1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti juu ya kuteswa watuhumiwa wa ugaidi Guantanamo

Abdu Said Mtullya9 Desemba 2014

Kamati ya seneti ya Marekani inayoshughulikia masuala ya upelelezi inatarajia kuchapisha ripoti juu ya mbinu zilizotumiwa na shirika la ujasusi CIA katika kuwahoji watuhumiwa wa ugaidi kwenye jela ya Guantanamo.

https://p.dw.com/p/1E1cQ
Wafungwa kwenye jela ya Guantanamo
Wafungwa kwenye jela ya GuantanamoPicha: Getty Images/J. Moore

Msemaji wa Ikulu ya Marekani ameeleza kuwa serikali inadhamiria kuhakikisha kwamba ripoti hiyo inachapishwa ili kuyaonyesha maadili ya Marekani.

Maudhui ya ripoti hiyo yanajumuisha habari za kina juu ya vitisho vya kuwadhalilisha mahabusi kingono na juu ya mbinu za kikatili zilizotumiwa na shirika la ujasusi la Marekani CIA katika kuwahoji watuhumiwa wa ugaidi waliokamatwa baada ya mashambulio ya kigaidi ya tarehe 11 mwezi septemba mwaka 2001 nchini Marekani.

Mwenyekiti wa kamati ya seneti inayoshughulikia masuala ya ujasusi Dianne Feistein amesema ripoti hiyo pia inaelezea jinsi mwanachama mmoja wa mtandao wa al -Qaeda alivyotishiwa na kekee ya umeme iliyokuwa imewashwa. Mtu huyo Abdel Rahman al Nashiri alituhumiwa kuliongoza shambulio la bomu lililofanywa kwenye manowari ya Marekani USS Cole, mnamo mwaka wa 2000.

Utawala wa Obama wataka ripoti ichapishwe

Licha ya madai hayo utawala wa Obama umesema unadharimia kuhakikisha kwamba ripoti hiyo inachapishwa.Msemaji wa Ikulu Josh Earnest ameeleza kwamba wanataka kuhakikisha kuwa ripoti hiyo inachapishwa na kwamba mambo yatawekwa wazi ili kuyaonyesha maadili ya Marekani. Amesema lengo ni kuhakikisha kwamba mambo kama hayo hayatokei tena

Lakini wabunge kadhaa wa chama cha Republican wamesema kuchapishwa ripoti hiyo kunaonyesha uzembe na hali ya kutowajibika.

Ripoti ya kamati ya Seneti ya Marekani pia inaelezea kwa kina jinsi mahabusi mmoja alivyotishiwa kudhalilishwa kingono kwa mpini wa ufagio.

Wasiwasi juu ya kutokea mashambulio

Kutokana na wasi wasi wa kutokea malalamiko duniani kote juu ya madai ya mateso waliyofanyiwa mahubusi, baada ya kutolewa ripoti hiyo, Ikulu ya Marekani na maafisa wa idara ya ujasusi wameuimarisha ulinzi wa sehemu zote zenye maslahi ya Marekani duniani kote.

Katika tamko lao Maseneta Marco Rubio na Jim Risch wametahadharisha kwamba kuchapishwa ripoti hiyo kunaweza kuyahatarisha maisha ya Wamarekani waliopo nchi za nje, pia kunaweza kuathiri uhusiano wa Marekani na washirika wake duniani, pamoja na kuchochea matumizi ya nguvu ,kusababisha matatizo ya kisiasa kwa washirika wa Marekani na kutumiwa ripoti hiyo na maadui wa Marekani .

Ripoti hiyo iliyochukua miaka mingi kuitayarisha inaonyesha historia ya mpango wa CIA wa kuwateka nyara watuhumiwa,kuwaweka mahabusu na kuwahoji-mpango ulioidhinishwa na Rais wa hapo awali George Bush ,baada ya kutokea mashambulio ya tarehe 11 mwezi Septemba.

Mwandishi:Mtullya Abdu/rtre,afp

Mhariri: Yusuf Saumu