Australia Catherine Hamlin amesaidia kuwapatia tiba,matumaini mema na hishma maefu ya wakinamama wasiojimudu kifedha barani Afrika.

Tuzo ya "haki ya kuendelea kuishi" imeanzishwa mwaka 1980 na mfadhili wa Sweeden mwenye asili ya kijerumani Jacob von Uexkull.

Zawadi hizo ambazo hazina mafungamano na tuzo ya amani ya Nobel inayotolewa kwa niaba ya tajiri mkubwa wa Sweeden,Alfred Nobel,zitatolewa wakati wa sherehe maalum katika bunge la Sweeden December nne ijayo.

Jumla ya wagombea 82 kutoka nchi 46 waliorodheshwa kupigania zawadi hiyo mwaka huu.

Mwandishi:O.Hamidou/dpa/AFP

Mhariri:Abdul-rahman