1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rice afanya ziara fupi Pakistan

Sekione Kitojo4 Desemba 2008

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani amekuwa na ziara ya saa chache nchini Pakistan ambako amewasilisha ujumbe wa kuchukuliwa hatua kali dhidi ya ugaidi.

https://p.dw.com/p/G94v
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Condoleezza Rice akizungumza na waziri wa mambo ya kigeni wa Pakistan Shah Mehmood Qureshi wakati wa ziara ya Rice ya muda mfupi nchini Pakistan.Picha: AP

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Condoleezza Rice ameitaka Pakistan leo kuchukua msimamo mkali dhidi ya magaidi baada ya mashambulio ya wiki iliyopita mjini Mumbai wakati wa ziara yake iliyotayarishwa kwa haraka mjini Islamabad.


Katika hatua tete ya kuleta uwiano, Rice alikutana na viongozi wa India siku moja kabla mjini New Delhi, ambako alitoa wito wa kujizuwia katika jitihada za kuzuwia hali ya wasi wasi baina ya nchi hizo jirani zenye silaha za kinuklia. Kitisho cha dunia cha watu wenye imani kali na ugaidi kinapaswa kushughulikiwa na mataifa yote, wakichukua msimamo mkali, na hicho ndio nitakachojadili, Condoleezza Rice amewaambia waandishi wa habari wakati akiondoka mjini New Delhi kuelekea Islamabad.

India imelenga shutuma zake kwa makundi yenye makao yao nchini Pakistan kutokana na mashambulio yaliyofanywa na makundi ya watu wenye silaha ambapo watu 171 wameuwawa ikiwa ni pamoja na Wamarekani sita, katika mji wa kibiashara wa Mumbai.

Maafisa wa Marekani pia wamelaumu makundi hayo yenye makao yao nchini Pakistan.

Pakistan inapaswa kuamua itakavyochukua hatua. Inahitaji kuchukua hatua kali na inapaswa kuwa na uwezo wa kufanyakazi, Rice amesema.

Rice kwanza alikutana na mkuu wa jeshi jenerali Ashfaq Kayani katika makao makuu ya jeshi mjini Rawalpindi, mji uliokaribu ya Islamabad. Kisha alikwenda kwa ajili ya mazungumzo na rais wa Pakistan Asif Ali Zardari na waziri mkuu Yousif Raza Gilani, viongozi wa serikali ya kiraia yenye umri wa miezi minane sasa.

Hakuna mtu anayeweza kufikiria kile kilichotokea mjini Mumbai, Gilani amemweleza Rice, akimhakikishia kuwa serikali yake ina mtazamo unaochukuliwa na watu wote katika kupambana na ugaidi.

Hili lilikuwa shambulio baya kabisa na haliwezi kuruhusiwa kutokea tena, Rice amemwambia waziri wa mambo ya kigeni Shah Mehmood Qureshi kabla ya kukutana na Gilani.

Barabara zilifungwa na hakuna watu walioruhusiwa kutembea barabarani mbali na walinzi wa usalama wakijipanga kandoni mwa barabara wakati mlolongo wa magari katika msafara wake yakipita katika miji miwili hiyo ambayo imo katika wasi wasi kila siku wa mashambulizi ya wapiganaji wanaohusika na makundi ya Taliban na al-Qaeda.

Rice alipangiwa kuwapo nchini Pakistan kwa muda wa saa chache tu.

Mvutano baina ya nchi mbili hizo hasimu unaweza kuharibu juhudi za kuleta uthabiti nchini Afghanistan na pia mapambano dhidi ya kundi la kigaidi la al-Qaeda.

►◄