1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia yashindwa kudhibiti uzalishaji gesi chafu

9 Agosti 2021

IPCC imetahadharisha kuwa viongozi duniani watashindwa kutekeleza ahadi zao za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi hadi pale watakapofanya uamuzi wa haraka wa kupunguza pakubwa uzalishaji wa gesi chafu.

https://p.dw.com/p/3ykEo
Waldbrände in Griechenland Euböa
Picha: Petros Karadjias/dpa/AP/picture alliance

Ripoti ya jopo la Wataalamu wa Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC) iliyochapishwa siku ya Jumatatu (Agosti 9) ilisema uchafuzi unaotokana na gesi ya kaboni umepanda kwa kiwango kikubwa duniani kinachotishia kuvuruga mpango wa kukabiliana na athari ya mabadiliko ya tabianchi, wa kuweka viwango vya joto ulimwenguni kusalia nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha Celsius kufikia mwishoni mwa karne hii, na kwamba kiwango hicho kitaongezeka ndani ya kipindi cha miaka 15 ijayo.

Ripoti hiyo iliyoidhinishwa na wajumbe kutoka nchi 195 imechapishwa katika wakati ambapo joto kali na mvua kubwa vinashuhudiwa katika mataifa mbalimbali duniani.

Soma zaidi: Maelfu wazikimbia nyumba zao kuepuka moto wa msituni Ugiriki

Hali hiyo ya hewa inachora picha kamili ya jinsi dunia ilivyoathirika na mabadiliko ya tabia nchi.

“Hii ndio hali halisi ilivyo,” amesema Valerie Masson-Delmotte, mmoja wa wenyekiti wa jopo la watalaamu wa mabadiliko ya tabia nchi waliyoiandaa ripoti hiyo.

Kwa kuchoma mafuta na kutoa gesi chafu hewani, viwango vya joto duniani vimeongezeka kwa karibu nyuzi joto 1.1 katika kipimo cha Celsius.

Jinsi hewa chafu inavyoongezeka

Kwa mujibu wa ripoti ya IPCC, hali hiyo imechangia kwa kiasi kubwa kuongezeka kwa mvuke na mvua kubwa. Pia vimbunga na upepo mkali vimeongezeka katika sehemu mbalimbali duniani kote.

Katika baadhi ya sehemu duniani, viwango vya ukame vimeongezeka na kufikia kiwango cha kutisha.

Tangu ripoti ya mwisho ya IPCC ya mwaka 2014, wanasayansi wamebaini kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi zimechangia kwa kiasi kikubwa moto, mafuriko na hata vimbunga vinavyoshuhudiwa katika sehemu tofauti tofauti duniani. 

Deutschland Überflutung Bad Neuenahr-Ahrweiler  Aufräumarbeiten
Mafuriko ni miongoni mwa athari za moja kwa moja za mabadiliko ya tabianchiPicha: Arafatul Islam/DW

Soma zaidi: Watu 100 waokolea Uturuki kufuatia tetemeko la ardhi

Wasayansi wanasema kuwa, suluhu ya haya yote ni rahisi-kuacha kuchoma mafuta na kutoa gesi chafu hewani lakini serikali, wafanyibiashara na hata watu wa kawaida wanashindwa kufanya hivyo ilhali wengine wanaofanya, wanajikokota.

Kwa mujibu wa shirika la utafiti la Ujerumani la Climate Action Tracker, licha ya nchi kadhaa zilizojiunga kwenye mkataba wa Paris wa kupambana na mabadiliko ya tabia nchi, kutangaza kuahidi kupunguza uzalishaji wa gesi ya ukaa, viongozi hao wanaonekana kwenda kinyume na ahadi walizotoa na badala yake wanafuata sera ambazo zinatishia kuongeza kiwango cha joto hadi nyuzi joto 3.