1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya SIPRI- matumizi ya kijeshi yaongezeka duniani

Sekione Kitojo
29 Aprili 2019

Matumizi ya kijeshi duniani yamefikia kiwango chake cha juu mwaka jana katika muda wa miongo mitatu, kwa kiasi kikubwa hali hii  imesababishwa na Marekani na China, imesema ripoti ya SIPRI leo Jumatatu(29.04.2019).

https://p.dw.com/p/3HbNN
F-22 'Raptor' Kampfjet
Picha: picture-alliance/dpa/J. Heon-Kyun

Taasisi  ya  kimataifa  ya  utafiti  wa  amani  mjini  Stockholm (SIPRI) imekadiria  kwamba  matumizi  ya  dunia  ya  kijeshi  yamefikia  jumla ya  dola  za  Marekani  trilioni 1.8 katika  mwaka  2018, ikiwa  ni  juu kwa  asilimia  2.6  kutoka  mwaka  2017.

Idadi  hiyo inatafsirika kuwa  ni  sawa  na  dola 239 kwa mtu  mmoja, kwa  mujibu  wa  SIPRI. Marekani  imebakia  kuwa  nchi  ya  kwanza duniani  kwa  matumizi  makubwa  ya  kijeshi  kwa  kutumia dola bilioni 649, ikiwa  ni  ongezeko kutoka  mwaka  mmoja  uliopita  la asilimia 4.

Symbolbild: Unbekannte greifen Stützpunkt in Mali an
Mataifa mengi yamejilimbikizia silaha mwaka 2018Picha: picture-alliance/dpa/T. Bindra

„Ongezeko  hilo katika  matumizi  ya  Marekani  limesababishwa  na utekelezaji  kutoka  mwaka  2017  wa  mipango  mipya  ya  ununuzi wa  silaha  chini  ya  utawala  wa rais  wa  Marekani Donald Trump," amesema  Aude Fleurant , mkurugenzi wa  mpango wa  SIPRI wa matumizi  ya  jeshi na ununuzi wa  silaha.

Marekani imechangia jumla  ya  asilimia 36 ya  matumizi  yote  ya dunia katika  mwaka  2018, na  ilitumia  karibu kiasi  kama hicho kwa  jumla  ya  mataifa  mengine  manane  yaliyofanya  manunuzi  ya juu, SIPRI imesema. Hata  hivyo, matumizi  ya Marekani  yalikuwa karibu  moja  ya  tano  chini kuliko matumizi  yake  ya  juu  kabisa mwaka  2010.

Matumizi  ya  nchi  iliyoshika  nafasi  ya  pili  China  yalikadiriwa kuwa  dola  bilioni 250, ikiwa  sawa na  asilimia 14 ya  matumizi  yote ya  dunia.

Matumizi  hayo  yalikuwa yameongezeka  kwa  asilimia  5 katika mwaka 2018, ikiwakilisha  ongezeko  la  chini  la  China  kwa  mwaka tangu  mwaka 1996 na  linaakisi  ukuaji wa taratibu  wa   uchumi.

Minigun Stand MG Symbolbild Waffenexporte
Mataifa mengi yamenunua silaha ili kujihami na kuwa na silaha bora zaidiPicha: picture-alliance/dpa/J. Lo Scalzo

„Ongezeko  la  matumizi ya  kijeshi  kwa  China  linafuata  ukuaji jumla  wa  uchumi  wa  nchi  hiyo," mtafiti wa SIPRI  Nan Tian amesema.

Saudi Arabia  imebaki  katika  nafasi  ya  tatu kwa  kutumia dola bilioni 67.6, licha  ya  kupunguza  matumizi ya  asilimia  6 ikilinganishwa  na  mwaka  2017, ikifuatiwa  na  India  na  Ufaransa. Akizungumza na DW mkuu huyo wa kitengo cha utafiti katika  SIPRI Nan Tian  alisema hata hivyo  kuwa  matumizi  haya sio mashindano ya silaha:

 

O-Ton Nan Tian:

"Siwezi kusema ni mashindano ya silaha, lakini  nchi hizi bila shaka zinaendelea kujihami kwa silaha mpya na zilizobora zaidi na  zenye uwezo mzuri zaidi. Na silaha hizi mara nyingi ni  ghali sana."

Matumizi  ya  India  yameongezeka  kwa  mwaka  wa  tano  mfululizo, kwa  kiasi  hali  hiyo kikubwa  ikisababishwa  na hali  ya wasi  wasi na  China  na  Pakistan, kwa  mujibu wa  taasisi  hiyo. Mataifa matano  ya  juu  watumiaji  wakuu yamechangia  asilimia  60 ya matumizi  yote kijeshi  duniani.

Unterseeboot U32 der Klasse 212A
Nyambizi ya chini ya bahari chapa U32 ya daraja 212APicha: picture-alliance/dpa/PIZ Marine/R. Schönbrodt

Urusi imeporomoka hadi  katika  nafasi  ya  sita, ikitumia  kiasi kinachokadiriwa  kufikia  dola  bilioni 61.4. Hii  ni  mara  ya  kwanza kwa  Urusi  kutokuwa  miongoni  mwa  nchi tano za  juu zenye matumizi  makubwa tangu mwaka  2006. SIPRI imeongeza kuwa matumizi ya  Urusi bado yalikuwa  juu  kwa  robo ikilinganishwa  na mwaka  2009.

Mataifa 10 ya juu  yaliyotumia  fedha  nyingi kwa ajili ya  jeshi ni pamoja  na  Uingereza, Ujerumani, Japan na Korea  kusini.

Kwa utaratibu wa  jumla kwa mujibu  wa  SIPRI ni kwamba matumizi kwa  ajili  ya  jeshi kama  sehemu ya  pato  jumla  la  taifa yamepungua  katika  kanda  zote  tangu  mwaka 1999.

SIPRI imesema  kwamba  sita kati  ya  mataifa  10  ambayo matumizi  ya  jeshi  yanakadiriwa  kuchukua  sehemu  kubwa  ya pato jumla  la  taifa GDP,ambayo  pia  yanaelezwa  kuwa  jeshi ni mzigo, yanapatikana  katika  mashariki  ya  kati.

Maschinenpistolen des Typs MP5
Silaha za kisasa zimenunuliwa na mataifa mbali mbali dunianiPicha: picture-alliance/dpa

Mataifa hayo ni  pamoja  na  Saudi Arabia katika  asilimia 8.8, Oman katika  asilimia 8.2, na Israel katika  asilimia 4.3.

SIPRI imesema  kinashindwa  kupata  data  kutoka  mataifa  kadhaa ikiwa  ni  pamoja  na  Syria, Umoja wa  falme za  Kiarabu, Qatar na Yemen. Lakini  kwa  mujibu wa  data zilizopo , mzigo wa  jeshi  katika mashariki  ya  kati  ni  asilimia  4.4 ya  pato jumla  la  taifa. Barani Ulaya  mzigo wa  jeshi  uko katika  wastani wa  asilimia 1.6, kiasi kidogo chini  ya  Afrika na  maeneo  ya  Asia  na  mataifa ya  bahari ya Pacifiki.