1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya mauzo ya silaha za Ujerumani

Elizabeth Shoo31 Januari 2013

Kila mwaka serikali ya Ujerumani inatoa ripoti juu ya silaha za kivita zilizouzwa nje ya nchi. Hata hivyo zipo taarifa nyingi muhimu kuhusu uuzaji wa silaha ambazo hazikutajwa katika ripoti ya mwaka huu.

https://p.dw.com/p/17V12
Kampfpanzer Leopard 2 A4 während einer Militärübung, Objekte; 2002 , Lehrvorführung der Kampftruppenschule Münster , Bundeswehr , Armee , Heer , Gefechtsfahrzeuge-Lehrübung , Gefechtsfahrzeug , militärische Übung , Militärübung , Manöver , Panzertrupp , Panzertruppe , A 4 , Panzer; , quer, Kbdig, Einzelbild, Freisteller, Fahrzeuge, Deutschland, Aktion, Militaer, Staat, Ohne, Niedersachsen
Kampfpanzer Leopard 2 A4Picha: imago

Kwanini silaha zilizotengenezwa hapa Ujerumani mara kwa mara zinakutikana katika maeneo yenye vita? Ni swali wanalojiuliza wengi kwani serikali ya Ujerumani imetangaza kwamba inadhibiti uuzaji wa silaha zake na kukataza kabisa uuzaji wa silaha katika nchi zisizozingatia kikamilifu haki za binadamu na kwenye maeneo yaliyo katika hatari ya kutumbukia vitani. Uuzaji wa silaha zozote za vita nje ya nchi lazima upewe kwanza kibali na serikali ya Ujerumani.

Lakini licha ya hayo, waasi nchini Libya walipopigana kumwondoa Muammar Gaddafi madarakani mwaka 2011 walitumia bunduki zilizotengenezwa hapa Ujerumani. Silaha hizo zilifikaje Libya? Bunduki hizo aina ya G36 haziwezi kuwa zimetoka katika akiba za jeshi la Ujerumani kwani jeshi huteketeza silaha zisizotumika. Na watengenezaji wa silaha pia wamekana kuuza bunduki Libya.

Waasi wa Libya wakiwa katika mji wa Sabha
Waasi wa Libya wakiwa katika mji wa SabhaPicha: Reuters

Anayetarajia kwamba ripoti ya mwaka huu juu ya uuzaji wa silaha nje ya nchi itajibu maswali kadhaa hatoridhishwa na kile kilichoandikwa ndani ya ripoti hiyo. Mtaalamu wa masuala ya silaha kutoka kituo cha kimataifa cha utafiti wa amani na migogoro mjini Bonn, Bwana Jan Grebe, anafafanua mambo ambayo hayakutajwa katika ripoti. "Ripoti ya silaha haielezei kwa namna yoyote ile kampuni gani iliuza silaha kwa nchi gani kwa wakati gani. Kuna tofauti kati yetu na nchi jirani kama Italia ambapo ripoti zinataja pia makampuni yaliyotengeneza silaha."

Serikali kufaidika na mauzo

Ripoti ya mauzo ya silaha inaorodhesha nchi zinaziruhusiwa kununua silaha zilizotengenezwa hapa Ujerumani. Hata hivyo, haielezwi iwapo nchi hizo zilinunua silaha au la. Pamoja na hayo, hakuna maelezo ya kina juu ya aina ya silaha na vifaa vinavyouzwa. Ripoti inataja magari, vifaa vya elektroniki, risasi, bunduki na mahitaji mengine ya kijeshi.

Bunduki aina ya G36 iliyotengenezwa na kampuni ya Heckler und Koch
Bunduki aina ya G36 iliyotengenezwa na kampuni ya Heckler und KochPicha: picture-alliance/dpa

Serikali ya Ujerumani kwa upande wake imesema kwamba ripoti yake inatoa maelezo ya kutosha. Wizara ya uchumi imeiambia DW kwamba majina ya makampuni yanayotengeneza silaha hayawezi kutajwa kwa sababu za kisheria.

Si makampuni ya Ujerumani tu yanayouza silaha za kijeshi bali hata serikali yenyewe. Nyaraka za serikali zinadhihirisha kwamba mwaka 2011 vifaru, risasi na vifaa vingine vyenye thamani ya takriban Euro milioni 11 viliuzwa kwa Brazil, Chile, Denmark, Canada na Sweden. Mwaka 2010, Ujerumani iliihakikishia Uturuki kwamba inaweza kununua vifaru 56 vya kijeshi vyenye thamani ya zaidi ya Euro milioni 13. Mapato yatokanayo na mauzo ya silaha hizo huingizwa kwenye bajeti ya serikali.

Mwandishi: Alexander Richter

Tafsiri: Elizabeth Shoo

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman