1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rice awasili Nairobi

18 Februari 2008
https://p.dw.com/p/D9Ch

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice, amewasili mjini Nairobi Kenya hii leo ili kushinikiza ugavi wa madaraka kati ya serikali na upinzani nchini humo.

Katika ziara yake hiyo Condoleezza Rice atafanya mazungumzo rasmi na viongozi wanaohasimiana ili kumuunga mkono aliyekuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, katika juhudi za kusaka makubaliano yatakayoumaliza mgogoro wa kisiasa nchini Kenya.

Bi Rice atakutana na Kofi Annan katika hoteli moja mjini Nairobi.

Kofi Annan, ambaye amekuwa akiongoza mazungumzo kati ya rais Mwai Kibaki na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, alisema jana kwamba makubaliano ya kuumaliza mzozo wa kisiasa nchini humo yanakaria kufikiwa.

Serikali ya rais Mwai Kibaki jana ilitoa taarifa ikisema haitakubali shinikizo la kuitaka ikubaliane na Raila Odinga.

Machafuko yalizuka nchini Kenya baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa tarehe 27 mwezi Disemba mwaka jana, ambapo watu zaidi ya 1,000 waliuwawa.

Rais Kibaki alitangazwa mshindi wa uchaguzi na tume huru ya uchaguzi lakini kiongozi wa upinzani Raila Odinga bado anashikilia kuwa uchaguzi huo ulikumbwa na udanganyifu.